Umuhimu wa kiongozi mkuu wa nchi
Upo ushahidi tosha kwamba nchi au kampuni hutegemea sana uwezo, nia, sababu, visheni, msimamo na mwelekeo wa kiongozi wake mkuu.
Kiongozi huyo akiwa anaona mbali na mbele; ana nia ya kweli ya kuwajenga watu wake, ana wasaidizi wenye uwezo na wanaofaa, anajua anachokifanya na anajituma kwa moyo wake wote huweza kufanikisha malengo mengi yaliyoko mbele yake.
Kiongozi huyo akiwa kinyume cha hapo juu, yaani sio mtu mwenye kuona mbali na mbele, sio mwenye uwezo, sio mwenye nia ya kweli ya kuwatumikia watu wake, hana visheni na katawaliwa na ubinafsi wa hali ya juu, choyo, husuda, tamaa na mambo kama hayo hawezi kuipeleka nchi au kampuni popote pale. Sana sana atairudisha nyuma miaka kadhaa kama sio kuimaliza kabisa.
Aidha kiongozi ambaye hana sifa njema za uongozi huweza kuwa mateka wa wafanyabiashara, wanasiasa na wanajamii wengine waliomweka madarakani. Kwa namna hii, hata maamuzi na utendaji wake huyumbishwa kwa matakwa ya wafadhili wake.
Ndivyo ilivyo katika kazi ya kukuza na kuimarisha demokrasia katika nchi. Kiongozi wa juu asipokuwa na nia, sababu na uwezo wa kuitetea na kujienga demokrasia katika nchi yake basi ujenzi wa demokrasia katika nchi inakuwa ni sawa na kupanda kilima kirefu na chenye hatari ya kila aina njiani.
Hapa Afrika kama kweli wakuu wetu wa nchi wana nia ya kujenga demokrasia ya kweli na ya kudumu kazi hii itakuwa rahisi na itafanyika kwa kasi kuliko inavyofanyika hivi sasa.
Ukiangalia kwa mapana na marefu kitabu hiki kinaonesha kuna mambo kadhaa ambayo yakifanyika basi nchi za Kiafrika zitakuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine duniani.
Mambo hayo ni pamoja na kuwa na Katiba inayoendana na Mfumo tuliomo. Aidha Tume Huru ya Uchaguzi, Utawala wa Sheria ndani ya Mfumo wa Vyama Vingi na Haki za Binadamu kwa mapana na marefu.
Vyombo vya Habari huru, wagombea huru, Kutobibiwa kwa fedha za umma Hazina na vyma vya siasa, Viongozi wa nchi na watumishi wenye nia, sababu na uwezo wa kujenga demokrasia ya kudumu na iliyo hai wakati wote na inayofanya kazi iliyokusudiwa na waasisi wa mfumo huu.
Mambo mengine ni ushirikishwaji watu katika maamuzi kwa vitendo na sio kwa maneno, Kasi ya Maamuzi na Utekelezaji wake na Uwajibikaji kwa wote.
Demokrasia pia haiwezi kujengwa kwa dhati kwenye nchi yenye umasikini na njaa kali. Katika hali kama hii matajiri watatumia mali zao kuvuruga sio tu demokrasia bali pia mfumo wa kichumi na kisiasa wa nchi.
Kiongozi huonesha njia wengine wakafuata
Sasa tuoneshe kwanini tunasema kuwa kama kiongozi wa nchi ana nia, uwezo na sababu ya kukubali na kuiachia demokrasia ifanye kazi nchini basi kukua na kuimarika demokrasia katika nchi inakuwa ni jambo rahisi. Na hili tunalisema katika hali ya unyonge kwa sababu viongozi wetu leo wamejigeuza kuwa wao ni mabwana na sisi ni watwana wao. Kwa hiyo hata kama tunataka jambo na wao hawataki pamoja na wingi wetu wanaweza kulikataa hilo jambo nasi tusiwe na lolote la kufanya.
Ikiwa kiongozi wa nchi anaamua kwamba kweli kutokana na mabadiliko makubwa ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yaliyotokea nchini basi nchi inahitaji katiba mpya basi mara moja nchi nzima itarindima kwa sauti moja ya kukubalika kuwepo kwa katiba mpya. Kama kiongozi huyo anaona katiba mpya ni hatari kwake na kwa chama chake cha siasa na wapambe wake atakataa na ndio mwanzo wa demokrasia kupiga maktaimu hadi maamuzi sahihi yafanyike.
Hivyo ndivyo ilivyo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Wagombea huru. Yeye kiongozi mkuu akikubali tu haya tayari yatafanyika. Akikataa hakuna kitakachofanyika. Demokrasia itaendelea kusinyaa na kuwa na utapiamlo wa kujitakia.
Iwapo mkuu wa nchi atavikataza vyombo vya dola kujifanya mabwana na kuanza kuwanyanyasa watu kutokana na itikadi zao hilo halitafanyika. Akikaa kimya polisi kinyume na inavyotakiwa watajiona wao mabwana na kuanza kuwaonea na kuwanyima watu uhuru na haki zao za msingi.
Kiongozi bora hawezi kuuza au kununua haki za watu wake ziwe zile za uhuru wa kuamua wanachotaka au zile za kisiasa kwa kulea ujinga na umasikini. Atavipiga vitu hivi ili kuhakikisha watu wanakuwa huru ili waikuze na kuipanua demokrasia kutokana na uhuru huo.
Kiongozi mkuu akikataa kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa na vyombo vya habari vya nchi na akavisifu vinavyosema ukweli siku zote na kuvikebehi vinavyompaka 'goldstar' au 'coral' waziwazi basi msingi wa kuwa na vyombo vya habari huru utajengwa, tena haraka sana.
