Saturday, June 27, 2009

DEMOKRASIA, UNDUGU NA UBAGUZI MPYA

Maana ya Undugu na Ubaguzi Mpya

Maana ya Undugu kwa muktadha huu ni pale mwanasiasa anapotumia nafasi aliyo nayo [akijua wake au chake haviwezi kukataliwa na wajumbe au wabunge-maana yeye ndiye anayewahakikishia kuwepo kwao na maslahi wanayopata, na kwa nafasi hiyo yeye kashika mpini na wanachama na wananchi kwa ujumla wameshika makali. ] kuwapa nafasi za kazi katika chama au serikali ndugu, watoto, wake, jamaa au marafiki zake. Undugu unapokithiri unamloga kiongozi kiasi cha kumfanya atake pia awe na sifa za kifalme falme, ikiwemo pia kurithisha uongozi kwa mwanae au yule amtakaye yeye na siyo yule wanayemtaka wanachama au wananchi. Na akiona anayemtaka hatakiwi anaweza akafanya yote yale ya kuwazaini na kuwatisha watu wake mpaka wakubali kumkubalia matakwa yake. Ingawa imekwishatokea pale watendaji wa chini wanapogundulika na viongozi wa juu kumpandikiza asiyetakikana kwa huyo aliyepandikizwa kuombwa kumuachia yule anayekubalika.

Wakati maana ya Ubaguzi wa aina mpya katika nchi nyingi za Kiafrika, Kiarabu na Kiasia
ni kuachiwa kuzuka kwa ubaguzi kati ya wananchi walio wanachama wa chama tawala na wale wasio wanachama wake. Hawa wanaweza kuwa wanachama wa vyama vingine vya kisiasa au wananchi ambao hawaoni umuhimu wa kuwa wanachama wa chama chochote cha kisiasa kwa kuwa wao malengo yao makubwa ni ya kiuchumi na kijamii na siasa kwao ni kikwazo na sio msaada au tajamali.

Kwa kuwa chama tawala ndicho kinachoshika serikali basi kinachotokea ni kuwa wanachama wake hupewa vyeo vyote katika nchi hata kama uwezo wao katika hilo ni mdogo au hawana uwezo kabisa. Inakuwa nadra sana kwa asiye mwanachama wa chama tawala kupewa nafasi yoyote ya maana katika kuchangia maendeleo ya nchi na watu wake. Huu ndio ubaguzi mpya. Na kadri demokrasia inavyokuwa dhaifu katika nchi ndivyo ubaguzi huo unavyoshamiri katika nchi ambayo badala ya kwenda mbele kidemokrasia na kimaendeleo huwa inarudi kinyume nyume.

Afrika ilipinga vikali kuwepo kwa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini. Hii leo nchi zenye tabia za kufanya baadhi ya watu wao watumwa zinatazamwa kwa jicho la hasira. Katika nchi mbalimbali za Kiafrika ubaguzi wa kijinsia uko mashakani. Wanawake sasa sio tu wanasemwa ni huru lakini wanaonekana kuwa huru kuliko huko nyuma. Wasiojiweza na walemavu nao hawakuachwa nyuma. Wote wanajua sasa kwamba wana haki sawa na raia au watu wengine nchini mwao. Haya yote yanaonesha kuwa Waafrika kwa asili yao hawakubali na hawapendi ubaguzi.

La ajabu ni kuwa ujio wa siasa za mfumo wa vyama vingi umekuja na aina mpya ya ubaguzi au 'apartheid' ya kisiasa kama sio ki-chama.

Watu wengi bado hawajaujua kwa undani ubaguzi huu unavyokwenda. Katika makala haya tutajaribu kuonesha jinsi ubaguzi huu ulivyo na unavyoendeshwa.

Ubaguzi wa kichama au kisiasa Afrika unajionesha kwa sura au njia mbalimbali. Kubwa kati ya hizo ni ule ubaguzi unaofanyika katika masuala ya nafasi za kazi,
mikopo na masuala ya fedha,misaada, ujenzi wa miundo-mbinu, elimu. afya, uongozi na fursa nyingine za kiuchumi na kijamii.

Aidha ubaguzi huo upo pia katika kuchagua wafanyakazi kwa ajili ya nafasi za ukatibu mkuu, balozi za nchi za nje, wakuu wa mikoa na wilaya, wakuu wa mashirika, wakuu wa tume au kamisheni mbalimbali, wakuu wa polisi, wakuu wa vyuo, wakuu wa mahospitali, wakuu wa mabenki au taasisi za fedha za umma na wakuu wa serikali za mitaa.

Vilevile kuna ubaguzi pia katika nafasi za masomo ya nje na uteuzi wa wajumbe wa bodi na tume mbalimbali nchini na wakuu wa vyombo vya habari vya serikali/umma.

Kwa upande mwingine wazee, wazazi, vijana
na wanawake aghalabu wa chama tawala huonekana kupendelewa na kupewa haki, fursa na neema zaidi kuliko wale wasio wanachama.

Katika utendaji kazi za serikali aghalabu utakuta mambo yanakuwa ni rahisi na nafuu zaidi kwa wale walio wanachama wa chama tawala kuliko kwa wale wasio wanachama wa chama hicho. Na hata pale serikali inapponesha kuvumiliwa mfumo wa vyama vingi, wapinzani hulazimika kujificha kwa sababu moja au nyingine.

Sio kwamba chama husika hakijui inachokifanya. Inajua vizuri sana. Hufanya hivyo ili kuhakikisha kuwa kinaendelea kujenga mapenzi kati yake na makundi hayo ili uchaguzi unapofika iwe ni rahisi chama hicho kuchaguliwa kuliko chama kingine.


Kwa kufanya hivyo chama tawala hujenga ukuta kati ya wanachama wake na wanachama wa vyama vingine.

Hili linakuwa ni rahsi kufanyika kwa sababu katika Afrika mpaka kati ya serikali na chama tawala huonekana kwa shida sana. Kwa nchi nyingi mpaka huo ni kitu kisichokuwepo.

