Saturday, January 8, 2011

Maandamano: CCM, Vyombo vya Dola Vinavovunja Katiba

MAMBO yaliyotokea Arusha na Mwanza hivi karibuni, hususan kuhusiana na suala la nani aongoze halmashauri za miji hiyo limeanza kuzua wasiwasi kama viongozi wa CCM wana nia ya kweli ya kushirikiana na wananchi wengine ili kuipatia nchi hii katiba mpya na kuivusha Tanzania kuelekea kwenye demokraia isiyo na mizengwe, pana na ya kina mapema iwezekanavyo.

Inaonekama kama vile hivi sasa CCM haina mwenyewe; haijiamini; haijui inafanya nini na imeamua kutumia vibaya vyombo vya dola na serikali yake huku ikikiuka katiba iliyoko kushoto na kulia bila kujali wala kuogopa. Ubabe na maguvu haya yanayotumika bila kuwepo na sababu ya kuridhisha, yanakuja wakati tayari kuna malalamiko ya msingi dhidi ya chama hicho kutokana na jinsi uchaguzi mkuu ulivyoendeshwa mwaka jana.

Matukio haya yanawafanya baadhi ya watu pia kuamini kuwa CCM inadhani ina mkataba wa milele wa kuwatawala Watanzania; inalea ukabila wa kichama ambao ni mbaya kuliko ule wa kikakabila halisi; inajenga chuki kutoka kwa wananchi walio wengi; na inaonesha kama ni chama chenye uchu na uroho wa kutisha na iko tayari kufanya lolote ili kubaki madarkani. Na baya zaidi ni kuwa chama hicho kinashindwa kujifunza kutoka kwingineko Afrika, Marekani ya Kusini na Iliyoko Urussi ya zamani, pengine kwa kuwa sasa ni muflisi wa wanaitikadi na viongozi wanaofaa kukabiliana na changamoto na hali ya kisiasa inayokikabili chama hicho hivi leo.

Ni kutokana na hofu hii ndiyo maana nimeonelea leo kusaidia nchi yetu kwa kukishajiisha chama cha mapinduzi kufungua macho yake katika mambo kadhaa ili kuepusha shari kubwa inayoweza kutokea baadaye. Watanzania wa leo sio wajinga wa enzi za ujamaa na kujitegemea, bali werevu waliofunguliwa macho na umaskini, njaa ya raha na furaha, kiu ya haki na usawa, ufisadi, rushwa na madhambi mengine ambayo yameendelea kukua dhidi ya kelele za siasa za mambo kuwa kinyume cha hivyo.

Ninaamini bado CCM kinaweza kuwa chama imara na madhubuti bila ya uoga, ujanja, nabavu na ubabe kwa kujenga haki na usawa wa kisiasa nchini. Kinyume cha hivyo, chama hicho kitakuwa kinatengeneza mazingira magumu na mabaya kwa chama hicho na nchi yetu katika chaguzi zijazo.

Ukikiimarisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kiutawala, kikatiba, kisheria, kihaki, kiusawa, kiuongozi na kidemokrasia utakuwa pia unaviimarisha vyama mbadala na nchi kwa ujumla. Amani na umoja unaoimbwa kila siku vitapatikana na sio kwa kufanya mambo kinyume cha hivyo.

Kama tunavyoingia mwaka 2011 na mchakato wa Katiba Mpya ya nchi upo umuhimu pia kwa Chama Tawala nacho kupitia kwa makini katiba yake. Katika kupitia huko chama hicho kiangalie masuala ya muundo, mifumo, utawala, usimamizi, uongozi na udhibiti wa shughuli zake kwa nia ya kukiwezesha kuaminiwa, kujihalalisha, kuwajibika, ufanisi na ufanifu zaidi.

Nguvu za chama hicho kwa kiasi kikubwa zinatokana na kuwa na mtandao nchi nzima. Mtandao huo unaanizia kwanye matawi/mashina, mtaa, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi taifa. Tatizo kubwa ninaloliona kwa sasa ni mitihani na changamoto za uratibu, usimamizi, udhibiti na ukaguzi wa shughuli za chama katika ngazi mbalimbali.

Ni vyema chama kiangalie kama muundo wake na mifumo yake ya kazi hivi leo unaendana na changamoto hizo hapo juu kwa nia ya kuwafanya watendaji wake kuwajibika ipasavyo kwa wanachama na wananchi. Hali kadhalika kuhakikisha kuwa vyombo vya dola vinatumikia Watanzania wote bila kujali mtu ana itikadi gani au ni wa chama gani. Kikatiba iwe ni kosa kuchanganisha mambo na kazi za chama hicho na yale ya serikali. Hivi ni vitu viwli tofauti na iwe hivyo. Serikali inastahili kuwepo wakati wote, lakini chama kinaweza kuondolewa madarakani au hata kufa kikikosa ridhaa ya wananchi.

Muhimu pia ni kwa chama kutenganisha dhahiri bin shayiri mipaka yake ya kiuongozi na serikali. Isifikie mahala pa chama chochote kupora mamlaka ya mangimeza au watumishi wa serikali na hivyo kuhatarisha dhana ya serikali endelevu katika mabadiliko ya viongozi kidemokrasia katika vipindi bayana. Yaani polisi, mahakimu, wanajeshi na watumishi wote wa serikali wasiwe na wasiwasi chama fulani kinapoondolewa madarakani na chama kingine kuingia madarakani. Ni lazima sikuzote watumishi wa serikali wawe juu ya chama chochote cha kisiasa katika tarafu zao na sio kinyume cha hili. Watumishi wa serikali kukubali kuporwa madaraka na wanasiasa ndiko kulikotufikisha hapa tulipo leo. Enzi za chama kushika utamu bado zipo, laki si za chama kushika hatamu!

Changamoto nyingine inakuja kwenye suala la wale wanaopewa dhamana ya kukiongoza chama hicho katika ngazi mbalimbali. Hivi sasa kuna madai ya ukabila wa kichama. Na ndio maana kuna wana CCM wanaamini wao wana haki zaidi ya kuchaguliwa kuiko wenzao kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine CCM haitaki na haifikirii hapa bara kuwashirikisha wanachama wa vyama vingine katika kuongoza nchi yao. Na kama alivyosema baba wa taifa ukianzisha mgwanyiko kati ya watu kwa nia au shabaha yoyote ile mgawanyiko hauishii pale ulipokusudia. Jambo hilo haliwezi kuwa chanya bali hafi. Mgawanyiko mmoja huzaa mgawanyiko mwingine. Kichama ni kwamba ukiwa na nchi ambayo viongozi wake ni wa kabila la chama na viongozi wengine wote wa serikali (sio chama) hawakubaliki kutoka chama kingine unakuwa ni mwanzo sasa wa wanachama wenyewe kugawanyika kati ya wanachama viongozi na wanachama wafuasi. Na katika wanachama viongozi hugawanyika kati ya viongozi wetu na viongozi wao. Na kati ya viongozi wetu hugawanyika tena kati ya wateule na wasiokuwa wateule. Matokeo ya hili ni kukisambaratisha chama kwa kukosa gundi ndani na nje ya chama katika kukiunganisha.

Chama lazima kichague viongozi wenye elimu, ujuzi, uzoefu, tija, hulka na saikolojia taibu na sifa nyingine zinazotakiwa katika kufanikisha nafasi mtu anayopewa. Isitokee kumchagua mtu tu kwa sababu ni mwanachama na kisha mtu huyo akawa ni mzigo na tatizo kwa chama na viongozi wake.

Sielewi ni kwa kiasi gani chama hiki kina Sera na Mifumo ya Menejimenti ya Rasilimali Watu bora na inayofanya kazi. Ila tatizo moja ninaloliona ni la ajira, mishahara na malipo mengineyo. Bila ya kuwa na mifumo ya ajira na ujira sahihi chama hakiwezi kudhibiti masuala yake mengine ya uhai na kimaendeleo.

