Sunday, June 15, 2008

MAKALA HII YA DEMOKRASIA KAMA KIPINDI MAALUM KATIKA REDIO

MAKALA hii imeandaliwa maalum ili iweze kutumika katika kipindi cha redio za Kiswahili ulimwenguni.

Lengo lake ni kutathmini maendeleo na matatizo ya demokrasia Afrika katika kipindi cha takriban miaka 20 hivi. Na hili linaweza kufanywa vizuri zaidi kama litafanyika kwa njia ya mjadiliano ndani ya studio kwa ushirikiano na mwandishi na mabingwa au wanataaluma wa demokrasia popote pale walipo duniani.

Mwandishi amejaribu kuainisha maeneo kama 19 hivi ambayo anadhani kuna matatizo na kama yakishughulikiwa ipasavyo basi Afrika inaweza kuwa na demokrasia safi na bora zaidi.

Muda wa kujadili mada hizi kwa ukamilifu na kwa undani zaidi unapendekezwa kuwa kati ya wiki nane na wiki 14.

Muundo wa kipindi utaanza kwa walioko studio kusoma sura moja au mbili kwenye Blogi na kisha kuanza kujadili kwa kuvuta mawazo ya wasikilizaji na wachangiaji kwenye yale yanayotakiwa kufikiwa mwisho wa kipindi kwa maana wote kukubaliana kwamba hilo ni tatizo na njia zilizopendekezwa zinafaa au hata pia kuongeza mawazo juu ya kibunifu kuhusu ufumbuzi wa tatizo au matatizo yaliyozungumzwa.

Sehemu ya pili itahusika zaidi na kupata ufafanuzi wa mawazo ya mwandishi na nini hasa ujumbe wake katika sehemu husika.

Sehemu ya tatu itakuwa ni kuachia jopo la wataalamu kuchangia mawazo yao kwa kukosoa au kuongeza vipengee vipya vitakavyochangia kuifanya blogi hii kuboreshwa zaidi kwa malengo ya hatimaye kuwa na kijitabu kuhusu DEMOKRASIA NA AFRIKA baada ya miaka 20.


Sammy Makilla
Barua-pepe: smakilla@out.ac.tz+255-732-929832

1. Demokrasia na Tume Huru za Uchaguzi

DEMOKRASIA ilipoingia Afrika ilichukuliwa kama vile ilikuwa ni mtoto wa chama tawala na serikali iliyopo madarakani. Pengine hali iliyokuepo wakati huo [ya mzazi kukosa mkunga wa kumzalisha] ndio iliyochangia kuwa na hali kama hii.

Mwana keshapatikana, hata hivyo, je, kweli tunastahili kuendelea kama tulivyokuwa tukifanya huko nyuma au tubadilike kwa kuzingatia mahitaji ya wakati tulio nao?

Haiwezekani kamwe kuwa na Tume ya Uchaguzi inayochaguliwa na chama tawala na serikali iliyopo ambayo itaonekana kutenda haki kwa wote siku zote. Hili ni kutokana na ukweli kuwa lazima mwana amheshimu mzazi. Na ni zaidi ya hapo kwa yakini, maana hao wanaopewa nafasi hiyo wanajihesabu kama wamelishwa fadhila na huyo aliyewachagua.

Ndio maana tunapendekeza ima fa ima lazima Tume za Uchaguzi Afrika zichaguliwe kutoka kwenye watu ambao hawafungani na upande wowote wa kisiasa. Ikizingatiwa kwamba uchaguzi ndio unaotupa wabunge na wabunge ndio wanaotakiwa kuwakilisha wananchi bungeni basi kwa mantiki hiyo ni lazima vile vile yale makundi ya kijamii yanayoweza kuitwa washikadau yawe na nafasi katika kuwapendekeza wale inaoamini kuwa watasimamia uchaguzi bila kupendelea upande wowote.

Kuwa na Tume ya Uchaguzi ambayo ina huruma na huba kwa serikali iliyoko madarakani na chama tawala hakuashiria mema kwa nchi inayotaka kujenga demokrasia ya kweli na yenye amani na manufaa kwa watu wake.

Tunaamini kwamba kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ni mwanzo wa kuondokana na tuhuma mbalimbali zinazoambatana na uchaguzi na pia ni msingi wa demokrasia madhubuti na yenye tijara kwa wananchi wa nchi hii. Kuna nchi kadhaa Afrika kati ya zote ambazo zimeweza hili na hakuna sababu ya Tanzania kuwa namba tatu katika jambo kama hili!

Tume Huru ya Uchaguzi itakuwa inawajibika kwa wapiga kura kupitia katiba mpya tarajiwa na sheria za haki kwa mujibu wa maazimio mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, Afrika na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sio kiongozi au chama chochote.

Kama ilivyo kwa Tume kuwa Huru ndivyo inavyostahili pia kwa Watanzania wote kuwa huru katika kupigiwa au kupiga kura ila pale mwananchi huyo anapoamua kufanya hivyo akiwa ndani ya Chama hiki au kile cha kisiasa. Haki ya kuwa huru inastahili kuwepo wakati wote iwe kabla ya kujiunga na chama au baada ya kukiacha chama fulani.
***

2. Demokrasia, Vyombo vya Habari na Jamii

AFRIKA imekuwa kwa miaka mingi ikitumia vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali kama vyombo vya kuwaacha watu wao katika giza kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa.

Demokrasia ya kweli haiwezi kupatikana kama mhimili huu muhimu wa nne hautaheshimiwa na kuacha kufanya kazi zake bila kuingiliwa na mtu yeyote isipokuwa kwa zile sheria na kanuni ambazo vyombo vya habari vimejiwekea kitaifa na kimataifa.

Vyombo vya habari ni walinzi wa demokrasia. Na vikiachiwa kufanya kazi zao bila kuingiliwa au kushawishiwa na walioko au wasioko madarakani vinaweza vikatoa mchango muhimu katika kuwapatia wananchi habari zilizo wekwa katika mizani vyema na kuwaachia wananchi wenyewe wafanye maamuzi kutokana na habari walizo nazo.