Kwa kuwa Gavana wa Benki anakuwa ni mtu wao inakuwa ni rahisi kumuamuru kuiba fedha hazina na kuwapa makuwadi na walanguzi wa chama ambao aghalabu huwa hawazifikishi zote. Ni asilimia ndogo tu hatimaye inayotiririkia kwenye kibakuli cha chama husika.

Kwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kodi ya Nchi fulani ni mtu wao inakuwa ni rahisi kiongozi wa chama kuamrisha mtu au kampuni fulani idaiwe kodi isipostahili au kodi kubwa kwa lengo la kumkomoa tu mtu huyo au kampuni hiyo kwa kutumia mabavu ya kisiasa.

Katika nchi nyingi kuna wazawa wengi tu wanaoweza kuwekeza katika nchi zao pengine uwekezaji wao ukashinda hata ule wa nje. Lakini kwa sababu ya vitendo vya uonevu na dhuluma wanayofanyiwa na chama tawala huamua kutofanya chochote na kuziweka tu fedha zao au kutanua kwani wanaona ni ujinga mtu kuingizwa matatani kwa sababu ya fedha zake mwenyewe.

Ubaguzi upo kila mahala, lakini kwa sababu za nafasi tuoneshe tu mifano michache ambayo yeyote yule anaweza kuipanua ikafikia kote kule anakotaka.

Katika nafasi za kazi kwa mfano kwa ajili ya mashirika ya umma, balozi za nje na mashirika ya kimaeneo na kimataifa ni dhahiri kuwa wanachama wa chama tawala ndio wanaochaguliwa zaidi sikuzote na hutokea kwa bahati mbaya tu akachaguliwa mtu ambaye sio kada wa chama tawala.

Matokeo ya hili ni kwamba mara nyingi unakuta watu wasiokuwa na uwezo wanapewa kazi au nafasi ambazo hawaziwezi na mwisho kuishia kuharibu kazi na kuziangusha taasisi wanazotakiwa kuziendesha. Hivi leo vipaji na uwezo wa Waafrika walio wengi wakiwemo Watanzania vimezikwa au vinafichwa na havitambuliki kutokana na ubaguzi wa kichama unaoendelea.

Katika nafasi za masomo ingia katika Wizara yoyote ya Elimu katika nchi mbalimbali za Afrika ufanye utafiti na utagundua watu wanaopewa nafasi nzuri za masomo ya juu ni watoto wa wanasiasa au makatibu wakuu wa wizara husika na watu kama hao na watumishi katika wizara hizo.

Katika nchi za Kiafrika vyama tawala vilitumia nafasi ile kabla ya kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi kupora majumba, viwanja vya michezo, viwanja na rasilimali zingine na kuzifanya ni zao. Apartheid ya kisiasa katika baadhi ya nchi imekuzwa sana pale chama tawala kilivyopora au kunyakua kinachostahili kuwa cha wote, baadhi ya vitu vilivyoporwa ni pamoja na:
-redio,
-magazeti,
-televisheni,
-viwanja vya michezo
-kumbi za mikutano au jamii
-maeneo ya maegesho
-vijiwe
-shule
-vyuo
-biashara
-ardhi na viwanja vilivyopimwa.

Hii ilikuwa bahati yao. Baya kwa hivi sasa ni kwa chama tawala kukataa kurudisha kile kilicho haki ya wananchi wote na kisha kuvinyima vyama mbadala nafasi ya kuwa na mali kama ilizonazo.

Wazee, wazazi, vijana na wanawake wa taifa au ?
Hili la wazazi, wazee, vijana na wanawake wa chama fulani kupata upendeleo sio tu linaleta ubaguzi wa kichama na kisiasa lakini pia linaigawa nchi katika makundi ya wazazi, wazee, vijana na wanawake wa chama tawala na wazazi, wazee, vijana na wanawake ama wasio na chama cha kuwapendelea na kuwasaidia au wale wa vyama mbadala. Huu ni mwanzo wa wanasiasa hapo baadaye kuyatumia makundi hayo kusababisha fujo, ghasia na uvunjaji amani wa aina nyingine hapa nchini.

Kwa maoni yangu, chini ya mfumo wa vyama vingi ni bora kama makundi ya wazazi, wazee, vijana na wanawake yatakuwa ni makundi huru yasiyo na mshkamano na chama chochote cha kisiasa. Au makundi hayo basi yaonekane ni ya kichama na yasipewe kiujanja ujanja sura ya kwamba ni jumuiya za kitaifa. Vinginevyo, makundi hayo yasibague kati ya wanachama wa chama tawala na wale wa vyama vingine au wasio wanachama. Na misaada inapokuja isipitishwa kijanja kusaidia jumuiya hizo kama vile ni za kitaifa kumbe ni za chama kimoja tu cha kisiasa.

Sababu kubwa za kuwepo kwa ubaguzi wa kisiasa au kichama ni ule ukweli kwamba rasilimali na hasa fedha ambazo chama tawala inaweza kuwa nazo wakati wote ni kidogo. Licha ya hivyo kama ilivyo kwa taasisi nyingine yoyote wakubwa hujipendelea kwanza wao na kisha makombo yanayobakia ndio hupewa wanachama.

Makombo hayo pia ni dhahiri hayatoshi. Na kutokana na hili hata wanachama wenyewe ndani ya chama sioi wote wanaopata na kama wanapata hawapati kwa usawa. Sikuzote kuna wanaopata zaidi ya wengine.

Ikifikia hapa ni dhahiri kuona kuwa endapo chama tawala kitafanya ujanja na kikapata fedha kwa njia halali au za kiwiziwizi bado kiasi kinachopatikana hakitoshi kuwagawiwa na wasio wanachama. Hapa ndipo ubaguzi unapoanza na kisha kuendelea siku zote chama hicho kitakavyokuwa madarakani.