Katika miaka hii ya leo kukosa sera nzuri ya rasilimali watu (Human Resource Management) ni kukaribisha uongozi dhaifu kielimu, kimaarifa na kiulimwengu katika safu za uongozi wa chama na zile za utumishi wa umma kwa ujumla. Jambo litakoloongeza tatizo la ukabila wa kichama na kushindwa kudhibiti mapato ya chama,
mali za chama na miradi ya chama. Hali inayolea ubabe wa viongozi ngazi za chini, rushwa, kulindana na kukidhoofisha chama katika ngazi hiyo.

Wakati waasisi wa chama walikuwa na nia nzuri ya kukifanya chama kijiendeshe chenyewe lakini ukweli ni kwamba
kimeshindwa kujiendesha kiuchumi na kifedha. Na habari za hivi karibuni ni kwamba chama kiko katika hali mbaya. Kwa kuwa kimekosa mifumo ya ndani ya kiujasirimali, kiutafutaji na uzalishaji kipato chama hicho kimekuwa kikitegemea watu binafsi kukifundisha ujanja wa kupata fedha na mara nyingi kukiingiza mkenge.
Ni hatari kubwa mno kwa chama kumtegemea mtu mmoja au wawili kukitafutia mapato, maana upo uwezekano mkubwa wa chama hicho kuuzwa bila kujua kinachoendelea. Lazima muundo na mifumo ya chama ukiwezeshe kuzalisha pato la kukidhi gharama zake za kila mwaka na sio vinginevyo. Hili hakika ndilo linaloonesha uhai wa chama, vinginevyo unakuwa na chama kinachoishi kwa kutegemea hewa ya oksijeni ya kupuliziwa na wazuri na wabaya wake.

Chama sio mapato tu ni pamoja na kuwa na mameneja, wajasirimali wa ndani na wana itikadi wanaoendana na wakati na wanaosaidiana kukipatia chama mikakati-mipango inayofanya kazi.

Ni muhimu pia CCM iangalie ubora na udhaifu wa kuwa na wakuu wa mikoa na wilaya wasiochaguliwa na wananchi au wanaochaguliwa na wananchi. Uamuzi wa kuwa na mikoa-huru kiuchumi na kijamii ambayo bado CCM ina sauti utakuwa ni wa faida kwa chama hicho bila ya kusubiri mabadiliko ya katiba yatakayodai jambo hili likiwa na chagizo la chama kinachoshinda kura katika mkoa fulani kuwa ndicho kinachoendesha pia serikali ya mkoa husika.

Kuna wanaosema CCM imeifanya Tanzania kuwa na nchi-nyanya (nanny state). Kwa maana ya kwamba serikali yake inavumilia wanaofanya makosa ili mradi tu wanakiunga chama mkono. Aidha, sheria nyingi hupuuzwa na hakuna kinachofanyika ili mradi wanaovunja sheria hawaungi mkono upinzani bali wanakiunga mkono chama tawala. Bila ya utawala wa kisheria iwe kwa viongozi au wananchi itakuwa ni kazi sana kuwa na chama bora nchini.

Katika dunia hii ambayo baadhi ya wezi na wahalifu wengine hujitahidi kufaulu ushindani na mitihani yake ili awe polisi, hakimu au mwanasheria sio kwa nia ya kulinda watu bali kurahisisha maslahi yake binafsi; Ni katika dunia hii ambayo mzinzi mzoefu hujitahidi kuwa padri au shehe ili ufanyaji madhambi wake usiwe rahisi kujulikana ni muhimu kwa chama makini kuwaangalia wale inayowapa kazi ya kukijenga na kukiendeleza. Ili wasijikute wana wabomoaji wengi zaidi kuliko ya wajenzi. Iwe ndani ya chama au ndani ya serikali.

Katika tafiti binafsi, nimegundua kuwa mengi ya matatizo ambayo nchi yetu leo inapitia yanasababishwa na vyama vya kisiasa, ikiwemo chama tawala kukosa njia za uhakika na zinazojulikana za kupata mapato ya kujiendesha na yale ya kugharamia kampeni wakati wa uchaguzi. Bila ya tatizo hili kutafutiwa dawa itakuwa ni ndoto iwe kwa chama kilicho madarakani au kwa kitakachokuja au vitakavyokuja baadaye kuepuka balaa la rushwa, ufisadi, wizi, dhuluma na uonevu usio na sababu wa wananchi wasio na hatia zaidi ya kuunga mkono chama wanachoona kina misingi ya haki na usawa zaidi kuliko ya kile kinachotawala kwa wakati huo .

Inasikitisha kuona kuwa kuna waandishi, watangazaji na wanahabari, viongozi wa dini na watu wengine ambao kwa sababu moja au nyingine wanaamua kuona huku wamevaa miwani ya watu wanaoona karibu lakini hawaoni ya mbali. Huu ni msiba mkubwa. Na hasa pale kitendo cha kuvunja sheria kinapofanywa na watumishi wa chama tawala. Ni watu kama hawa ambao hawana tofauti kabisa na watu wa Radio Mille Colonnes ya Rwanda na kile ilichokisababishia nchi hiyo. Haiwezekani ikawa siku zote kuwa chama tawala na viongozi wake ndio watu wasiofanya makosa, lakini watu wengine sikuzote ndiyo wenye hatia. Wanaokataa kuona ukweli kwa kuwa wanaajiriwa na serikali au chama fulani ni mamluki na mkosi kwa Watanzania. Ndio wanaosababisha matatizo kama tunayoyaona katika nchi nyingine za Kiafrika. Na watu kama hawa wajue ni waliolaaniwa jana, leo na kesho pia. Hii ni laana ya kizazi cha kwanza hadi kizazi cha mwisho. Kweli, watanufaika kwa posho na hongo za chama hicho lakini kizazi chao chote kitakuwa kizazi kilicholaaniwa na kitakachokuwa kikiadhibiwa hapa hapa duniani kwa kuingiza nchi na watu katika matatizo, wakati walikuwa na nafasi ya kuikoa nchi.

Swali wengi wanalojiuliza ni kama viongozi na polisi mkoani Arusha wanafahamu mkoa wanaoishi au wote ni watu wa kuja. Maana Arusha ni kitovu cha Utalii Tanzania kama sio Afrika Mashariki. Kitendo walichokifanya kimeonekana 'laivu' dunia nzima. Hii leo picha iliyotoka Arusha ni kwamba nchi iko matatani, haikaliki na haifai kutembelewa na watalii. Je, haya ndiyo waliyoyataka. Hivi kwa kutumia akili zao kweli walishindwa kuwalinda na kudhibiti walioandamana toka mwanzo mpaka mwisho. Au wao kama kawaida yao walikuwa wakitekeleza amri toka juu. Hii, haithibitishi tukiwachia wanasiasa kututawala toka Dar es salaam mwishowe watatuingiza kwenye matatizo yasiyokwisha. Na kwamba wakati umefika wa mikoa kama ilivyo Zanzibar kujitawala yenyewe ?

Watanzania wenzangu tusiwaachie watu tuliowaajiri kutuongoza kufikia mahala ambapo inakuwa ni sawa na wezi kumwamuru mbwa wao kumng'ata mtu anayeibiwa na sisi tukaona kila kitu ni sawa tu.

Hivi polisi anayejua wajibu wake kwa umma anaweza akakubali kuamrishwa toka juu na kwenda bila fikira au roho kufanya kazi zake. Wewe ukiambiwa ua watu wako uue tu, bila kuangalia kama amri kama hiyo na mazingira yaliyopo unastahili kufanya unyama huo. Je, unaweza kweli kugeuzia baba, mama na ndugu zako bunduki na risasi za moto wakati wao wanafanya maandamano bila silaha.