Ni ufujaji fedha bure kama vyombo vy a habari viwe vya serikali au chama au watu binafsi vitakuwa vinatumiwa na walioko madarakani ili kufunika ukweli na kupaka nyumba mbovu rangi staii ya wenye simu za mkononi. Kibovu ni kibovu tu, kibaya ni kibaya tu, ukweli ni ukweli tu! Na yule anayeamini kuwa kaitwa mbovu naye ni ngangari; au kaitwa mbaya naye ni mzuri basi akavishtaki vyombo vya habari kwenye mhimili wa tatu, yaani, mahakama.

Juhudi zinazofanywa na serikai nyingi Afrika katika kuvidhibiti vyombo vya habari zinadhihirisha uozo na ubovu wa serikali zinazofanya hivyo katika vita vya kuwaondoa watu wao kutoka kwenye umasikini, ujinga na maradhi.

Ukiachia serikali yoyote kuvidhibiti vyombo vya habari, kuwanyanyasa waandishi wa habari ni kuachia serikali na chama tawala hatimaye kudhibiti watu wote na kuwanyanyasa watu wote na mwisho wa yote kuliingiza taifa husika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na machungu yanayoandamana na hilo.

Hapana sababu yoyote ya Afrika kushindwa kuheshimu na kufanya kazi kwa uelewano mkubwa na vyombo vya habari kwa faida ya wananchi wote.

Mara kadhaa ukiona waandishi na vyombo vya habari vinaandamwa hapa Afrika lazima kuna baya lililonaswa ma walioko madarakani wanatumia fedha za umma kujikosha mbele ya dunia.

Mathalani, mwaka 1994 kuelekea Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi Watanzania toka kampuni ya Business Times Limited walifikishwa mahakamani kwa kosa la uhaini. Kosa lao eti lilikuwa ni kuanika uwazi kuhusu rada mbovu serikali na chama tawala wakati huo vilivyopanga kuinunua. Miaka michache baadaye imegundulika kuwa rada hiyo sio tu ilikuwa mbovu bali pia kuna rushwa iliiyotembezwa na Waingereza hapo pia.

Katika hali kama hii kuwa kwa upande mmoja kuna serikai inayoweza kutumia nguvu za dola kumsingizia mtu uongo na upande wa pili kuna watu walioko tayari kujitoa mhanga ili ukweli ujulikane haiwezekani kwa serikali hiyo hiyo kuwachukulia hatua waandishi au wachapishaji. Lazima apatikane mtu wa tatu kuja kuamua ugomvi huu, maana ugomvi hii ni wa watu wawili--mmoja serikali na mwingine vyombo vya habari ambao wote wana haki sawa katika kutetea haki za umma. Haiwezekani serikali wakati wowote ikaonekana kuwa ni takatifu na wengine ni wachafu labda kama kuna hila fulani inayofichwa na viongozi husika.

Nchi inayotaka kufuata demokrasia ya kweli na ya uhakika; uwazi katika uendeshaji wake; isiyo na jambo la kuficha na inayopigania haki za wengi na sio kundi la wajanja wachache haiwezi kamwe k uhitaji Wizara ya Habari! Maana kazi hii tayari ina wenyewe na tena wanaifanya uzuri sana. Kinachohiajika ni sekta hiyo kuwa kamilifu kwa kuwa na vyombo vyote vya kusimamia na kuendesha mambo yake kwa ufanisi na ufanifu zaidi.
***

3. Demokrasia na kuwapendelea wale wanaokiunga mkono chama tawala

IMEKUWA ni tabia ya kawaida kwa vyama tawala kutoa upendeleo kwa wale wanachama wake na kusahau kabisa kuwa hakitawali tu wanachama wake bali pia na wale wa chama au vyama mbadala.

Hili katika demokrasia ya kweli libadiike. Maana lina madhara makubwa sana kutokana na kuwatenga watu wengi katika kutoa mchango wao kwa maendeleo ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia.

Kwa namna za ajabu inaelekea chama kinachoshinda huwa kinajua ni nani watu wake na nani sio watu wake. Na hapo biashara haramu ya huyu ni mwenzetu na huyu si mwenzetu ndipo inaanza. Ulikuwa na biashara nzuri sasa chama tawala na serikali yake itaiua. Ulikuwa huna chochote sasa chama tawala kwa kuwa ni mwenzao kitahakikisha kwa jino na ukucha unafanikiwa katika mambo yako. Swali, je, kweli hii ni biashara halali? Na kama sio, ikiendelea, itatupeleka wapi?

Ni dhahiri kuwa haiwezekani kuwachukulia wanasiasa wa vyama mbadala kama vile ni maadui na nchi hii ifanikiwe katika mambo yake. Ni lazima tujifunze kuwachukulia wanasiasa wa vyama mbadala kama wenzetu na washirika katika dau la maendeleo ya nchi zetu ili mambo yetu na nafasi zetu wenyewe ziendelee kuheshimika na kutabirika.

Kwa maneno ni muhimu kwa upinzani kutambulika kama pia nao ni viongozi wa taifa na wapewe heshima na haki zote viongozi wanazostahili kadri ya uwezo wa taifa hili.

Kila inapowezekana akili na ubunifu na uzuzi wa wanasiasa wa vyama mbadala visiachiliwe vipotee bure bali vidakwe na kutumika kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya watu na nchi yao.

Sio siri kwamba maendeleo na ustawi wa nchi kama Uingereza na Marekani vinapatikana sio haba kwa kugonganisha akili na ubunifu wa wanasiasa tofauti na kwa serikali ya wakati wowote kutumia kile kilicho bora na sio lazima kile kilichotoka kwa mwanasiasa wao. Hakuna mifano mingi mizuri ya kuiga toka Marekani lakini huu ni mfano bora kuliko yoyote kutoka mahala pengine popote ulimwenguni kuuiga kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu na Afrika kwa ujumla.