Kwa hiyo hatimaye ubaguzi ulioanza kisiasa au kichama huanza kuingia kuwa ubaguzi wa kijamii (matabaka ya wanaopendelewa na wasiopendelewa) kisha ubaguzi wa kijamii huwa ubaguzi wa kiuchumi (walio nacho hupewa zaidi na wasio nacho hunyang'anywa hata kile kidogo walicho nacho) na kisha kukomalia kuwa ubaguzi wa kiraia na kimaeneo ambao huzaa makundi ya watu ambao kufa kupona hukipigia chama fulani tu kura lakini sio chama kingine.

Ubaguzi wa kichama au kisiasa kama ulivyokuwa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini sio kitu chema na hakiashirii kuendelea kwa umoja, amani na mshikamano wa kitaifa bali kinyume chake. Chama chochote ambacho huwagawa wananchi kati ya wale ambao ni wanachama wake na wale ambao sio wanachama wake wakati kikiwa serikalini sio chama kinachostahili kuwa madarakani hata siku moja.

Apartheid ya kisiasa inaanzishwa na kuendelezwa Afrika kwa malengo ya chama fulani kupata wafuasi watumainiwa na wasiokitupa chama hadi pale hao wanachama wanapotupwa. Hili linaingiza gharama isiyoonekana kiuchumi ya kuwafadhili watu wasiochangia lolote katika ukuaji wa uchumi wa nchi husika.

Kutokana na kuwa rasilimali ikiwemo fedha ni chache na adimu vyama tawala katika nchi nyingi vinaona ni rahisi kugawa wananchi kati ya wananchi wake na wananchi wasio wananchi wake. Baada ya hapo inakuwa ni rahisi kuwatumia watu hao ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. Aghalabu, wananchi wanaokubalika na chama tawala kutokana na ama kuwa wanachama au wapiganaji wake kisiasa ndio wanaopata misaada mbalimbali inayotolewa kwa watu wote. Katika baadhi ya nchi imefikia kwamba hata wakati wa maafa, watumishi wa serikali au wafuasi wa chama tawala wanaopewa majukumu ya misaada hubagua kati ya wenzetu na wengine. Hawa wenzetu ndio wanaofikiriwa na kupata kwanza, wakati wengine huachwa bila huruma wala msaada wowote. Katika tathmini ya mali iliyoharibika 'mwenzetu' sio tu analipwa zaidi lakini juu ya hivyo huweza akapewa na mkopo usiorudishwa pia.

Rushwa ya kisiaasa.

Apartheid ya kisiasa ni rushwa kama zilivyo rushwa nyingine. Wapenda demokrasia wote wanapaswa kuipiga vita kwa ukucha na jino. Ni rushwa mbaya zaidi maana inatumia umasikini na unyonge wa mwananchi kumlazimisha raia kujiunga na chama fulani au kukipigia chama fulani kura hata kama yeye moyoni hakipendi na hakitaki chama hicho.

Nimewahi kuzungumza huko nyuma kwamba rushwa mbalimbali tunazoziona katika nchi yetu asili na chanzo chake ni wanasiasa. Rushwa ikishapangisha kwenye ghorofa ya juu kabisa ya nchi kupitia chama tawala basi inakuwa ni vigumu sana kuipiga rushwa vita katika ghorofa za chini. Na hii ndiyo hali iliyopo katika nchi nyingi za Kiafrika. Rushwa imo katika chama tawala na chama tawala kinapona na kubakia madarakani kutokana na rushwa na sasa inakuwa ni kazi kuwa na uhakika kwamba kinaweza kurudi tena madarakani bila kupewa na chenyewe kutoa rushwa.

Faida za apartheid ya kisiasa

Zaidi ya manufaa ambayo viongozi na chama fulani hupata apartheid ya kisiasa haina faida kwa wananchi walio wengi na nchi husika.

Hasara za Apartheid ya kisiasa

Hasara ya kwanza ni kuwagawa wananchi kati ya wanachama na wasio wanachama. Jambo hili huongeza jeuri, kiburi na ujibari wa wanachama wa chama tawala dhidi ya wananchi wenzao.
Katika hali kama hii kuna kuwa hakuna amani, kuaminiana wala mshikamano kati ya wananchi.

PIli, apartheid ya kisiasa huwanyang'anya walio wengi kipato na kipato hicho kupewa watu wasiostahili kukipata. Matokeo yake ni kuwa na wanasiasa uchwara ambao fedha huwalewesha wakajihusisha na uchafu wa kila aina na kusahau majukumu yao kama viongozi na wasimamizi wa maendeleo ya watu na nchi yao.

Tatu, vyombo vya dola hulazimika kupendelea kabila moja (wanachama) dhidi ya makabila mengine (wasio wanachama) na hatari ya hili ni kwamba dhuluma na unyanyasaji ukizidi nchi 'inarwandishiwa'.

Nne, katika jamii yoyote asilimia ya watu walio na akili ya kuleta maendeleo ya watu wote ni chini ya asilimia nne. Hawa wamegawanyika sio kwa kufuata uzawa, kabila, makazi au jinsia bali kwa namna isiyoeleweka na isiyotambulika. Lakini katika kundi lolote la watu ukilichunguza utakuta halina zaidi ya asilimia hiyo nne, aghalabu, idadi huwa chini ya hapo. Katika Afrika asilimia hii inasemekana kushuka chini hadi 2 kama sio moja tu.

Unapojenga apartheid ya kisiasa, kwa bahati mbaya wewe ukawa na 'wajinga' zaidi kuliko wale 'wenye akili' ndio unajenga safu za uongozi usiokubali kukosolewa, ambao ukifanya madudu bado unaona umefanya sawa tu na unaoamini siku zote wao ni bora na safi zaidi kuliko watu wengine na kinachotokea ni wao kuonewa tu wivu na wale waliokosa. Kiburi na dharau hii ya kutupwa haiwezi kamwe kujenga taifa bora na imara.