Hivi jamaa hawa wanajua kuwa katiba ya nchi inamruhusu mtu kuandamana wakati wowote, mahala popote na kazi ya polisi ni kutoa ulinzi kwa raia wanaoandamana na sio kuwatupia risasi za moto.

Je, wana uwezo wa kufikiri kuwa amri au sheria yoyote inayokinzana na katiba ambayo ni sheria mama ni kitu au amri batili na haramu?

Itambulike kwamba, 'Mbuyu unapokaribia kuanguka ndio kwanza huwa unavimba na kujitanua kwa ukubwa na maguvu,' na kila dalili kwa baadhi ya wanasiasa zimeanza kuonekana likiendana na hili. Kadri watu waadilifu wanavyowahamasisha wananchi kukataa dhuluma, uonevu, wizi, ufisadi ndivyo pia 'wafa maji' watakavyozidi kuwang'ang'ania watu wema ili kufa nao. Hawa tena sio watu wa kuwashika mikono bali ni watu wa kuwapa fimbo au magogo wajiokoe wenyewe.

Somo kwa Watanzania hivi leo ni kuwa wasipoangalia wataendelea kutawaliwa na watu wanaotumia ghiliba, wizi, ubabe, kupandisha bei ovyo baada ya kuingia kwenye mikataba ya kipumbavu, dhuluma na uonevu wakati kuna vyama mbadala vyenye tabia tofauti na vitakavyowaletea nafuu kubwa katika maisha yao ya kila siku.

Uoga ni tabia ya kawaida kwa watawala ambao wameshindwa kuleta mabadiliko ya kimsingi kwa watu wanaowaongoza. Lakini wananchi kuwa waoga kukataa uonevu, dhuluma, wizi na ubaya mwingine ni kitendo cha aibu, dharau na 'kike' ambacho hata dini zinazojulikana huwa hazikubali. Ndiyo hali ya CCM sasa hivi na makombora inayotupa ovyo kwa wananchi wasio na hatia na kusingizia lawama kwingine.

Chama chochote cha kisiasa kitaendelea kuwa madarakani sio kwa ubabe, maguvu na kutumia vyombo vya dola kukandamiza watu wengine. Kubakia huko kutawezekana tu ikiwa chama hicho kina ridhaa ya wananchi. Chama kikiisha anza kupoteza ridhaa ya wananchi ujanja sio kutumia ulaghai na ubabe bali kujisahihisha, kujirekebisha na kujizaa upya ili kuukabili ukweli na hali halisi iliyopo ana kwa ana na sio vinginevyo.

Waandishi na wananchi wengine wasikubali kuwa vipofu kwa yale yaliyojiri Arusha na Mwanza kwa vitisho kwamba watu wakipigania haki zao basi watakuwa wanavunja sheria. Mida ya kukubali sheria za kimabavu na kibabe siku zote zinahesabiwa. Na ndio maana upo umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uandaaji wa Katiba Mpya na sio Tume itakayoendeshwa kwa rimoti kontroli kutoka Bagamoyo.

CCM ikiendelea kuzuia na kuwakatalia watu haki zao za kikatiba kwa kutumia watu wasioijua katiba na haki za wananchi wengine ni dhahiri na wananchi nao WATAENDELEA KUKIKATAA CHAMA CHA MAPINDUZI !

Mzimu wa Mwalimu utaendelea kuwaonesha na kuwadhihirishia pamoja na jitihada zao za kukipaka udini chama cha CHADEMA, bado chama hicho ndicho kimbilio la kufaa kwa Watanzania na sio vinginevyo.

Kila CCM ikitumia vyombo vya dola kulemaza na hata kuua watu basi musuli na vifua vya wananchi wasiokubali dhuluma vitazidi kupanuka na kugeuka chuma kwa mapambano ambayo chama hicho kikiwa kistraarabu na kinachowajali Watanzania kinaweza kuwaepusha.

Kila CCM ikishindwa kubadili hali ya wananchi na kuwaacha katika unyonge na umaskini wa kutisha, ijue hili litazidi kuvipa nguvu vyamba mbadala nchini.


Kila CCM ikiivunja kwa mabavu na kiburi katiba yake iliyopo ndivyo pia madai na misukumo ya raia kutaka katiba mpya itakayoandaliwa na watu huru na kasoro na maradhi ya CCM ndivyo yatakavyozidi kurindima.

Jinsi CCM inavyoua na kulemaza watu wasio na hatia kwa kutumia polisi wake ndivyo pia vijana wapenda haki wanavyozidi kuikataa na ndvyo pia wanavyozaliwa watoto watakaokichukia chama hicho milele.

Yaliyojiri Arusha na Mwanza na yanayoendelea kwingineko kwa jitihada za CCM kubaki madarakani kwa hila, ulaghai, wizi na mabadu; sio tu ni uthibitisho tosha kuwa tumechelewa kuipata katiba mpya bali pia bado kuna Watanzania wanaotishia kuikataa demokrasia pale wao wanapogeuka kuwa watu walioshindwa. Aidha, tumeshuhudia dhahiri kuwa watakaovunja amani na umoja wa nchi hii sio wengine ila wale watakaothubutu kutumia polisi na vyombo vya dola vibaya kwa faida zao binafsi na sio maslahi ya nchi hii!
Na mojawapo ya kazi ya katiba hiyo mpya iwe ni kukomesha kabisa vyombo vya dola kutumiwa na wanasiasa; ubomojaji wa nchi kwa mikataba ya kiwizi; ulaghai na wizi wa haki za watu unaofanywa na vyama vya kisiasa; na viongozi bomu wanaong'ang'ania kubaki kwenye vyeo, lakini hawawezi kuongoza wala kujenga nchi.

Tuesday, December 28, 2010

Ujinga Kuhusu Katiba Usivumiliwe

Nikiwasikiliza wakuu wa vyombo vya dola ninahsi kwamba hawaijui katiba, tena katika sehemu muhimu zinazowahusu, na hasa katika kuendesha kazi zao kwa haki na usawa kati ya wananchi. Ninapozungumza wananchi hapa ni kuwa hata rais na watumishi wa serikali ikiwemo polisi na wanajeshi ni wananchi kama ilivyo wanasiasa mbalimbali na raia kwa ujumla wao. Hakuna kati yetu anayestahili kuwa juu ya katiba au sheria. Lakini pamekuwa na mchezo kwa muda mrefu wa chama fulani cha kisiasa kule makao makuu na hata ngazi za chini katika ofisi za mikoa, wilaya na matawini kujiona kwamba wao wako juu ya katiba ya nchi na sheria. Huu ni mchezo tunaotaka uishe kwa kuwa na katiba mpya. Haukubaliki. Na wananchi watakuwa wajinga kuukubali. Enzi za udikteta wa chama kimoja umekwisha na tusikubali urudi maana yanayotokea katika baadhi ya nchi za kijamaa kwa ile iliyokuwa Russia leo yanatisha na iwe fundisho kwetu kukataa kata kata kuruhusu mizizi ya udikteta wa mtu au chama kuanza tena kuota hapa nchini.

Kosa kubwa nchi za Kiafrika zilizofanya ni lile la kuwaabudu viongozi wao na kuwafanya mungu wadogo hapa duniani. Na hakuna asiyependa kuabudiwa kama ilivyo kawaida yetu viumbe. Lakini hili si tu kosa la kiimani ni kosa katika maisha yetu ya kila siku kwa sababu watu hao wanaoabudiwa wakiwa wajinga au kuleweshwa na cheo na madaraka watataka hata kumzidi Mungu. Na kisha wanaowafuatia nao watataka kuwa miungu wadogo pia kama tunayoyaona yakitokea huko Kigoma, Arusha, Mwanza, Mara na kwingineko ambako Mungu wetu wa kisiasa wakubwa kwa wadogo hawataki upinzani ufurukute na kuwafanyia wananchi wao yaliyo mema, ya haki na wajibu kwa upande wao.