Aghalabu katika nchi zilizokosa mwelekeo Afrika ni zile zinazowanunua wanawake na vijana ili watu hao watumike kufanya ghasia dhidi ya vyama mbadala. Tusiruhusu jambo hili kutokea. Badala yake tubuni njia za kuwashirikisha vijana wetu bila kujali chama wanachotokea kuweza kupambana na umasikini wetu katika mazingira ya utandawazi ambao wao wana mengi ya kupoteza kama watatumiwa vibaya na wanasiasa wa nchi zetu.

Mfano wa Zimbabwe, Kenya, Ethiopia na Misri ni mifano ya uahlifu wa kisiasa unaofanyika machoni mwa Afrika na dunia nzima na watu kushindwa kukemea wale wanaotaka kubaki madarakani kwa gharama zote hata kama watakayoacha nyuma ni majivu ya mamilioni ya watu wao. ***

4. Demokrasia, chama tawala, na kutumia wafanyabiashara na mangimeza

KILA inapokaribia uchaguzi mkuu katika nchi ya Kiafrika ndoa za haraka haraka kati ya wafanyabiashara na chama tawala, au mangimeza na chama tawala hufungwa. Matokeo ya ndoa zote hizi ni kuvunjika kila baada ya uchaguzi kwa sababu ahadi huwa siku zote nyingi kuliko uwezo wa mtawala. Na hapo ndipo nchi inapoingizwa kwenye matatizo mengine ambayo nadhani Watanzania wengi sasa watajua ninachokizungumza.

Mpaka pale kutapokuwa na uwazi kuhusu jinsi vyama vya kisiasa, yaani, chama tawala au vyama tawala na vile vya mbdala vinavyopata fedha za kujiendesha na kuendesha uchaguzi mkuu itakuwa ni kazi sana kujenga demokrasia ya kweli Afrika.

Lazima vyama vyote vya siasa viige mfano wa vyama vya SACCOS kwa kuwa na shughuli za kiuchumi na kijamii zinazoweza kuwaingizia sio tu wanachama wao bali washirika wao wengine na wao wenyewe kipato cha kutosha kujiendesha bila kujiingiza katika njia ambazo zinazoweza kuhesabika ni za kiuhalifu na za kiharamia kuliko zile za magaidi wa nje.

Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wengine wa serikali hawatumii nafasi zao kufanya kazi za chama kwa kutumia fedha ya serikali. Hili sio haki na katu lisikubalike katika mwenendo wa demokrasia na uwajibikaji wa wanasiasa.

Aghalabu, hatima ya yote hayo ni kuwa ujanja huo pia huishia kuwa ujanja wa kufanya shughuli binafsi kwa kutumia mali ya umma au ya serikali.

Tumeruhusu kuwa na viongozi ambao ni wanasiasa na wakati huo ni wafanyabiashara lakini hili ni kosa. Ni lazima tulitazame upya jambo hili.
Huwezi ukawa na waziri ambaye ni mfanyabiashara na akaacha kuitumia ofisi yake kujinufaisha katika masuala binafsi. Lazima tuone hili, lazima tujue ukweli huu. Na kwamba wakati umefika wa kuamua mtu ama aolewe au kuoa biashara, au aolewe au kuoa siasa. Basi. Hakuna njia ya kati.

Hili litatuhakikishia wale wanaolipwa mshahara na serikali kuwa saa zote mawazo na moyo wao uko katika kazi waliyopangiwa na sio vinginevyo.
***

5. Demokrasia, sheria na viongozi kuwa juu ya sheria

MIFUMO yetu ya utawala imejengwa kwa namna ambayo kwamba baadhi ya viongozi katika nchi na pengine jamaa zao huonekana kuwa juu ya sheria.

Kwa maneno mengine, wao wakifanya kosa sawa na la mtu mwingine wanaweza wasikamatwe wala kushtakiwa. Hili sio jambo zuri. Kama tumezikubali sheria fulani kuwa ni zetu basi ni lazima bila kujali nafasi, wadhifa au uwezo mtu sheria ifanye kazi sawasawa.

Ni muhimu kuhakikisha kuwa vyombo kama vile polisi na mahakama haviachiwi fursa ya kuuza na kununua haki za watu. Hilo likifanyika utakuwa mwanzo wa mengi mabaya yatakayoiandama nchi yetu. Na hili Mungu alieepushilie mbali. Kwa hiyo tusikubali ukubwa, uroho, uchu na wivu wa wachache miongoni mwetu kutumia mianya inayojitokeza popote pale kuuza au kununua haki ya mtu na hasa katika wakati kama huu ambapo sasa ardhi Tanzania imeanza kuonekana kuwa ni mali!

Demokrasia ya kweli itakuwepo tu pale ambapo kila mahala patatawalia na utawala wa kisheria na sio kinyume cha hivyo.

Kiongozi mzuri sio yule anayejionesha kwa watu bali yule ambaye hata kama haonekani mambo anayoyafanya yanaonekana.

Mara nyingi yule mtu anayetka kuonekana sana, akiwashughulisha watu huku na huko na hasa masuala yake binafsi na yale ya wale wanaomhusu yanapokuwa mengi kamwe hawezi kuwa kiongozi mzuri.

Kubwa katika hili, hata hivyo, ni ile tabia ya wanasiasa kutaka kubadili sheria na katiba ya nchi sio kwa sababu ya maslahi ya wananchi bali kwa sababu watalinda vyeo na nafasi waliyonayo katika jamii. Hili ni lazima likemewe na kupigwa vita na watu na taasisi zozote katika nchi iliyodhamiria kujenga demokrasia ya kweli.
***

6. Demokrasia na kukanyagwa kwa haki za wanyonge na walio wachache.

DEMOKRASIA halali ni ile inayoheshimu na kujali haki na uhuru wa wachache kama inavyowapa wengi nafasi ya kuamua na kuendesha mambo ya serikali.

Wazee, wastaafi. wasiojiweza, vijana na watoto ni lazima walindwe dhidi ya wale wanaoweza kutumia udhaifu wao kuwakandamiza katika jambo hili au lile.