Huko Afrika Mashariki kwa mfano katika kisiwa cha Zanzibar wananchi wengi waliojaliwa akili na ujasiriamali wametengwa na waliomo serikalini. Na katika kijinchi hicho inavyoelekea wenye majaliwa ni chini ya asilimia 2 na wote hawa wamewekwa nje ya serikali. Matokeo ya hili yako wazi kwa yeyote mwenye macho kwenda kusikia na kuona hao waliobeba jukumu la uongozi katika sehemu hiyo ya Afrika Mashariki. Laiti isingelikuwa kubebwa na Tanzania bara, Wazanzibari wanaofanya kazi nje, biashara za kiajabuajabu na misaada toka nje leo wanavisiwa hao wangelikuwa wakitembelea magoti.

Wengi wa wanaojifanya ni wanachama wa chama hiki au kile Afrika wanafanya hivyo kutokana na njaa au uoga.
Aghalabu kwa kuwa mara nyingi chama tawala huonekana kwamba ndio walioshika mpini, basi wananchi walioshika makali wanaogopa wasikikaidi kisha kikavuta mpini huo kwa hasara yao. Hili halina dawa nyingine bali kuhakikisha kuwa wanaoshika mpini ni wananchi na sio chama chochote kile cha kisiasa kwa kuimarisha na kukuza demokrasia inayofanya kazi Afrika.

Kama tulivyokataa apartheid na ubaguzi wa aina nyingine hapa Afrika lazima wapendwa Uafrika na Waafrika wa kweli hapa duniani wakatae kabisa ubaguzi wa kichama. Lazima tulee familia, koo, mitaa, kata, tarafa, wilaya na mikoa ambayo sisi sote bila kujali ni wanachama wa chama fulani tunachukuliana kama watoto wenye sifa na tabia tofauti ambazo ni lazima tuviumiliane kama tunataka tuishi kwa amani na upendo.

Wanaochgia kasi ya kukua kwa ukabila wa kichama ni 'washangiliaji' na wala sio watendaji na wazalishaji mali wa kutegemewa na watu na nchi zetu.

Nini kifanyike ?

Jambo la kwanza la kufanya kabla ya kuchukua hatua zinazofaa kuirejesha hali kama ilivyokuwa kabla ya leo ni pamoja na kujiuliza:

Je, kuna chama chochote mtaani, wilayani au mkoani kinachoweza kuanzisha jambo la manufaa bila kukwaza na serikali ?

Je, kuna wanachama wa chama chochote isipokuwa chama tawala wanaoweza kukutana au kufanya maandamano bila kuingiliwa na vyombo vya dola ?

Je, mfanyabiashara akikiunga mkono au kukipigia debe chama kingine isipokuwa chama tawala biashara na mali zake zitakuwa salama ?

Je, chama chochote cha siasa kinaruhusiwa kujenga viwanja vya michezo, shule, hospitali na majengo mengine bila bughudha ?

Je, vyama vya upinzani vinaruhusiwa kuwa na vyombo vyao vya habari ?

Je, nini kinatokea kama chombo fulani cha habari kinaunga mkono au kuwatangaza zaidi upinzani kuliko chama tawala ?

Je, usipokuwa mwanacha wa chama tawala ajira yako na kupanda kwako cheo na maslahi yako yanakuwa sawa na wale wa chama tawala ?

Je, watoto na wake wa wasiokuwa katika chama tawala wanapata jamala na nyenzo sawa na wale wa chama tawala ?

Majibu kwa maswali haya yatatoa njia na mbinu za kushughulikia ukabila au ubaguzi wa kichama katika nchi zetu kwa namna bora na ya uhakika zaidi.

© 2009 Sammy W.I.Makilla

Sunday, June 21, 2009

DEMOKRASIA NA VYOMBO VYA DOLA

Maana ya Vyombo vya Dola

Vyombo vya Dola ni vyombo vyote ambavyo huwepo ili kulinda amani ya wote au amani ya wachache kulingana na hali itakavyokuwa ili mradi anayetoa amri ya mwisho kwa vyombo hivyo ndiye mkuu wa nchi. Katika demokrasia halisi vyombo vya dola hutumika kuwalinda wananchi wote na havitumiki kuwalinda wachache au wakubwa fulani tu katika nchi. Katika demokrasia finyu au chipukizi au demokrasia inayoorojeshwa au kuwekwa pembeni kabisa vyombo vya dola hutumika kuwadhibiti wananchi ili watawala wasibughudhiwe katika mabaya au mazuri wanayowafanyia watu wao. Kwa maneno mengine, vyombo vya dola vinaweza kutumika kuimarisha haki, uhuru na demokrasia ya watu au kinyume cha hivyo.


Katika demokrasia ya kweli ni muhali kwa wanajeshi au askari polisi au mgambo au makundi mengine ya kiulinzi yaliyoidhinishwa na bunge kuwaelekezea mtutu wananchi.
Vyombo vya dola havitumiki kuleta fujo na madhara kwa wananchi bali kuepusha mambo hayo, hata kama inabidi, polisi au askari kuteseka au kuumia au hata kufa.

Urithi wa mkoloni uliokubalika

Urithi ambao Mwafrika kiongozi aliukubali kwa mikono miwili ni ule wa vyombo vya dola. Aidha kwa kuhofia udhaifu wao na uwezo wao wa kuwatimizia watu wao mahitaji na matakwa yao viongozi wengi wa Afrika wameendelea kuvitumia vyombo vya dola kwa kazi ileile iliyofanywa wakati wa mkoloni nayo ni ile ya kumdhibiti mwananchi ili aibiwe, anyonywe, adhalilishwe, adhulumiwe na asifurukute kwenda upande wowote anaoweza kujichomoa.

Katika Afrika hili linakuwa rahisi kwa sababu karibu polisi na walinzi wote hulipwa mshahara mdogo sana ambao unawaingiza katika vishawishi vya aina nyingi. Vishawishi hivyo ni pamoja vile vya rushw ya fedha na rushwa za kisiasa na kiuongozi.