Maandamano na kuandamana hakuvunji katiba na sheria. Ni sehemu ya katiba na sheria. Na wanaovunja amani na mshikamano nchini sio wengine ila wale wanaotumiwa (na hawajui katiba na sheria kwa ukamilifu wake) na baadhi ya wanasiasa kuingilia haki ya kikatiba ya wananchi wengine.

Tuna kazi kubwa ya kuwaelewesha askari wetu kuwa bosi wao ni mwananchi na sio chama chochote cha siasa au ofisi ya mkubwa fulani serikalini. Na aliye na haki baina yetu juu ya suala hili la mahakama ni idara ya sheria/mahakama iliyo huru ambayo kwa sasa ni sawa na haipo.

Katiba yetu iko wazi kabisa katika suala la maandamano. Maandamano ni haki ya mwananchi. Kinachotakiwa ni kwa polisi, mgambo au wateuliwa wa chama au kundi husika watakaohakikisha usalama na amani wakati wa maandamano hayo. Lakini bado hii inabaki nikazi ya polisi, na haki ya kikatiba ya kila Mtanzania kuandamana ili mradi wanaofanya hivyo wanathibititha kutovunjwa imani. Polisi au FFU wanatuchekesha wanaposema walihisi 'uvunjikaji' wa amani endapo maandamano yatafanyika.

Soma Kifungu cha katiba kifutacho kwa uhakika wa hili : Katiba kifungu namba " 20.-(1) Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria
za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani,
kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo
hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au
mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au
kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo."

Kifungu hiki ni sehemu ya sheria za nchi wananchi walioziwekea wenyewe katika katiba ambayo leo baadhi yetu hatuitaki kwa sababu ya mapungufu yake ikiwemo kutafsiriwa ndivyo sivyo na vyombo vya dola.


Kama ilivyo katika jambo lolote ambalo hatimaye linaanza kukubalika na umma na nguvu ya umma kuanza kuliendesha lazima pazuke kambi mbili kuu.

Kambi ya kwanza ni ile ya lambalamba (sycophants) ambao hawana sababu nyingine ya kupinga kuwepo kwa katiba mpya ila tu kujihakikishia kuendelea kuwepo kwao leo na kesho. Hao hucheza karata eti umma utashindwa na mabavu ya kidikteta yataendelea kuwepo. Lakini sote tunajua kuwa udikteta sikuzote siku zake zinahesabika. Maana hili sio jambo linalokubalika na wananchi. Wananchi hutaka kujiendeshea mambo yao bila ya kufuatwa fuatwa na kusagwasagwa ili waridhie upande huu au ule. Umma unachokitaka na hoja thabiti za kuelewa bora na kinachowafaa kinyume na uongo, udhaifu na kisichowafaa.

Na kambi ya pili ni ile ya wale wana vukuto, wanaharakati na wafunguka macho wanaodai haki ambazo ziko wazi ndani ya katiba ya nchi.

Ni jambo la kusikitisha kwamba wakati nchi yetu ina maeneo ambayo majambazi wanavamia na kukata kata mapanga abiria eti FFU wako Dar es salaama kupambana na maandamano ya CUF na hatari yake ni kwa kuwa sio chama tawala tu na sio vinginevyo; wakati wanachi katika asilimia 70 ya hospitali zetu wilayani hawana magari ya wagonjwa tuna magari ya kuwamwagiwa watu maji ya pilipili yanayowasha; wakati tunahitaji zana na vifaa vya kutuondoa kwenye umaskini tunanunua na kutumia mabomu ya kuwalalzimisha watu kulia. Ama hakika aliyelewa na madaraka ni mwepesi wa kukufuru na kufanya isirafu ilhali anaona kila kitu kwake ni sawa!

Monday, December 20, 2010

ANAYEKATAA KATIBA MPYA HAITAKII MEMA TANZANIA

WAPO ambao kwa sababu wanazozijua wenyewe hawataki Watanzania wawe na katiba mpya. Wanadiriki kudai kwamba viraka vinavyowekwa kwenye katiba iliyopo vinatosha kabisa kukidhi haja na matakwa ya vijana wa Kitanzania leo kama ilivyokidhi haja ya Wazee wetu ambao wanatoweka kwenye safu za kisiasa na kimaisha siku hadi siku kwa kasi kubwa na ya kutisha.

Katika kukataa kwao kuwepo kwa katiba mpya wapinzani wa katiba mpya hawaonekani kuwa na hoja zaidi ya kwamba viraka vinatosheleza mahitaji na madai yote ya katiba mpya. Katika kuonesha dhahiri haja ya kuwepo kwa katiba mpya nchini mimi kama mwanaharakati wa demokrasia kwanza na pili mwanachama wa CCM (hai) na tatu Mtanzania mzalendo ninabainisha hoja kadhaa ambazo hata kwa wasiokwenda shule watazielewa na kuzikubali. Changamoto ni kwa wale wanaokataa katiba mpya kuja na hoja za kuwaaminisha wananchi vinginevyo.
Katiba si kitu cha watu wachache au chama kimoja cha kisiasa. Katiba ni makubaliano kati ya wanaotawala na wanaotawaliwa. Ni agano la watawala watawale vipi na wana haki gani kwa upande mmoja. Na upande wa pili wanaotawaliwa wana haki gani ya kuwawajibisha ikiwemo kuwaondoa madarakani wale wanaowatawala pindi inapoonekana watawala wamekosea au wameshindwa kutimiza wajibu wao.

Historia ni mwalimu tosha wa kuonesha fika kwamba nchi inapofanya mabadiliko makubwa kama yale ya kuutaliki ujamaa na kuukumbatia ubepari; kutoweka kwa waasisi wa uhuru katika medani za siasa na kuacha mfumo wa chama kimoja na kuukubali mfumo wa vyama vingi ni muhimu sana kuwa na mkataba mpya kati ya watawala na watawaliwa. Katika hali kama hii ndipo ulazima wa katiba mpya unapojitokeza.

Tuangalie hapa chini baadhi ya sababu zinazohalalisha kuundwa kwa katiba mpya itakayokubaliwa na walio wengi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katiba Ndio Kitu Pekee Kinachoweza Kubeba Mabadiliko Makubwa Leo na Kulihami Taifa na Wannanchi na Matukio Yajayo. Hili nitawaachia wataalamu kulizungumzia zaidi maana ni pana na zito sana katika maisha ya taifa na watu wake. Itosheleze tu kusema kwamba baadhi ya viongozi wetu leo wanaamini kwamba ni pale haja fulani inapoonekana, kwa mfano, matatizo ya muungano au nafasi yetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki au uporaji wa wawekezaji au kugundulika petroli ndio tu tunapohitaji kuibadili katiba. Sivyo ilivyo. Wingi wa viraka katika katiba unaonesha umuhimu na haja isiyokanushika ya kutengenezwa kwa katiba mpya. Katiba mpya inatakiwa ione mbali, itulinde na yaliyopo na yajayo na ituongoze na sio sisi tuiongoze. Haja hii sidhani inahitaji mjadala.

Nafasi ya Mgombea Huru katika Tanzania. Ingawa nchi hii inatoa haki kuwepo kwa mgombea huru lakini kutokana na matashi ya chama kimoja tu cha siasa haki hiyo haipo. Haiwezekani kuwa na katiba ambayo inaendeshwa kwa matakwa ya chama kimoja au wanasiasa fulani tu na sio matakwa ya wananchi walio wengi.