Iwe ni mwiko katika nchi inayokubali demokrasia kuruhusu wanajeshi au polisi kuelekeza mitutu ya bunduki zao dhidi ya wananchi eti kwa sababu tu wanadamana.

Tuirejee katiba na hata ikija katiba mpya haki ya kuandamana iwe ni haki inayotambulika na kuheshimiwa wakati wote angalau kwa kujua hii ndio njia pekee ya kupunguza presha ya watu wenye malalamiko au wasioridhika na maamuzi au hali fulani katika eneo fulani la nchi au jamii.

Ni lazima tukubali kuwa jeshi na polisi, kama vyombo, vyenye watoto, ndugu, jamaa wa Watanzania kamwe havipo kwa ajili ya kuwahujumu ndugu zao bali kuhakikisha haki inatendeka wakati wote. Jeshi na polisi katika Afrika lazima lijengwe katika misingi ambayo kwayo ni yule mwenye haki ndiye anayeipata na asiye na haki asistahili kupata haki isiyo yake.

Vyombo vyetu vya dola lazima visisimuliwe na muamko na mwamsho wa demokrasia na haki za binadamu. Na kama kuna jambo la kujivunia kwa majeshi yetu lazima jambo hilo liwe ni kutetea na kulinda demokrasia daima dawamu.

Yeyote aliye rafiki wa demokrasia atastahili kuwa rafiki yao; na yeyote aliye dhidi ya demokrasia atakuwa ni adui yao. Ndivyo inavyotakiwa, ndivyo inavyostahili kuwa.

Hatuwezi kuwatumia watu wetu katika vyombo vya dola kama vile ndondocha au misukule au midubwana ambayo haijali nani mwenye haki na nani asiye na haki katika kutekeleza majukumu na wajibu wao wa kulinda nchi na watu wake.
Katika Afrika kundi lolote liwe la raia au jeshi linalokiuka haki za binadamu kwa kuua, kubaka na kutesa watu hata iwe kwa sababu gani lazima litengwe na kuonekana ni kundi la waovu. Lazima tuwe na maadili ya kitafia

yatakayodhihirisha pamoja na mambo mengine jinsi gani Watanzania wanatakiwa waishi -iwe katika hali ya ustawi na amani au hali ya kukosa staha na migogoro ya ndani kwa ndani au vita na nchi za nje.
***

7. Demokraia, unyanyasaji wakulima, wanafunzi na vijana

KWA KUKOSA ajenda zinazoeleweka katika kilimo, elimu na ajira wakati mwingine nchi zetu zimeishia pengine bila kujua kufanya maisha yawe magumu sana kwa wakulima, wanafunzi na vijana kwa ujumla.

Ukiangalia kwa undani utakuta katika taasisi zote hizi kuna udikteta unaojificha na unaotumia fursa hiyo kulinda ubinafsi wao na sio kutetea maslahi ya umma mkubwa ulio chini yao.

Ni laizma tubuni mifumo inayofaa kuhakikisha kwamba viongozi katika kata, mashule, vyuo na taasisi zingine wanafanya mambo yao kwa uwazi na kwa namna ambayo inagundua dalili za kuzuka matatizo mapema kabla haayajalipuka na hivyo kuweza kufanya maamuzi yayakayoepusha mizozo na migongano isiyo ya lazima.

Ni lazima tujitahidi kutenga kati ya masuala ya kisiasa na yale ya kiuchumi na kijamii [ikiwemo elimu] ili kuhakikisha mtu hakwazi katika azma zake za maisha na siasa au wanasiasa au mashabiki wa wanasiasa fulani. Ni lazima pia tutenge urafiki na kazi. Na kutoa kazi kwa wale tu ambao wanaimudu kazi hiyo kwa kujenga mazingira yote yanayokubalika kwa watu wa aina zote na kwa shughuli za aina zote.

Katika miaka hii ambayo tuna wataalamu wengi mara kadhaa ukilinganisha na hali ilivyokuwa huko nyuma kwanini tushindwe kuwa na wataalamu wa menejimenti na oganaizesheni wanaoweza kutushauri njia bora za kuendesha kata, vijiji au shulena vyuo kwa namna ambayo ni nadra kuzuka migogoro isiyo ya lazima?
***

8. Demokrasia, utendaji na tathmini ya kazi

KUNA maswali kadhaa kuhusiana na Rasilimali Watu [Human Resource] yanayopaswa kujibiwa ili tuwe na uwezo wa kujenga demokrasia na taifa imara kiuchumi.

Je, elimu na ujuzi watu wetu walio nao sasa vinawatosha kusimamia ujenzi wa demokrasia nchini?

Kama panahitajika elimu na ujuzi zaidi au tofauti ni ujuzi na elimu gani hizo? Ni nani anayeweza kutupatia ujuzi na elimu hizo? Je, gharama ya kukosa elimu na ujuzi huo itakuwa ni ndogo ukifananisha na kuwa na elimu na ujuzi huo?

Hivi sasa tunajua ni mambo gani ambayo kila waziri, naibu waziri, katibu mkuu, mkuu wa idara, mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na watumishi wengine wa serikali wanayotakiwa kufanya. Tunayachagua vipi? Ni kigezo tosha cha utendaji kazi? Kuna utafiti wowote uliofanyika na pengine kulinganisha viongozi wetu na watu wa taifa lingine ambalo labda lina utendaji bora zaidi kiutumishi?

Ni kwa namna na njia gani tunazoweza kuzitumia kuwatathmini viongozi waliopo? Tunatumia vipindi gani? Na kama mtu akionekana anapwaya afanywe nini?

Palikuwa na hatua za kuanzisha kutumika kwa mfumo wa tathmini wazi [OPRAS]-lakini inaelekea umekwama mahala fulani. Lakini penda tusipende hatuwezi kuendelea na hatuwezi kujenga demokrasia bila ya kuwa na menejimenti ya utendaji na uwajibikaji [Perfomance Management] -chombo pekee kinachoweza kutenganisha kati ya takataka na nafaka halisi..