Ndivyo ilivyo pia kwa watumishi wa umma. Kama kiongozi mkuu anakemea wao kufanya kazi zao kwa kukiogopa chama fulani basi yaliyotokea na yanatokea kwenye Hazina za nchi hayawezi kutokea. Na fedha ya wananchi itakuwa salama hata kama chama fulani kinaondolewa madarakani. Kinyume chake kila baada ya uchaguzi mkuu wanaoingia madarakani wataikuta hazina haina kitu.
Ni kiongozi mkuu pia anayeweza kuzuia ubia usio mtakatifu kati ya wafanyabiashara, hazina na mangimeza wa serikali unaoziingiza nchi katika matatizo ya kila aina kila mwaka.
Kiongozi Mkuu akijua kuwa wizara ni vyombo vya kurahisisha uzalishaji mali na utoaji huduma hawezi kuunda baraza la watu 30 au zaidi ili kuwapendeza na kuwatafutia kazi waliomuunga mkono. Badala yake ataunda Baraza dogo la Mawaziri na kuweka mkakati wa kuzifanya kazi nyingine za serikali kuwa zinafanyika kwa gharama fulani kwa watumiaji na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendesheja serikali.
Haiyumkiniki kukosa demokrasia ndani ya chama chochote na kisha utegemee kwamba viongozi wa chama hicho hicho watatekeleza majukumu ya kidemokrasia kitaifa. Demokrasia huanzia ndani ya chama, kinyume cha hivyo ni longolongo tu.
Kiongozi wa nchi akijua kwamba kuwepo kwa demokrasia kutarahisisha kazi yake ya kujenga uchumi, utamaduni na jamii bora na imara basi shughuli zote za kimaendeleo katika nchi zinakuwa nyepesi zaidi.
Kiongozi wa nchi kama anatumia hekima na busara katika vita vya kuwatoa wananchi kutokana na umasikini, ujinga na maradhi anaweza akachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa msingi imara wa demokrasia. Jambo hili likifanyika, hata hivyo, kisiasa kwa ajili ya kupata umaarufu wa papo kwa hapo linaweza kuichimbua demokrasia na kuigeuza miguu juu, kichwa chini.
Mambo ya msingi kuzingatia
Kwa maneno mengine kuna mambo ya msingi ya kuzingatia kabla ya kukuza na kuimarisha demokrasia nchini. Mambo hayo ni pamoja na kutosheleza mahitaji ya msingi ya wananchi, matumizi ya lugha mama katika nchi kwa mapana na marefu, madaraka walipo watu, matumizi ya Teknohama katika kila sekta na hata ile ya kisiasa, haki za binadamu na tathmini za kazi za watu na kujua mchango wa kila mtu katika maendeleo ya nchi. Haya yakiwepo na kuzingatiwa wakati wote basi yumkini nchi inakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kukuza na kuendeleza demokrasia katika maeneo mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Haya yote ni mambo yaliyo ndani ya uwezo wa kiongozi wa nchi. Tathmini ya kiongozi yeyote kwa hiyo katika suala lal ujenzi wa demokrasia itafanyika kwa kuoanisha alichokifanya au kukizuia katika ujenzi wa demokrasia nchini mwake. Kiongozi anayekuwa kizingiti cha kukua demokrasia hawezi kuwa kiongozi safi na bora. Lakini upo uwezekano mkubwa kwa kiongozi anayekuwa chachu ya kukua demokrasia nchini mwake kuwa kiongozi safi na bora.
Kiongozi anayejiaminisha kwamba demokrasia ipo na hakuna tena la kufanya katika kuiboresha demokrasia hii atatambulika kwa hicho alichokuwa. Nacho sio kingine ila mgando wa demokrasia kwa kipindi fulani, yaani, ule muda anaokuwa madarakani.
Na hata kama kiongozi huyo hatawafanyia watu makubwa lakini akafanikisha kusimamisha tu misingi imara ya demokrasia basi kwa vyovyote vile watu na nchi yake watamheshimu na kumpa kiti cha juu katika kumbukumbu zao na historia yao.
Nchi hupata viongozi wa kila aina kadri miaka inavyopita. Hata hivyo, unaweza kugawa viongozi wa nchi katika vipindi vyote katika makundi matatu makubwa; Kwanza, kuna viongozi wanaoingia na kutoka madarakani bila kuleta tofauati yoyote katika maisha ya jamii na nchi -ni kama vile hawakuwepo; Pili, kuna viongozi wanaoingia na hadi kutoka madarakani huwa wameibomoa na kuiparananyisha kama sio kuisambaratisha nchi vibaya sana: na mwisho kuna viongozi wanaoingia na kutoka madarakani huku wakiiacha nchi imepiga hatua kadhaa mbele kimaendeleo.
Haya yote hutegemea kiongozi kaingi a madarakani kwa nia gani. Kama kiongozi huingia ili kujinufaisha yeye na jamaa zake tu basi ndio unapata aina zile mbili za kwanza. Na kama kiongozi kaingia ili kuwa endeleza watu na nchi yake ndipo unapopata ile aina ya mwisho.
Kwa kuhitimisha, pamoja na yote yaliyosemwa hatima ya nchi hutegemea sana kiongozi aliyeko madarakani. Akiwa anajua anachotaka na kule anakokwenda kama anavyojua watu wake wanachotaka na wanakotak kwenda bila kuyumbishwa wala kubabaishwa na watu wake basi nchi inaweza kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo. Kiongozi huyo kama hajui anakokwenda na anafuata mkumbo tu basi maendeleo na ustawi huwa ni kitu adimu.
Monday, September 14, 2009
Subscribe to:
Posts (Atom)