Demokrasia Dhidi ya Tabia za Kidikteta. Baadhi ya viongozi na taasisi nchini zinaonekana kuwa na uwezo wa kuweza kukataa hata yale wananchi wanayoyataka. Ikifikia hatua ya nanmna hii ni rahisi zaidi kujenga udikteta kuliko kujenga nguvu ya umma. Katiba mpya inahitajika kwa kiasi kikubwa kuzuia kuzuka kwa udikteta dhahiri na uliojificha katika nchi yetu -iwe ni kwa chama tawala au vyama mbadala vitakavyotawala siku zijazo.

Mahakama, Haki na Uwajibikaji wa Vyombo vya Kisheria. Mfumo uliopo hivi sasa hauwapi wananchi imani, maana kuwepo kwa viongozi wa juu wa mahakama badokwa kiasi kikubwa kunategemea matashi, mapendekezo na maamuzi ya mtu mmoja- iwe ni kwa sifa, upendeleo, udugu au ubinafsi wa aina hii au ile.

Upendeleo kwa Walioko Madarakni na Uonevu Dhidi ya Upinzani. Mapungufu na kasoro mbalimbali zilizopo katika katiba leo ndizo zinazochangia uchakachuaji demokrasia na kuifanya serikali iliyoko madarakani kuendelea kuwa na wabunge wengi bungeni kwa njia zilizo halali na zisizo halali pia.

Matumizi Mabaya ya Rasilimali na Maliasili za Nchi. Mfumo uliopo hivi leo unaruhusu baadhi ya viongozi na watumishi wa serikali kutumia maliasili na rasilimali kwa namna ambayo zinawanufaisha wao au chama fulani cha kisiasa. Mifano ni kama ile ya dhahabu waliyopewa Wachina kule Chunya au viwanja vya uwindaji walivyopewa wageni kule Loliondo na kwingineko au migodi ya madini waliyopewa wageni kwa bei sawa na bure.

Katiba lazima iweze sio tu kulinda maliasili na rasilimali zetu bali pia kuhakikisha kwa mapana na marefu yake vitu hivyo vinawanufaisha Watanzania zaidi kuliko wageni. Mathalani, katika madini Tanzania ingeliweza kukodi mitambo, wataalamu na vifaa vingine toka nchi za Ulaya Mashariki ya zamani au Afrika Kusini na kuchimba dhahabu yake wenyewe badala ya kuwapa wageni kwa kiasi cha mrabaha duni kama kilichokubalika kwa sheria zilizosababishwa na mapungufu ya kikatiba.

Katika kuongelea rasilimali za nchi ni wazi pia kwamba Benki Kuu na Hazina viko wazi kwa yeyote aliyeko madarakani kuchota chochote kilichomo humo bila ya katiba iliyopo kuwakamata na kuwawajibisha. Katiba mpya inahitajika ili kuhakikisha kilichopo Benki Kuu na Hazina bila kujali ni chama gani au kiongozi gani yuko madarakani. Vinginevyo, iko siku tutakuta Benki Kuu na Hazina kweupe na hakuna wa kuwajibishwa.

Upuuzaji na Udhalilishaji wa Rasilimali Watu Wazawa. Katiba iliyopo inazungumzia zaidi haki na usawa wa rasilimali watu. Lakini hakuna lolote la maana juu ya kuendeleza rasilimali watu na kuthamini rasilimali yetu kuliko fedha za wageni na mashine zao. Matokeo yake, Mtanzania miaka hii ya 2010 hathaminiwi na serikali yake na hathaminiwi na wageni wanaowekeza nchi hii. Angalia mishahara ya Mtanzania ukilinganisha na ya wageni au fidia Mtanzania anapopata ajali au huduma mbalimbali Mtanzania anazoahidiwa lakini hazipati kabisa au hazipati kwa ubora unaokubalika.

Kuzuka kwa Ukabila wa Kichama. Katiba iliyopo inaruhusu chama tawala kuwapa wanachama wake tu (hata wakiwa hawana uwezo) nyadhifa zote za uongozi ikiwemo uwaziri, ukuu wa mikoa, ukuu wa wilaya, ukuu wa mashirika na taasisi mbalimbali. Zanzibar inatufundisha kwamba upinzani nao unaweza ukawa na viongozi bora sawa au kuliko wale wa chama tawala. Tujifunze toka kwao. Hali ya chama kimoja tu kutoa viongozi kwa nchi nzima ni kosa. Ni hali inayojenga tunaouita UKABILA WA KICHAMA. Kama ulivyo ukabila mwingine, ukabila huu una hatari ya kubomoa zaidi ya kujenga.

Matumizi Mazuri ya Misaada Toka Nje. Tunahitaji pia katiba mpya ili tujadili pia misaada toka nje na jinsi inavyoweza kuiondoa nchi kwenye umaskini baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa takriban miaka 50 sasa. Kuna wanaoamini misaada sasa inafanana na kuwapa watu samaki badala ya kuwapa nyavu wakavue wenyewe. Na wengine wanaamini kinachopewa serikali kingi zaidi kinapotea kwenye mifuko ya wanasiasa kuliko kile kinachotumika katika kuwaondoa wananchi toka kwenye umasikini.

Kujikita Vizuri Katika Dunia ya Utandawazi. Sio tu Katiba yenu ina mapungufu makubwa ya siasa za nje, hali tunajua ni muhali kuendelea bila kutumia vyema ushirikiano wetu na nchi zinazotuzunguka na zile za mbali. Bali kubwa zaidi Tanzania kikatiba haina lolote juu ya kujilinda na kunufaika na utandawazi. Siasa za nje zilizomo mle ni zile za enzi za Vita Baridi na Nchi Zisizofungamana na upande wowote.



Kujikita Ipasavyo Katika Teknohama na Teknolojia Mpya. Ingawa Tanzania ndiyo ya kwanza kukumbatia Tekhohama hapa Afrika Mashariki leo ndio ya mwisho ila kwa simu za mkononi tu. NI dhahiri Katiba isiyo na upeo juu ya masuala kama haya (angalia wizi wa kutumia Teknohama katika mabenki) imechangia kwa kiasi kikubwa kutufanya tuwe wa mwisho na kupitwa na nchi ndogo kama Rwanda. Kwa kuzingatia Teknohama (ICT) ndio dunia ya kesho, na dunia ya kesho ni Teknohama ni muhimu tukawa na katiba inayoendana na enzi na miaka ya Teknohama na sio vinginevyo.


Teknolojia, Utengenezaji Mitambo Yetu na Maendeleo ya Viwanda. Ujenzi wa viwanda na ubunifu katika kuunda na kutengneza teknolojia na vifaa vyetu vyenyewe ni kitu adimu katika katiba iliyopo. Hatuwezi kuzungumza juu ya viwanda na teknolojia kama Waswahili kwenye kijiwe cha kahawa na kisha tukaendelea kikwelikweli. Ni lazima hili liwemo katika katiba likisaidiwa na mikakati ya kulifanikisha katika vitendo sasa na baadaye. Si vigumu kuelewa kwamba Tanzania hivi leo tunatumia kwa asilimia kubwa vitu na vifaa vilivyotengenezwa nje, japo kuna vingi tunavyoweza kuvitengeneza hapa hapa nchini na kubadili kabisa hali yetu ya kiuchumi. Sera peke yake hazitoshi. Tunahitaji Katiba Mpya kuzipa sera hizo ndimi, meno na makucha. Hatuwezi katu kuendelea kama viwanda, barabara, mifumo ya maji na umeme na kadhalika vitaendelea kutegemea mitambo na mashine toka nje badala ya sisi kuvitengeneza sisi wenyewe. Katiba mpya inahitajika kutunusuru na kuwa taifa la wachuuzi na wanunuzi wasiotengeneza chochote kile wanachokitumia wao wenyewe.