Kwa kuwa mkuu wa nchi ndiye anayetoa fadhila kwa fulani kuwa mkuu wa polisi au majeshi na kadhalika msururu wote wa watumishi katika vyombo vya dola huelekeza utii wao sio kwa raia ila kwa rais wa nchi na watu wake maalum au vyombo vyake vingine. Katika hali kama hii walio wengi katika vyombo vya dola kama tulivyoona kule Zimbabwe, Kenya, Liberia, Misri na kadhalika ni rahisi sana kutumiwa kwa maslahai yasiyo ya wananchi.

Kila nchi huwatumia polisi ili kudhibiti uhalifu na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao. Aidha polisi hutumika ili kuhakikisha kuna ustaarabu na utaratibu unaokubalika wakati wa maingiliano ya watu katika shughuli zao mbalimbali za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

Majukumu mengine waliyonayo polisi zaidi ya kupambana na uhalifu ni pamoja na: upatanishi kati ya wagombanao, usalama barabarani na kutoa msaada wakati wa maafa.

Majukumu haya yanatekelezwa kwa viwango tofauti katika nchi mbalimbali kulingana na uchanga au ukomavu wa demokrasia ya nchi.

Polisi kama kiungo muhimu katika demokrasia
Polisi ni kiungo muhimu katika ujenzi wa demokrasia. Ili mradi kiungo hicho kinatimiza yafuatayo:
1. Kufanya kazi kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi na sio kwa kufuata amri au matakwa ya kiongozi mbabe au chama chenye kuendekeza udikteta;
2. Kuingilia kati maisha ya raia pale tu ambapo ni lazima kabisa lakini kwa umakini na uangalifu ili kutosababisha hasara ya maisha au mali; na
3. Wanawajibika kwa wananchi wote na sio kwa kikundi fulani cha watu katika nchi.

Hata hivyo sio kweli kuwa ni polisi tu wanaoweza kuepusha ghasia au fujo ili pawepo na utulivu, mshikamano na amani katika jamii. Yapo mambo kadhaa ambayo kwa pamoja na mchango wa polisi ndio yanayoweza kuihakikishia nchi umoja na amani ya kudumu. Mambo hayo ni pamoja na:
. jamii kuwa na maadili na tabia zinazokubalika katika maingiliano yake,kwa maneno mengine, hili linalazimisha watu kutambua kwa dhahiri na bayana ni nini ni uovu na nini ni wema, nini ni dhuluma na nini ni haki, nini ni ukweli na nini ni uongo;
. shauku ya kila mtu kutaka kuthaminiwa na kuheshimiwa na wanajamii wenzake,
. ushirikiano na kusaidiana kwa wanajamii, na
. haja ya ulinzi na kupambana na mazingira yanayoizunguka jamii.

Polisi ni muhimu kwa sababu wao peke yao kisheria ndio wanaoruhusiwa tu kutumia nguvu na kuwanyima watu uhuru wao.

Uwezo huu wa polisi unaweza kukubalika na watu fulani katika jamii (kwa kuwa polisi wanawalinda au kuwasaidia) lakini ndio huohuo unaoweza kutafsiriwa kwamba ni mabavu na uonevu na kundi linaloamini linanyimwa uhuru au haki zao za kimsingi.

Uwezo huo wa polisi kwa kweli pia unatoa mwanywa wa polisi kufanya kile wanachokitaka hata ikiwa ni kinyume cha sheria.

Utekelezaji wa kazi za upolisi katika jamii yoyote ya kidemokrasia huhitaji mizania linganifu wakati wote. Maana ukweli ni kuwa polisi wanaweza wakawa ama msaada mkubwa au hatari kubwa kwa demokrasia ya nchi fulani.

Uwezo wa polisi kutumia nguvu, kutoa adhabu za papo kwa hapo, kufuatilia na kuwapeleleza watu kwa siri hivi hivi au kwa kutumia teknolojia, kuwasimamisha, kuwasachi na kuwakamata watu kunaweza kutumika kusaidia udikteta ulioko madarakani kirahisi tu.

Polisi ni neno linalotokana na neno 'polity' ambalo huko Ulaya miaka 500 iliyopita lilitumiwa kuonesha aina ya serikali inayosimamiwa na chombo cha kisiasa. Chombo hicho kilihusishwa zaidi na maisha, afya na mali za watu. Nchi hazikuwa na polisi tunaowajua leo. Waliofanya kazi hizo walikuwa ni askari au watu maalum wa kuteuliwa na viongozi.
Katika karne ya 18 polisi wakawa wanajihusisha zaidi na masuala ya ndani na usalama wa watu.

Polepole, polisi ikageuka na kukengeuka baada ya dhana ya nchi huru zanye mipaka kuibuka kuwa taasisi ya kulinda mipaka ya nchi, usalama wa ndani na kudhibiti kisheria maingiliano ya watu katika maisha yao ya kila siku.

Nchi zinahitaji polisi wa kidemokrasia sio kikoloni

Hivi leo tunazungumzia jinsi ya kuwa na jeshi la polisi linaloendana na kanuni za kidemokrasia. Polisi wa kidemokrasia wana sifa zipi? Ni rahisi kwa kweli kueleza au kufafanua polisi wasio na mwelekeo wa kidemokrasia wakoje. Hii ni kwa sababu ni wale wote wanaovunja karibu kila msingi na kanuni ya demokrasia. Hata hivyo, tutajitahidi kuelezea kwa kifupi hapa ni namna gani polisi wa kidemokrasia wanatakiwa kuwa.

Polisi wa kidemokrasia kwa kawaida huwa na sifa hizi: hufanya kazi kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi na sio kwa matakwa ya mkuu wa nchi au wanasiasa. Polisi hutumiwa nguvu na uwezo wao kwa umakini, uangalifu na kwa kuwajali sana wananchi. Mahalani, Uingereza, kwa ridhaa ya wananchi, hairuhusu polisi wake kutembea na silaha. Watu hutii polisi kwa kuwaheshimu kutokana na jukumu lao kijamii na sio kwa kutishwa.