Demokrasia sio mfumo unaoweza kujengwa na wababishaji, waigizaji na watu wanaofanya utani na ujinga, umasikini na maradhi kwa hasara ya watu wetu.
***

9. Demokrasia, uwazi na mahesabu ya nchi

Ni lazima mahesabu ya serikali, wizara zote, miji yote, Benki kuu na taasisi nyingine muhimu yawe wazi na yanayoweza kufikiwa na yeyote anayetaka kuyachambua na kuyafanyia upembuzi wa kina.



Katika hili haki na uhuru wa mwananchi kufikia nyaraka za serikali lazima iwepo na itumike kwa jinsi mtu anavyotaka ili mradi ndani ya wigo wa kisheria na kikatiba.



Pengine wakati wa kuwa na SERIKALI YA VITABU WAZI [OPEN BOOK GOVERNMENT] kwa maana ya kwamba tutakuwa na nafasi ya kuona kila baada ya muda fulani serikali imepata nini na imetumia nini na sisi kuweza kuipongeza au kuikosea umefika?



Hapa Tanzania toka zoezi la ubianfsishaji [mali ambazo kinadharia zilikuwa zetu wote] hatujui ni fedha kiasi gani ilipatikana, imekwenda wapi na sisi tuliokuwa na HISA KATIKA TAIFA LA KIJAMAA tunaambulia nini?



Ni muhimu kukumbuka kuwa Karl Marx alikwishatutahadharisha juu ya kutumia mfumo wa demokrasia kama mfumo wa kujenga jamii ya kistaarabu. Yeye alisema kwamba: 'Mfumo huu ni mzuri tu mpaka pale watu wanapogundua kwamba wanaweza kuifilisi benki kuu na mtu asiwafanye lolote!'

Demokrasia ndio. Lakini lazima ifungamane na mifumo ya kulinda watu na nchi dhidi ya uovu na hasara zinazoweza kusababishwa na wajanja wachache katika jamii wakishirikiana na mabwana zao wa nje.

***

10. Demokrasia na uwekezaji kaika sekta za uchumi na jamii

LENGO mojawapo muhimu la Demokrasia ni kuhakikisha kuwa watu wanakuwa na uhuru na haki ya kufanya maamuzi yote katika masuala mbalimbali yanayogusa maisha yao.

Jambo moja muhimu ni hali yao ya maisha. Na hali ya maisha ya mtu wa Arumeru hadi Zanzibar au Amboni mpaka Zambia haiwezi kuamuliwa na mtu aliyeko Dar es salaam au Lusaka.

Maamuzi lazima yafanyike pale pale watu walipona makazi yao maana wao ndio wako katika fursa nzuri ya kuamua ni lipi muhimu kulifanya au kulipata katika wakati uliopo.

Na demokrasia ya kweli haitegemei fedha za msaada. Demokrasia ya kweli inategemea zaidi kutumia akili za watu kupata ufumbuzi wa matatizo na matarajio yao ya kila wakati.
Kwa miaka kadhaa sasa, mathalani, nchi nyingi zimeshindwa angalau kukarabati na kutengeneza barabara na reli tulizoachiwa na wakoloni au viongozi wetu wa mwanzo tulizopata kwa njia ya mikopo au msaada. Achilia mbali kujenga miundonmbinu mipya.

Ili kuwa na demokrasia ya kweli ni muhimu Afrika iweze angalau kuwa na akili ya kuhakikisha hatupotezi hata hiki tulicho nacho kwa sera zinazolenga kuwa na uwezo wa watu na rasilimali kwa ajili ya ukarabati na uboreshaji kile kilichopo.

Pengine, hata ufanyaji kazi wetu unapaswa ubadilike.

Hiki katika miaka hii ya sayansi na teknolojia Waziri wa Miundombinu anastahili kuwa kwenye ofisi iliyoko kwenye jengo fulani au kwenye hema kando ya barabara au reli au bwawa linalojengwa? Au basi maalum lenye uwezo wa kuwa na ofisi na sehemu ya kuishi waziri huyo na wasaidizi wake kadhaa?

Bila shaka Waziri akiendelea kukaa ofisini kila mwaka kama sio kila mwezi tutaendelea kupata taarifa mbovu kuhusu

Ujenzi wa barabara, reli, daraja, bwawa, kiwanja cha ndege, bandari na kadhalika. Watakaofanya kazi kwa kutania wataendela kufanya hivyo na watakaokwiba wataendelea kufanya hivyo.i

Ni lazima tuwe na utaratibu fulani wa kuhakikisha kuwa asilimia fulani ya kipato cha taifa inatumika katika ukarabati na kuhifadhi kile kilichopo wakati huo na hasa katika miundombinu na huduma za jamii.
***

11. Demokrasia, sera za serikali na ujinga

KUNA wanaodai kuwa hakuna nchi inayopenda wananchi wake wazinduke na kufahamau kuwa demokrasia Afrika sio kitu kibaya bali ni jambo zuri na litakalowasaidia watu kubadili maisha yao.

Kwa sababu hii Afrika nzima inalalumiwa kwa kuwafanya watu wa vijijini waendelee kuwa wajinga kuhusu haki na uhuru wao wa kidemokrasia.

Haiwezekani kabisa kuwa na demokrasia ya kweli hadi wananchi vijijini waelewe kuwa chama tawala sio baba wala mama au taasisi ambayo ikiondoka basi na wao ndio utakuwa mwisho wao.

La. Chama Tawala kilichopo na vingine vitakavyokuja ni taasisi zitakazostahili kuwepo tu kama zitawafanyia wananchi kazi nzuri inayoonekana na wote. Kama sivyo, ni ruksa kukikataa chama chochote ili chama mbadala kishike nchi ili nacho kijaribu kutumikia watu kwa utii na uaminifu zaidi. Nacho kikiboronga pia fimbo ya kura itakichapa na vitaendelea kujirudi na kujirekebisha vivyo hivyo mpaka angalau kimojawapo kiweze kufanya kazi iliyotumwa na wananchi.