Umaskini kama karata turufu ya watawala. Yapo madai kwamba wanasiasa wa nchi yetu hawawezi kabisa kuruhusu umaskini utoweke maana kwa kufanya hivyo mtaji unaowasaidia kurudi madarakani kila baada ya miaka mitano hautakuwepo. Kwa maneno mengine, serikali na wanasiasa wanafanya mbwembwe tu kupiga makelele kuwa wanapiga umaskini vita. Ukweli ni kuwa wanapigania umaskini kuendelea kuwepo milele ili na wao watawale wajinga na wenye njaa milele.

Nafasi ya Lugha ya Kiswahili katika Maendeleo ya Nchi. Hivi sasa kuna baadhi yetu baada ya miaka 50 ya Uhuru wakingali wanaamini kwamba nchi yetu itaendelea kwa kutumia lugha za kigeni na hususan ile ya Kiingereza.

Hata hivyo, kuna waliofunguka macho ambao wanajua fika kwa kutumia Kiingereza kila tunalopangwa litapanguliwa tu hatimaye. Na kama walivyofanya ndugu zetu wa Kichina, Kikorea, Kihindi, Wajapani, Waindonesia, Wamalaysia, Kiarabu ni lazima tutumie lugha yetu wenyewe ili tukwepe kuvurugwa na Waingereza wa sasa na wa kesho.

Ipo haja pia kwa wale wote wanaotaka kuanzisha shule za chekechea, msingi, sekondari na Vyuo Vikuu vinavyotumia lugha ya Kiswahili kuruhusiwa kufanya hivyo na katiba na hivyo kuepuka mizengwe wanayofanyiwa sasa na serikali ambayo kwa kiasi kikubwa bado inaonekana kuabudu Uzungu na hususan Uingereza na kudharau lugha yetu wenyewe ya Kiswahili.

Isitoshe katika miaka na karne hii, shule na vyuo viwe huru kutumia Kiarabu au Kichina au Kijapani au Kihindi au Kiswahili (lugha za nchi zinazoendelea kwa kasi zaidi) badala ya kila shule au chuo kulazimishwa kutumia Kiingereza.

Kutekwa Nyara kwa Mjadala wa Katiba. Upo uwezekano mkubwa pia kwamba jambo hili la uundwaji wa Katiba Mpya lisipofanyika hivi sasa upo uwezekano mkubwa wa Chama Tawala kuteka mjadala na uundaji wa Katiba mpya. Hili ni dhahiri kwa kuzingatia pia kuna wafadhili ndani na nje ya nchi ambao wako tayari kufadhili kazi hii.

Na ndivyo ilivyo kwa Kilimo cha zamani, Kilimo ni Uhai, Kilimo cha Umwagiaji, Kilimo Kwanza na Kilimo "Kijacho" -bila Katiba kuwa na mashiko yenye dhamira na nia ya kweli ya kubadili hali za watu wetu, tutaendelea kuwa watu wa maneno na nyaraka nzuri lakini wafupi katika vitendo na mafanikio yetu.

Nafasi ya Mikoa Huru Kiuchumi na KIjamii. Kasoro kubwa katika muundo wa nchi yetu ni ule unaojitokeza pale ambapo watu chini ya laki nne wanapopiga kura kuchagua rais, wabunge/wawakilishi na baadaye baraza la mawaziri kwa eneo moja la Tanznia-Tanzania Visiwani. Lakini mkoa wenye wapiga kura zaidi ya milioni hauna nafasi ya kumchagua yule anaouongoza mkoa achilia mkoa huo kuwa na wajumbe na baraza lake la mawaziri, ingawa huu ndio muundo unaoonekana una nafasi kubwa zaidi ya kututoa toka kwenye umaskini kuliko ule uliopo hivi sasa. Ni dhahiri katiba mpya inahitajika ili kurekebisha hali hii.

Kutambulika na kukubalika Nafasi ya kila Mtu na Kila Chombo katika Taifa. Hivi leo nafasi ya mtu katika eneo moja la nchi inaweza ikaingiliwa na mwingine eti tu kwa sababu mtu huyo yuko Wizarani au Ikulu. Hili si sawa. Hali kadhalika, ni dhahiri kuwa vyombo vya dola kama vile polisi, jeshi na usalama wa taifa vinaweza vikaingilia kazi za taasisi zingine ama kwa ridhaa ya vyombo hivyo au kwa kulazimishwa na kiongozi fulani au chama fulani. Mwanzo wa mwisho wa demokrasia huanza pale vyombo vya dola visipotambua nafasi yao katika taifa linaloamini na kufuata demokrasia ya kweli.

Thursday, September 16, 2010

Demokrasia bila Mijadala au Midahalo

LAITI ingelikuwa hivyo, basi Plato na Wagiriki wangeliipa demokrasia jina lingine. Lakini kwa kuipa demokrasia jina hili waliotangulia walishangilia uwezo wa binadamu katika kubishania juu ya kilicho bora na heri kwao. Tualewaje wasiotaka tupate bora na heri zaidi ?

Laiti wangelisoma h apa; haya yasingetokea...

Kenya 3; Tanzania 0

KWA mara nyingine tena imeiaibisha Tanzania baada ya kuipiku katika kuzungumzia na kuiafiki katiba mpya ya Jamhuri ya Kenya.Tulishapitwa pia katika kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na serikali ya Umoja wa Kitaifa. Laiti upinzani ungeliungana hili kwa sasa lingekuwa yakini, yaani, lingekuja kwa kulazimishwa watawala wetu wa sasa.
Ninaamini, Tanzania bila kuwepo na mabadiliko ya kweli, ya kina na ya msingi haiwezi kubadilika. Itakuwa tu juzi kama jana, na jana kama leo!

Monday, September 14, 2009

DEMOKRASIA NA KIONGOZI MKUU WA NCHI

Umuhimu wa kiongozi mkuu wa nchi
Upo ushahidi tosha kwamba nchi au kampuni hutegemea sana uwezo, nia, sababu, visheni, msimamo na mwelekeo wa kiongozi wake mkuu.

Kiongozi huyo akiwa anaona mbali na mbele; ana nia ya kweli ya kuwajenga watu wake, ana wasaidizi wenye uwezo na wanaofaa, anajua anachokifanya na anajituma kwa moyo wake wote huweza kufanikisha malengo mengi yaliyoko mbele yake.

Kiongozi huyo akiwa kinyume cha hapo juu, yaani sio mtu mwenye kuona mbali na mbele, sio mwenye uwezo, sio mwenye nia ya kweli ya kuwatumikia watu wake, hana visheni na katawaliwa na ubinafsi wa hali ya juu, choyo, husuda, tamaa na mambo kama hayo hawezi kuipeleka nchi au kampuni popote pale. Sana sana atairudisha nyuma miaka kadhaa kama sio kuimaliza kabisa.

Aidha kiongozi ambaye hana sifa njema za uongozi huweza kuwa mateka wa wafanyabiashara, wanasiasa na wanajamii wengine waliomweka madarakani. Kwa namna hii, hata maamuzi na utendaji wake huyumbishwa kwa matakwa ya wafadhili wake.

Ndivyo ilivyo katika kazi ya kukuza na kuimarisha demokrasia katika nchi. Kiongozi wa juu asipokuwa na nia, sababu na uwezo wa kuitetea na kujienga demokrasia katika nchi yake basi ujenzi wa demokrasia katika nchi inakuwa ni sawa na kupanda kilima kirefu na chenye hatari ya kila aina njiani.

Hapa Afrika kama kweli wakuu wetu wa nchi wana nia ya kujenga demokrasia ya kweli na ya kudumu kazi hii itakuwa rahisi na itafanyika kwa kasi kuliko inavyofanyika hivi sasa.

Ukiangalia kwa mapana na marefu kitabu hiki kinaonesha kuna mambo kadhaa ambayo yakifanyika basi nchi za Kiafrika zitakuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine duniani.