Kazi za polisi wa kidemokrasia hujulikana kutokana na jinsi wanavyofanya kazi zao na namna wanavyofikia malengo yao. Mambo kama utesaji, kuua watuhumiwa papo kwa hapo, kuteka watu nyara au kuwakamata na kuwajeruhi watoto, ndugu au jamaa wa mtuhimiwa huwa hayakubaliki na hukatazwa kisheria.

Masuala kama kutumia nguvu au kumnyima mtu uhuru wake au kuwahoji watuhumiwa hufanyika kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na kwa ruhusa kutoka kiongozi au mamlaka husika.

Kwa ufupi polisi huwa na haki tu ya kumkamata mtuhumiwa lakini hawana haki ya kuchukua sheria mkononi mwao. Jambo ambalo sasa mara kwa mara linaonekana la kawaida katika jamii yetu.

Ni wajibu wa polisi wa kidemokrasia kuhakikisha sikuzote kuwa mtawala na mtawaliwa, tajiri na masikini, mnyonge na mwenye nguvu hakuna anayekuwa juu ya katiba na sheria za nchi.

Sio lazima polisi wa demokrasia nchini mwetu wafanane na wale wa nchi nyingine. Lakini ni lazima kwa polisi kuhakikisha kuwa wanawajibika kwa walipa kodi na sio kwa watawala au wale ambao kuwepo kwao kama wao kunategemea kodi anayolpa mwananchi. Baada ya hapa mengine yanakuwa ni rahisi.


Kukua na kukomaa kwa demokrasia kunategemea sana jinsi jeshi la polisi linavyolelewa katika nchi husika.

Vyama tawala visihodhi polisi

Viongozi wa chama tawala katika nchi husika wanaweza wakalilea jeshi la polisi kama vile ni jeshi la kulinda chama tawala na viongozi wake. Au wanaweza wakalilea jeshi hilo kama lenye kuwajibika kwa wananchi wote bila kujali wanatokea chama gani.

Dhuluma, uonevu, wizi na ubabe katika siasa, aghalabu, hutokea pale ambapo jeshi la polisi linalelewa kwa namna ile ya kwanza.

Hili huzaa hali ya polisi kuona kwamba chama tawala, viongozi na wanachama wake kwamba wao sikuzote ndio wenye haki, wenye kusema ukweli na walio safi kuliko wanajamii wengine na makundi au vyama vyao vya kisiasa na visivyo vya kisiasa. Tatizo linakuja pale ambapo chama husika kinakuwa ndio mwizi au jambazi na wengine ndio wanaoibiwa au kudhulumiwa. Polisi wa nchi atasimama wapi ?

Katika hali kama hii wananchi wasiokiunga chama tawala mkono na hususan wanachma na viongozi wa vyama mbadala huonekna sikuzote ni wakorofi, wabishi na wavunja sheria.

Uhusiano wa polisi na chama tawala kwa hiyo huwa ni wawenzetu na ule wa jeshi hilo na wasio wanachama wa chama tawala huwa ni uhusiano na wahalifu au wahalifu watarajiwa.

Haya yote yanaonesha upo umuhimu wa kurejea vipengele katika katiba ya nchi (na kama tutakuwa na katiba mpya ni vyema zaidi) ili kuweka uhusiano wa polisi na viongozi kwa upnade mmoja na polisi na wananchi kwa upande mwingine bayana. Katika marejeo hayo izingatiwe kuwa ni kosa kwa polisi kutumiwa na chama chohcote cha kisiasa, kikiwemo, pia chama tawala. Na endapo hili linakiukwa basi wananchi wawe na haki ya kulishtaki jeshi hilo kwa kuvunja katiba na sheria za nchi.

Nani kumteua polisi mkuu

Jeshi la polisi, hata hvyo, haliwezi kubadilika kama wakuu wa polisi wataendelea kuchaguliwa na rais na sio bunge au Jaji mkuu kama jaji huyo ndiye anayechaguliwa na bunge. Uoga wa makamanda wengi kuwa wanaweza wakatemwa na chama tawala kama wasipokipendelea chama hicho na kuvionea vyama mbadala utatoweka mara moja kama kamanda huyo atakuwa hawezi kufukuzwa kazi na rais au waziri mkuu au kiongozi mwingine wa serikali.

Katika miaka hii ambayo tunazungumzia pia kuwa na wizara chache na wizara zilizo nyingi kugeuzwa kuwa ni wakala, kamisheni, tume au taasisi maalum ni muhimu pia kuangalia ni jinsi gani jeshi hilo linaweza kugeuzwa kuwa la kukuza na kupanua demokrasia zaidi na sio jeshi la kukwaza na kuidhofisha.

Hili litahitaji jeshi letu kutokuendelea kuwa la kupokea amri za kikoloni, kibabe na kidhulumati na kutumia mabavu badala ya busara na hekima ili kujenga udugu na mshikamano muafaka katika jamii husika. Jambo ambalo husaidia wananchi kujipolisi wao wenyewe.

Aidha, hili litasaidia kuzika tabia iliyozika ya baadhi ya vyama vya siasa Afrika kujijenga kwa kuruhusu baadhi ya wanajamii kuvunja sheria za nchi na kuwalinda.

Masharti ya matumizi bora ya polisi

Ili haya yote yafanikiwe ni muhimu mambo kadhaa kufanyika:

Kwanza, lazima pawe na jitihada zinazoonekana kufanyika na kuendelezwa wakati wote na kuzuia polisi kutumiwa na chama cha kisiasa hata kama kikiwa ni chama tawala wakati huo. Katika misingi ya utawala wa kisheria hakuna chama kinachostahili kuwa juu ya sheria katika demokrasia. Vyote lazima viwe chini ya sheria. Kazi nyeti zaidi itakuwa ni kwa jeshi hilo kujua namna ya kutenga kati ya mambo ya serikali na yale ya chama au vyama tawala vya wakati huo. Na pasiwe na raia yeyote anayeweza kuonewa au kunyanyaswa kwa kuwa amefuata sheria za nchi nukta baada ya nukta.