Ni muhimu kwa serikali zetu kuondoa kodi na mikwara yote inayosababisha magazeti, redio, televisheni, vitabu na machapisho mengineyo kuwa ghali kuliko uwezo wa wananchi wengi vijijini.

Na wafadhili na wanaoitakia nchi hii mema ni lazima wasaidie uanzishwaji wa magazeti, redio na televisheni za jamii ambavyo kazi yake kubwa itakuwa ni kuwaamsha watu vijijini juu ya ukweli kuhusu haki, uhuru na demokrasia katika nchi yao.

Aidha ni haki ya wananchi kudai kuwa fedha zinatokana na kuchimbwa kwa dhahabu, almasi, tanzanite na madini mengineyo kiasi fulani kitumike katika kuhakikisha kuwa elimu ya msingi, sekondari na chuo kikuu kwa kiasi fulani inakuwa bure.

Watoto wetu kuwa na elimu ya angalau sekondari [inayotolewa bure au kwa gharama nafuu sana] ndio mwanzo sio tu wa kujenga taifa lenye kujali na kufuata demokrasia bali pia msingi imara wa watu wenye ufundi na ujuzi unaohitajika na wawekezaji wa ndani na nje.

Juu ya yote, binafsi, ninaamini kuwa lazima elimu ya chekechea hadi Chuo Kikuu hapa Tanzania iwe inatolewa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

Anayetaka kusoma kwa Kiingereza awe na haki hiyo. Na anayetaka kusoma kwa Kiswahili naye asinyimwe haki hiyo.

Ni dhahiri mataifa koloni kama Uingereza na Marekani yatapenda sana Tanzania idharau Kiswahili kwani kwa kufanya hivyo tutabakia kuwa koloni lao daima dawamu.

Tukiiga mfano wa China, India, Malaysia, Korea, Japani na wengine kama hao ni hatari kwao maana tutajiondoa kwenye makucha yao haraka kuliko wanavyotaka.
***

12. Demokrasia, Vyombo vya Habari na Mabadiliko katika jamii.

TANZANIA imejaliwa kuliko nchi nyingi Afrika isipokuwa labda Kenya ambao ni washindani wetu katika lugha ya Kiswahili.

Ninasema Tanzania imejaliwa kwa sababu ndio nchi inayoweza kama ikipenda kuwa na Redio ya Kiswahili Afrika, Televisheni ya Kiswahili Afrika, Tovuti Kuu ya Kiswahili Afrika na gazeti na jarida la Kiswahili kwa Afrika nzima.

Vyombo hivyo vikijengwa kwa mfano wa BBC, Deutsche Welle, Aljazeera na vyombo vinginevyo kwa kutumia Kiswahili na kuutanguliza mbele utamaduni wa Afrika tunaweza kufungua fursa nyingi za kujiendeleza na kujiajiri kwa vijana wetu hapa nyumbani.

Ni dhahiri taasisi mbalimbali za Kiswahili zitashirikiana na chombo hicho ili kuwafundisha wote wanaosikiliza au kutazama vyombo hivyo kujifunza Kiswahili. Hali kadhalika, pakiwa na michezo mizuri ya kuigiza ya Kiafrika basi Afrika nzima kila jioni itakuwa inaketi kutazama kinachozalishwa na vijana wa Kitanzania.

Lakini kubwa zaidi ni kuwa vyombo hivyo vya habari vitachangia si haba katika kuharakisha kupatikana kwa umoja wa Afrika ambao sasa hivi tunatapatapa na hatujui njia ya kuuleta kwa upole na ustaarabu.

Ili tufikie hatua hiyo, hata hivyo, lazima vyombo vyote vya habari viwe vinavyomilikiwa na serikali, vyama vya kisiasa au vya watu binafsi lazima viwe huru kuendesha mambo yao bila kuvunja misingi na taratibu vyombo vya habari vilivyojiwekea.
***

13. Demokrasia, polisi na raia

AFRIKA wakati mwingine inachekesha. Pakiwa sio wakati wa uchaguzi askari wetu wanashindwa kulinda usalama wa raia na mali zao. Lakini, ghafla bin vuu, uchaguzi au ugomvi wa kisiasa ukizuka askari polisi lukuki wanatoka hukowanakotokana na kuifanya kazi ya kuwalinda walio madarakani kwa namna ambayo wanawashinda hata polisi wa nchi za Magharibi.


Swali hapa ni, je, polisi kazi yao ni kuwalinda wale walioko madarakani au raia wote bila kubagua.



Ni nini kitakachotokea kama anayelindwa ni mwizi wa kura au kitu kingine?



Je, haitachekesha na pengine kuhuzunisha sana kuona mtu kaibiwa kisha mwizi ndiye anayemsakizia mbwa amuume au amuue eti?



Je, kuna nafasi katika mfumo wetu kuwa na jeshi la polisi ambalo haliwajibiki kwa aliyeko madarakani bali kwa raia. Ni nani achague Mkuu wa Polisi-Bunge au Rais?



Jibu moja kwa moja ni kuwa ili kuwe na haki ni lazima Mkuu wa Polisi achaguliwe na bunge kwa niaba ya wale wanaowawakiisha.



Kwa namna hii kiongozi huyo hatamuogopa mtu au chama tawala katika kufanya maamuzi yake. Na hii ndio demokrasia katika medani ya usalama wa nchi na watu wake.

***

14. Demokrasia, Mahakama na haki

MAHAKAMA ni mhimili muhimu katika taifa linaloamini katika demokrasia.

Jaji Mkuu kama kiongozi wa kitaifa ana haki sawa na Rais au Waziri Mkuu au Spika au Kiongozi yeyote wa chama cha kisiasa kilicho madarakani.

Wote wanaaminiwa na umma kufanya kazi zao si kwa faida yao binafsi bali kwa faida ya taifa na wananchi wake.

Haifai kabisa kiongozi yeyote au mtu yeyote kusababisha mahakama na uongozi wake kufanya kazi kwa upendeleo kwa sababu za kifedha au ksiasa au kimadaraka.