Mambo hayo ni pamoja na kuwa na Katiba inayoendana na Mfumo tuliomo. Aidha Tume Huru ya Uchaguzi, Utawala wa Sheria ndani ya Mfumo wa Vyama Vingi na Haki za Binadamu kwa mapana na marefu.


Vyombo vya Habari huru, wagombea huru, Kutobibiwa kwa fedha za umma Hazina na vyma vya siasa, Viongozi wa nchi na watumishi wenye nia, sababu na uwezo wa kujenga demokrasia ya kudumu na iliyo hai wakati wote na inayofanya kazi iliyokusudiwa na waasisi wa mfumo huu.

Mambo mengine ni ushirikishwaji watu katika maamuzi kwa vitendo na sio kwa maneno, Kasi ya Maamuzi na Utekelezaji wake na Uwajibikaji kwa wote.

Demokrasia pia haiwezi kujengwa kwa dhati kwenye nchi yenye umasikini na njaa kali. Katika hali kama hii matajiri watatumia mali zao kuvuruga sio tu demokrasia bali pia mfumo wa kichumi na kisiasa wa nchi.

Kiongozi huonesha njia wengine wakafuata
Sasa tuoneshe kwanini tunasema kuwa kama kiongozi wa nchi ana nia, uwezo na sababu ya kukubali na kuiachia demokrasia ifanye kazi nchini basi kukua na kuimarika demokrasia katika nchi inakuwa ni jambo rahisi. Na hili tunalisema katika hali ya unyonge kwa sababu viongozi wetu leo wamejigeuza kuwa wao ni mabwana na sisi ni watwana wao. Kwa hiyo hata kama tunataka jambo na wao hawataki pamoja na wingi wetu wanaweza kulikataa hilo jambo nasi tusiwe na lolote la kufanya.

Ikiwa kiongozi wa nchi anaamua kwamba kweli kutokana na mabadiliko makubwa ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yaliyotokea nchini basi nchi inahitaji katiba mpya basi mara moja nchi nzima itarindima kwa sauti moja ya kukubalika kuwepo kwa katiba mpya. Kama kiongozi huyo anaona katiba mpya ni hatari kwake na kwa chama chake cha siasa na wapambe wake atakataa na ndio mwanzo wa demokrasia kupiga maktaimu hadi maamuzi sahihi yafanyike.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Wagombea huru. Yeye kiongozi mkuu akikubali tu haya tayari yatafanyika. Akikataa hakuna kitakachofanyika. Demokrasia itaendelea kusinyaa na kuwa na utapiamlo wa kujitakia.

Iwapo mkuu wa nchi atavikataza vyombo vya dola kujifanya mabwana na kuanza kuwanyanyasa watu kutokana na itikadi zao hilo halitafanyika. Akikaa kimya polisi kinyume na inavyotakiwa watajiona wao mabwana na kuanza kuwaonea na kuwanyima watu uhuru na haki zao za msingi.

Kiongozi bora hawezi kuuza au kununua haki za watu wake ziwe zile za uhuru wa kuamua wanachotaka au zile za kisiasa kwa kulea ujinga na umasikini. Atavipiga vitu hivi ili kuhakikisha watu wanakuwa huru ili waikuze na kuipanua demokrasia kutokana na uhuru huo.

Kiongozi mkuu akikataa kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa na vyombo vya habari vya nchi na akavisifu vinavyosema ukweli siku zote na kuvikebehi vinavyompaka 'goldstar' au 'coral' waziwazi basi msingi wa kuwa na vyombo vya habari huru utajengwa, tena haraka sana.
Ndivyo ilivyo pia kwa watumishi wa umma. Kama kiongozi mkuu anakemea wao kufanya kazi zao kwa kukiogopa chama fulani basi yaliyotokea na yanatokea kwenye Hazina za nchi hayawezi kutokea. Na fedha ya wananchi itakuwa salama hata kama chama fulani kinaondolewa madarakani. Kinyume chake kila baada ya uchaguzi mkuu wanaoingia madarakani wataikuta hazina haina kitu.

Ni kiongozi mkuu pia anayeweza kuzuia ubia usio mtakatifu kati ya wafanyabiashara, hazina na mangimeza wa serikali unaoziingiza nchi katika matatizo ya kila aina kila mwaka.

Kiongozi Mkuu akijua kuwa wizara ni vyombo vya kurahisisha uzalishaji mali na utoaji huduma hawezi kuunda baraza la watu 30 au zaidi ili kuwapendeza na kuwatafutia kazi waliomuunga mkono. Badala yake ataunda Baraza dogo la Mawaziri na kuweka mkakati wa kuzifanya kazi nyingine za serikali kuwa zinafanyika kwa gharama fulani kwa watumiaji na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendesheja serikali.

Haiyumkiniki kukosa demokrasia ndani ya chama chochote na kisha utegemee kwamba viongozi wa chama hicho hicho watatekeleza majukumu ya kidemokrasia kitaifa. Demokrasia huanzia ndani ya chama, kinyume cha hivyo ni longolongo tu.

Kiongozi wa nchi akijua kwamba kuwepo kwa demokrasia kutarahisisha kazi yake ya kujenga uchumi, utamaduni na jamii bora na imara basi shughuli zote za kimaendeleo katika nchi zinakuwa nyepesi zaidi.

Kiongozi wa nchi kama anatumia hekima na busara katika vita vya kuwatoa wananchi kutokana na umasikini, ujinga na maradhi anaweza akachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa msingi imara wa demokrasia. Jambo hili likifanyika, hata hivyo, kisiasa kwa ajili ya kupata umaarufu wa papo kwa hapo linaweza kuichimbua demokrasia na kuigeuza miguu juu, kichwa chini.

Mambo ya msingi kuzingatia
Kwa maneno mengine kuna mambo ya msingi ya kuzingatia kabla ya kukuza na kuimarisha demokrasia nchini. Mambo hayo ni pamoja na kutosheleza mahitaji ya msingi ya wananchi, matumizi ya lugha mama katika nchi kwa mapana na marefu, madaraka walipo watu, matumizi ya Teknohama katika kila sekta na hata ile ya kisiasa, haki za binadamu na tathmini za kazi za watu na kujua mchango wa kila mtu katika maendeleo ya nchi. Haya yakiwepo na kuzingatiwa wakati wote basi yumkini nchi inakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kukuza na kuendeleza demokrasia katika maeneo mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Haya yote ni mambo yaliyo ndani ya uwezo wa kiongozi wa nchi. Tathmini ya kiongozi yeyote kwa hiyo katika suala lal ujenzi wa demokrasia itafanyika kwa kuoanisha alichokifanya au kukizuia katika ujenzi wa demokrasia nchini mwake. Kiongozi anayekuwa kizingiti cha kukua demokrasia hawezi kuwa kiongozi safi na bora. Lakini upo uwezekano mkubwa kwa kiongozi anayekuwa chachu ya kukua demokrasia nchini mwake kuwa kiongozi safi na bora.
Kiongozi anayejiaminisha kwamba demokrasia ipo na hakuna tena la kufanya katika kuiboresha demokrasia hii atatambulika kwa hicho alichokuwa. Nacho sio kingine ila mgando wa demokrasia kwa kipindi fulani, yaani, ule muda anaokuwa madarakani.

Na hata kama kiongozi huyo hatawafanyia watu makubwa lakini akafanikisha kusimamisha tu misingi imara ya demokrasia basi kwa vyovyote vile watu na nchi yake watamheshimu na kumpa kiti cha juu katika kumbukumbu zao na historia yao.