Polisi nao wanapaswa kuwa chini ya sheria- ikiwa ni sehemu muhimu ya uwajibikaji katika mfumo wa vyama vingi. Hili lisipofanyika ni rahisi kutoa mwanya kwa watu wezi, wauaji, wauza madawa na kama hao kujipenyeza ndani ya jeshi hilo na kuunda dola ndani ya dola au serikali ndani ya serikali. Angalia kinachofanyika sasa Algeria, Arbezeijan, Kenya, Kongo, Burundi, Ethiopia, Misri, Moldovia, Burma, Mexico, Colombia na Zimbabwe.

Kurejesha imani ya wananchi kwa jeshi la polisi kama ilivyokuwa katika siku za mwanzo za uhuru itatupasa tuyasuke upya majeshi yetu ya polisi. Polisi na wananchi laizma wawe ni pande mbili zinazotegemeana kwa faid aya jamhuri nzima. Pasiwe na upand unaougeuza upande mwingine kuwa ni buzi la kuchuna mchana kweupe!

Ili uhuru, usawa na haki viimarike katika nchi ni muhimu sana kwa jeshi la polisi kuonekana kama ni walinda haki na watu sio tu wanaokubalika bali wanaothaminiwa sana na jamii. Mfumo unaowafanya wananchi walione jeshi la polisi kama ni jeshi la watu wabaya na wasioaminika haliwezi kujenga jamii bora na nchi inayoheshimika. Na mara nyingi hali hutokea pale jeshi hilo linapogeuzwa kuwa ni jeshi la 'wanyama wakali' waliokusanywa kumlinda mmiliki wao hata kama mmiliki huyo akiwa jambazi.

Ndio kusema kwamba jeshi la polisi linastahili kurudishwa chuoni. Huko watajifunza kuwa demokrasia sio tu jambo zuri kwa nchi bali kwao pia na kwa wananchi wenzao.

Itapaswa wajue kwamba raia ni dada, kaka, baba, mama, bibi na babu zao. Na chochote wanachokifanya kiwe kizuri au kibaya hakiwezi kutoka nje ya mduara ambao wote tunacheza humo.

Wito wa polisi katika nchi inayotaka kujenga demokrasia inayofanya kazi kikwelikweli ni lazima uwe -'usalama na ulinzi kwa wote bila kubagua.'

Kukua na kuimarika demokrasia na polisi
Zipo njia mbalimbali ambazo nchi inaweza ikatumia ili kukuza na kupanua demokrasia. Njia hizo ni pamoja kwa haraka haraka na masuala kama:

. Kutenganisha kazi zao na masuala ya kisiasa.
. Kutokubali kuingizwa katika hali au mitego inayoweza kusababisha wao kuwa ndio waanzishaji fujo mahala fulani. Hii ni pamoja na kukataa kuingia kwenye maeneo ya shule na vyuo. Tabia iliyozuka siku za karibuni kuruhusu mkuu wa shule kuwaita polisi au wanajeshi kuvamia vyuo sio uamuzi wa busara wala hekima. Kila shule au chuo kinastahili kuwa na walinzi wake wanaotenda haki kwa wote bila kujali nafasi au cheo cha mtu katika taasisi husika;
. Kurahisisha na sio kuzuia kufanyika kwa mikutano na maandamano ya wananchi. Ni kosa la katiba na kisheria kuwazuia wananchi popote pale nchini kufanya mikutano au maandamano;
. Kuhakikisha kuna mwingiliano kati ya mapolisi na raia kupitia mambo mbalimbali kama vile michezo, starehe, uwekezaji na shughuli za maendeleo ya kijamii.
. Kusaidia makundi ya kijamii ikiwemo vyama vya kisiasa kuendesha mambo yao katika hali ya utulivu na usalama.
. Kutokubali kuwepo kwa wezi, makuwadi, vibaka, dhulumati, wala rushwa, walevi, wazinzi, matapeli na wababishaji katika jeshi hilo.

Ikiwa hayo hapo juu yatafnyika bila shaka kutakuwa na uhusiano mzuri kati ya polisi na jamii. Uhusiano mzuri kati ya polisi na jamii huchangia kwa kiasi kikubwa kuchanua na kustawi kwa demokrasia na shughuli zote zinazoendana na ujenzi wake.

Aidha Polisi wanastahili pia kufanya kazi kwa ushirikiano na ukaribu zaidi na mahakama, bunge na viongozi wa kijamii ili kukuza na kupanua demokrasia wakati wote.


Polisi ni watumishi sio mabwana
Aidha serikali na wakuu wa polisi wakati mwingine hujisahau na kudhani kuwa wao ni mabwana na wananchi ni watwana. Katika demokrasia inayofanya kazi sawasawa yeyote anayejisahau kwamba ni mtumishi wa wananchi anapaswa kuondolewa mara moja na nafasi yake kuchukuliwa na yule anayetambua ukweli huu kuwa watumishi wa serikali wakiwmo polisi ni watumishi wa wananchi na sio mabwana wao. Hili la polisi kuwa watumishi na sio mabwana ni jambo muhimu sana. Ni pale ambapo aghalabu polisi wamepewa vichwa na viongozi kisha wakajiona wao ndio mabwana kwa sababu wana silaha na nguvu za dola ndipo ambapo nchi zimechafuka na kutokea uvunjaji haki wa kutisha na hata mauaji ya kimbari. Tuliepuke hili kwa kuwakumbusha polisi wetu sikuzote kuwa wao ni watumishi wa watu na sio mabwana.