Kwa sababu ya hili tunaamini kuwa ni vyema Jaji Mkuu akachaguliwa na bunge kwa umoja wake na kupitishwa na rais na sio vinginevyo.

Kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa Jaji Mkuu anawajibika kwa wananchi kupitia kwa wabunge waliowachagua na sio kwa mtu fulani aliyeko madarakani kwa wakati huo.

Endapo, Tanzania, itafanikiwa katika hili sio tu nchi itakuwa na heshima bali tarafu nzima ya sheria na unasheria Afrika itapata heshima kubwa itakayoihakikishia Tanzania nafasi ya uongozi Afrika.

Ni lazima wanasheria wetu waone mbali zaidi ya kuwa wanasheria hapa nchini kwa maana kwamba wafikiriwe kuwa majaji katika mahakama za Afrika Mashariki, Afrika na dunia kama ndio kigezo kikuu cha kufanikiwa kitaaluma.
***

15. Demokrasia, uwakilishi na bunge

NCHI iwe na demokrasia au isiwe na demokrasia lazima bunge lililochaguliwa na wananchi liwakilishe mawazo na msimamo wa wananchi wanaowakilishwa.

BUNGE linalojiegemeza pembeni ya serikali na chama chochote cha kisiasa sio bunge la watu ni bunge la wabinafsi wachache wanaotetea maslahi yao wenyewe na sio ya wale waliowatuma.



Kazi ya mbunge katika nchi yoyote inayofuata demokrasia sahihi ni kuwakilisha mawazo na masuala yanayowahusu wale waliowachagua.

Na ni wajibu wa chama chochote na serikali yoyote kuhakikisha kuwa mbunge anayefanya kazi zake za kibunge hanyimwi uhuru na haki yake hata kama hakubaliani na serikali na chama kilicho madarakani.

Ikiwa vinginevyo basi ujumbe wanaostahili kuupata wananchi ni kuwa hawana uwakilishi na sio wajibu kwao kulipa kodi kwa sababu sheria inasema pasipo uwakilishi hapana haki ya kulipa kodi.

Katika kuimarisha bunge ni dhahiri kuwa wabunge ndio wanaostahili kumchagua Kamanda Mkuu wa Polisi, Wakuu wa mikoa [kwa hali ya sasa], Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Gavana wa Benki Kuu, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Mkuu na wale wengine wote ambao wanatakiwa wawajibike kwa watu na sio kwa watawala wa wakati huo.

Hatutakaa tuone mambo yanayotokea leo Zimbabwe, Kenya, Ethiopia, Zambia na Malawi hapa Tanzania.

Hili likifanyika ni kuwa Kamanda Mkuu wa Polisi atakuwa hawezi kutishwa na chama cha siasa wala mwenyekiti wake; na vivyo ndivyo itakavyokuwa pia kwa washika nyadhifa nyingine waliotajwa hapo juu.

Na pale ambapo mkuu wa polisi, mkuu wa mkoa, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Mkuu na watu wengine kama hao watakuwa hawatishwi na Mkuu wa nchi au chama tawala basi itakuwa ni rahisi kwa haki kufanyika wakati wote. Na haki inapokuwepo ndipo palipo pia na ukomavu wa demokrasia.

Bunge linalokuwa ni muhuri wa serikali iliyoko madarakani na na chama tawala basi inakuwa ni hasara kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Ni ujasiri kwa mbunge yeyote wa leo kusimama, kutetea na kupigania haki hii kwa faida ya kizazi cha leo na kizazi cha kesho.
***

16. Demokrasia na matumizi ya mikopo katika maendeleo.

NI DHAHIRI kuwa mara kadhaa nchi za Kiafrika zinakopa na kisha fedha hizo hazitumiki katika miradi husika.

Fedha inaweza kuhamishwa wakati wowote kwa amri ya mtu mmoja na ikatumika vibaya au vizuri bila watu kujua kinachoendelea.

Demokrasia mikoani itahakikisha kuwa kila mkopo unaohusu mkoa unatumika kweli kuleta maendeleo ya wakazi wa mkoa husika na sio vinginevyo.

Pengine utafika wakati pia ambapo serikali za nje, benki za ndani na nje na wafadhili wengine wanaweza kuingia mkataba moja kwa moja na waziri mkuu wa mkoa husika na hivyo kuhakikisha fedha yote inafika pale inapohitajika kufika.

Mazungumzo na wageni kadhaa imeonesha kuna 'walakini' mkubwa katika mfumo wa kidemokrasia kuikabidhi serikali ya nchi fedha zote za msaada na mkopo. Kutokana na 'lakini' hii sasa hivi wageni wengi wanaangalia jinsi wanavyoweza kufadhili mikoa, miradi na watu binafsi ili kuharakisha kasi ya kuondokana na umasikini Afrika. Tukiwa na serikali za mikoa zenye madaraka ya kujiamulia masuala yao ya kiuchumi na kijamii kazi hii itakuwa rahisi mno.
***

17. Demokrasia, fedha za wafadhili na wawekezaji

HALI ilivyo sasa ni kuwa wanaofaidika sana na fedha za wafadhili na wawekezaji ni wale walioko makao makuu ya nchi.

Endapo mikoa itakuwa na fursa ya kuendesha mambo yake ya uchumi na kijamii ni wazi kuwa fedha nyingi tu za wafadhili na wawekezaji sasa hazitaishia Dar es salaam bali zitamiminika kwa kiasi cha kutosha mahitaji ya mikoa na kanda mbalimbali nchini.

Katika mtazamo wa kisekta uliogusiwa mahala fulani katika makala hizi inaaminika kuwa Tanzania inaweza kugawanya katika kanda zinazofaa kuendeleza:. Katika uvuvi, kilimo cha umwagiliaji maji na utalii wa kando ya bahari na biashara ya kimataifa.. Katika utalii wa wanyama na sura ya nchim, kilimo maalum, elimu, tiba na huduma za afya.. Katika ufugaji na uuzaji nyama, ngozi, maziwa na mboji.. Katika kilimo cha nafaka, utalii wa kando ya maziwa.. Katika kilimo cha mboga, maua, matunda na viwanda vya usindikaji vyakula.. Katika uchimbaji madini, teknolojia nyeti, utengenezaji vito na urembo.