Nchi hupata viongozi wa kila aina kadri miaka inavyopita. Hata hivyo, unaweza kugawa viongozi wa nchi katika vipindi vyote katika makundi matatu makubwa; Kwanza, kuna viongozi wanaoingia na kutoka madarakani bila kuleta tofauati yoyote katika maisha ya jamii na nchi -ni kama vile hawakuwepo; Pili, kuna viongozi wanaoingia na hadi kutoka madarakani huwa wameibomoa na kuiparananyisha kama sio kuisambaratisha nchi vibaya sana: na mwisho kuna viongozi wanaoingia na kutoka madarakani huku wakiiacha nchi imepiga hatua kadhaa mbele kimaendeleo.

Haya yote hutegemea kiongozi kaingi a madarakani kwa nia gani. Kama kiongozi huingia ili kujinufaisha yeye na jamaa zake tu basi ndio unapata aina zile mbili za kwanza. Na kama kiongozi kaingia ili kuwa endeleza watu na nchi yake ndipo unapopata ile aina ya mwisho.

Kwa kuhitimisha, pamoja na yote yaliyosemwa hatima ya nchi hutegemea sana kiongozi aliyeko madarakani. Akiwa anajua anachotaka na kule anakokwenda kama anavyojua watu wake wanachotaka na wanakotak kwenda bila kuyumbishwa wala kubabaishwa na watu wake basi nchi inaweza kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo. Kiongozi huyo kama hajui anakokwenda na anafuata mkumbo tu basi maendeleo na ustawi huwa ni kitu adimu.

Sunday, July 26, 2009

DEMOKRASIA, TEKNOHAMA NA WIZI WA KURA

INDIA, taifa lenye kufuata demokrasia na lenye watu wengi kuliko mataifa mengine duniani yanayofuata demokrasia mwaka huu kwa mara ya kwanza liliweza kuendesha uchaguzi wake mkuu kwa kutumia TEKNOHAMA.

Nchi hiyo imedhihrisha inawezekana kabisa kuondoa mkono wa mtu unaolaumiwa sana kwa kupandikiza majina ya uongo katika daftari la wapiga kura, kutowaandikisha wapiga kura walio na haki ya kupiga kura, kuingiza kura za uongo, kuharibu na kupoteza kura za halali na mambo mengine kama hayo.

Jambo hili linaashiria kwamba ikiwa patakuwa na muundo na mfumo unaokubalika wa Katiba mpya katika mfumo wa vyama vingi na Tume Huru isiyoegemea upande mmoja na kisha kutumiwa TEKNOHAMA haki na usawa katika upigaji kura ni mambo yanayoweza kuwa kitu cha uhakika zaidi kuliko ilivyo sasa.

Katika nchi nyingi za Kiafrika kile kinachoitwa Tume ya Uchaguzi ni kiumbe cha chama tawala na seriklai yake. Ni zao la Katiba za viraka na ziizopitwa na wakati. Ni zao za sheria zilizopitwa na wakati na zisizokidhi matarajio ya ushindani wa kisiasa, soko huru na haki za binadamu.

Kwa kuwa wanaoongoza taasisi hizo ni watu wanaolishwa fadhila na chama tawala matokeo yake sikuzote ni kukisaidia na kukipendelea chama hicho kishinde hata pale kinapostahili kushindwa.

Uhakika wa kura ya mpiga kura kwenda kwa yule anayemtaka, Haki na Ukweli ni vitu vinavyowezekana endapo kutakuwa na upigaji kura kieletroniki.

Madhali nchi kama India imeshaanza kazi kama hii kinachotakiwa ni kwa chombo cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulika na Demokrasia na Haki za Binadamu kuwa wakala wa kukodisha vifaa vya Teknohama toka India ili vitumike wakati wa uchaguzi katika nchi mbalimbali za Kiafrika na dunia ya tatu kwa ujumla.

Vinginevyo, utafiti uendelee kufanyika zaidi ili kuja na mashine bora zaidi za kieletroniki zitakazoondoa kabisa wizi na ujanja wa aina nyingine wakati wa kupiga kura Afrika na duniani kote kwa ujumla.

Ikumbukwe kwamba WIZI NA RUSHWA KUBWA KULIKO ZOTE ni zile zinatokea wakati wa chaguzi katika nchi mbalimbali Afrika. Ukkomesha wizi na rushwa hii katika ngazi hiyo utakuwa umelisaidia bara hili sio haba.

Nini kifanyike
Serikali ya India ambayo kwa sasa iko karibu na nchi za Kiafrika kuliko wakati wowote uko nyuma inaweza kuanza kwa kuwaalika wanasiasa na vijana wa vyama mbalimbali vya kisiasa kwenda India ili kupata mafunzo ya muda mfupi kuhusu upigaji kura kielektroniki. Huko watajifunza kwa nadharia na vitendo na hivyo kutambua uboa na udhaifu wa njia hiyo ya kupiga kura. Endapo wataona ni jambo linaloifaa Tanzania basi bila shaka watakuwa na hamasa ya kuja kulieleza, kulieneza na kulifanya likubalike hapa Afrika kwa urahisi.

Kama shabiki wa Teknohama nimekuwa nikijiuliza hivi kuna uwezekano wa kuwa na sanduku la kura lenye kutumia betri na linaloweza sio tu kupokea kura bali kuhakikisha halikubali kura mbaya na kisha kupiga hesabu ndani kwa ndani na kuonesha kwenye skrini juu yake kila mgombea kapata kura ngapi? Kisha boksi hilo liwe na uwezo wa kutuma majibu hayo kioto kwenda kwenye kompyuta kuu ya uchaguzi kiwilaya, kimkoa na kitaifa ?

Boksi hilo litakuwa na uwezo pia wa kuainisha vidole vya mpiga kura na kama namba yake inaendana na alama hiyo anakubalika na kama sivyo anakataliwa?

Simu za Mkononi
Kuna wanaofikiria pia upo uwezekano wa kutumia simu za mkononi maalum au za kawaida katika uchaguzi mkuu na upigaji kura wakati wowote.

Simu maalum za kupiga kura zitakuwa ni simu ambazo zinatumika kwa ajili hiyo tu na taifa litawajibika kumnunulia kila mpigaji kura simu yake kutokana na kodi za wananchi. Simu hiyo itanunuliwa mara moja tu katika maisha ya mtu. Na wale wanaokufa zitarekebishwa ili wapewe wapigaji kura wapya wanaoingia kwenye orodha ya wapiga kura baada ya kutimiza umri wao.

Aidha kwa simu za kawaida baada ya wananchi kuandikisha simu zao zote itachaguliwa namba moja mama itakayokubalika katika kupiga kura na masuala mengine ya kijamii na kiuchumi katika mfumo maalum wa kurahisisha na kupanua matumizi ya simu za mkononi.

Kwa kutumia namba ya simu yako iliyoandikishwa na inayokubalika baada ya kila kitu kuthibitishwa utaweza kupiga kura yako ukiwa unastarehe nyumbani kwako bila ya kwenda mahala ukacheleweshwa, kunyeshewa na mvua na kuchomwa na jua bila ya sababu ya maana. Jambo hili sio tu litawapa nafuu kubwa wapiga kura lakini pia litachangia idadi kubwa ya watu kupiga kura wakati wowote upigaji kura unapohitajika bila ya kugonja miaka mitano.

Itakuwa ni rahisi pia kufanya chaguzi ndogo kwa sababu gharama yake itakuwa ni ile tu ya uratibu na mawasiliano.

Kwa kifupi, Waafrika ambao ndio wanaokabiliwa na tatizo hili la wizi wa kura wanastahili kuwa mstari wa mbele kutafuta ufumbuzi wake. Mawazo haya ninaamini yanaweza yasifae au kukubalika lakini lengo langu la kuamsha mjadala kama Teknohama inaweza kutusaidia kuwa na chaguzi za huru, haki na zenye ukweli zaidi litakuwa limefanikiwa.