Bila shaka kila mkoa nchini unaweza ukajikita katika kile unachokiona una nafasi ya kufanya vizuri sana na kuhakikisha watu wake wananufaika sasa na sio baada ya WAO kwisha kufa.

Haya hayawezi kupatikana kwa urahisi kama demokrasia haitiririki hadi mkoani na watu wakawa na kiongozi wanayemchagua, bunge lao dogo na wizara zinazofanya kazi ya kuleta maendeleo haraka katika mazingira yao kwa kutumia mbinu na ubunifu wa asili wa wakazi wao.
***

18. Demokrasia na Matumizi mabaya ya fedha na kusahaulika serikali za mitaa

TATIZO la serikali kuu kuwa katika mji mmoja ni kwamba fedha nyingi za matumizi ya serikali huwa zinawanufaisha wakazi wa jiji husika na sio wakazi wa miji mingine.

Aidha, serikali katika mji mkuu hujiona ina majukumu makubwa ya siasa za nje na kwa kiasi kikubwa fedha nyingi hutumika katika masuala ya nje ukilinganisha na kile kinachotumika katika serikali za miji na mikoa nje ya makao makuu.

Demokrasia ya kweli haiwezekani kama serikali kuu nzima itaendelea kuwa katika mji na mkoa mmoja.

Kwa kufuata nadharia ya siasa na uchumi wa kisekta wakati umefika sasa wa wizara kugawanya kulingana na shughuli wanazofanya katika kanda mbalimbali.

Hii ina maana Dar es salaam inaweza ikawa na Makao Makuu ya Wizara nne au tano; Mwanza wizara nne au tano; Arusha Wizara nne au tano; Mbeya Wizara nne au tano; Dodoma Wizara nne au tano na hivyo kuifaidisha miji hiyo na kanda nzima hususan katika fedha za matumizi ya serikali na masurufu ya watumishi wake.

Mifano ipo ya kuwa na jengo moja linaloweza kuweka Makao Makuu ya Wizara tano,kumi au serikali nzima. Tuige lile linalofaa.

Mabadiliko haya yatawezesha pia serikali kuwa inaangalia kwa karibu zaidi maendeleo ya ndani ya nje badala ya kujishughulisha na mambo mengi madogo madogo ya nje lakini yenye gharama nyingi na kubwa lakini hakuna manufaa yanayolingana na matumizi yanayofanyika mwaka hadi mwaka.
***

19. Demokrasia na mahitaji ya msingi ya biandamu.

DEMOKRASIA ya kweli hufanya kazi katika nchi ambayo haina njaa; watu wake wanalipwa mishahara mizuri; na kwa ujumla hali ya uchumi hairuhusu upungufu au umasikini wa kutisha.




Demokrasia yenyewe hufanya kazi pale mtu anapolazimishwa kulinda shibe yake; kipato chake na hali yake ya uchumi kwa ujumla.



Hali kama hii haiko Tanzania. Na kwa kuwa haipo lazima wananchi wakishirikiana na wanasiasa mbalimbali kujikita katika kufikiri na kubuni shughuli mbalimbali za uchumi na kiuzalishaji mali zitakazowawezesha kwanza kutosheleza mahitaji yao ya msingi na pili kuwaweka katika nafasi nzuri ya kuimarisha uchumi na maendeleo ya nchi katika siku za baadaye.



Itakuwa ni muhali kuwa na demokrasia ya kweli pale ambapo hata mahitaji ya msingi ya watu wetu hayatoshelezwi.



Demokrasia katika hatua tuliyofikia pengine ni kuwa na mijadala inayoendelea siku zote kuona jinsi gani watu wetu watapata maji, umeme na huduma mbalimbali za jamii kiasi cha kutosheleza wote na kwa uhakika kwa maana ya kwamba teknolojia na uendeshaji vitu hivyo vyote vitakuwa ni vitu tunavyovishughulikia sisi wenyewe.



Kujitosheleza kwa maji, umeme, miundombinu, shule na vyuo, mahospitali na huduma za afya peke yake vinaweza vikawa ni shuighuli za kuingizia taifa pato la kutosha na hivyo kuharakisha kasi ya kuwatoa wananchi wetu kwenye umasikini. Lakini yote haya yanataka uwezo wa kuona mbali, kuukataa ubinafsi na kujitolea kwa viongozi kuona wananchi wao wananufaika wao kwanza kabla wao viongozi hawajanufaika. Je, tuna viongozi wa aina hii Afrika?



Umaskini huu wa kutisha aidha unaweza kuondolewa kwa kuhakikisha kuwa mikoa na sehemu za nchi husika zina uwezo wa kuendesha mambo yao ya kiuchumi na kijamii bila kuingiliwa sana na serikali kuu.



Dhana ya madaraka mikoani bado ni hai na sasa imeongezeka umuhimu wake baada ya kuona kuwa nchi zetu Afrika ni kubwa mno na hawezi mtu mmoja aliyeko huko kunakoitwa makao makuu ya nchi kuwaletea neema na ukwasi watu wa nchi nzima.



Ukweli ni kuwa mikoa ikiwa na uwezo wa kutekeleza sera zao za uchumi na kijamii kwa ushirikiano na marafiki wa ndani na nje basi nafuu na neema kwa wakazi wa mkoa husika itakuwa ni ya haraka zaidi kuliko ilivyo sasa.


Nafasi ya mikoa kujiendesha yenyewe kiuchumi na kijamii pia inalisaidia taifa kwa kuzalisha watu wanaofaa kushika nafasi za uongozi wa taifa badalal ya kuwa sisi ni watu wa kuwajaribu watu wasiotahiniwa katika tarafu hizo.

***