© 2009 Sammy W.I.Makilla

Saturday, June 13, 2009

DEMOKRASIA, VYAMA NA HAZINA

Marx na Demokrasia.
YULE mkomunisti maarufu duniani mwenye asili ya Kijerumani, Profesa Karl Marx aliwahi kusema kwamba : " Mfumo wa Kidemokrasia sio mfumo endelevu. Huweza kudumu tu hadi pale viongozi wanapogundua kwamba wanaweza kupora Hazina na wasifanywe lolote na umma. Basi watakapopora Hazina ndio unakuwa mwisho wa demokrasia.'



Hata hivyo, demokrasia anayozungumzia Marx hapa sio ile ambayo wananchi ndio wameshika mpini. Hii ni demokrasia ambayo wananchi wameshika makali na viongozi ndio walioshika mpini.
Anayoizungumzia Marx ni demokrasia ambayo viongozi wachache na chama tawala ndivyo vyenye sauti na uwezo wa kifedha na mwingineo na watumia majaliwa yao hayo kuzuia kuwepo kwa demokrasia ya kweli inayoendeshwa kwa nguvu za wananchi.

Ni demokrasia ambayo haina mashiko ya kikatiba, nguzo zingine za kitaifa haziheshimiwi na zinaburuzwa na serikali, wanasiasa wanawatumia watumishi wa serikali kukidhi matakwa na mahitaji yao na siyo yale ya wananchi na wanaoamua kuwepo au kutokuwepo kwa mabadiliko sio wananchi bali wanasiasa wachache.

Binafsi yangu ili mradi wananchi wenye nchi wana uwezo na nguvu ya kuwawajibisha viongozi wao jambo kama hilo la kufilisiwa kwa hazina haliwezi kutokea na viongozi wasiwajibishwe. Na huu ndio uzuri na ubora wa demokrasia. Humzawadia anayeijenga na kuiimarisha na kumwadhibu anayetaka kuiharibu ikiwa kila kitu kinakwenda sawa na wananchi ndio watawala (kwa tasihili ya kufanya maamuzi ya kuwaondoa au kuwaweka watu wengine madarakani ) na sio chama au kikundi cha watu wachache katika nchi.

Katika demokrasia ya kweli inayosimamiwa na wananchi watu hawamuheshimu wala hawamwogopi mtu au chama fulani eti kwa kuwa kimeshika madaraka.

Mtu na chama chochote kile huheshimiwa na kuthaminiwa kutokana na jitihada zake za kutetea mamlaka ya wananchi dhidi ya watawala wao, uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi na kulindwa kwa maslahi ya walio wengi dhidi ya vitimbi vya watu wa chache katika nchi.

Katika demokrasia ya kweli hakuna kiongozi yeyote au mtumishi yeyote toka ngazi ya chini hadi juu ambaye analindwa anapokiuka misingi ya sheria na katiba ya nchi.

Kiongozi au chama kinachopora au kuwalaghai au kuwatapeli wananchi kwa namna yoyote ile ni adui wa demokrasia na maendeleo ya watu.

Demokrasia haiwezi kukua wala kuendelezwa katika nchi yoyote ile ambayo viongozi, vyama vya kisiasa na taasisi chache zina njia lukuki za kupata fedha kirahisi na viongozi na vyama vingine vingi vinazuiwa, vinatiliwa ngumu au mikwara, vinanyimwa, havipewi au havipati fursa kama hiyo. Wakati mwingine viongozi wengine na vyama vingine vinazuiwa hata fursa za kuendesha shughuli halali za kujiingizia mapato ili kuendesha mambo yao bila kutegemea sehemu nyingine.

Katika nchi nyingi za Kiafrika vyama tawala hutumia nafasi waliyo nayo kuchota fedha toka Hazina na mabenki; wakusanyaji kodi, makadirio hewa yaliyoko kwenye bajeti na kadhalika; kudanganya kwa kalamu katika masuala ya ununuzi wa vifaa ghali vinavyodaiwa kuhitajika kitaifa hata kama ' watu watakula manyasi' au na serikali na kisha kulipwa fedha nyingi zaidi kuliko bei halali ya chombo husika; kutangaza hali ya njaa na kisha kuuza chakula cha njaa na kuweka mfukoni pesa ipatikanayo; kuchota toka Mifuko ya Pensheni, Hifadhi za Jamii, Bima mbalimbali na mashirika mengine ya umma fedha kwa matumizi ya chama cha kisiasa kinyume na sheria za nchi.

Aghalabu panapotokea kisingizio kama kile cha Ugaidi au 'udobi wa fedha' wajanja huitumia fursa hiyo pia kama njia ya kuwapatia viongozi wezi na walafi na chama husika fedha. Hakuna anayejali kama fedha hiyo ni ya jumuiya fulani au mtu fulani na kamwe haikutumwa kwa ajili ya matumizi mabaya. Baadhi ya waumini hapa nchini bado wana majeraha na maumivu ya fedha zao kukamatwa na kishwa kuliwa kwa namna isiyofahamika huku maendeleo yao katika kila nyanja yakibaki nyuma kutokana na kitendo hicho.

Je, haya hutokea kwa sababu chama cha siasa husika kinahitaji sana fedha za matumizi ya kawaida?

Hapana haya yote, aghalabu, hayafanyiki kwa kukidhi fedha za matumizi ya kila siku bali fedha kwa ajili ya kuhonga na kuwarubuni wananchi ili wakipigie tena kura chama husika. Hii ni rushwa tunayoweza kuitwa mama wa Rushwa zote. Ni rushwa hii ndiyo inayokuwa gugu lenye sumu kali na lisiloruhusu kabisa demokrasia kukua, kuota mizizi mirefu na kupanuka kwa mapana na marefu.

Mbio za chama chochote cha siasa zinazoelekea katika kujilimbikizia fedha kutoka vyanzo vyenye mashaka ni mbio za kuzuia na kupiga vita kukua na kuimarika kwa demokrasia katika nchi yoyote ile duniani. Katika baadhi ya nchi vyama vya kisiasa vinavyotawala vimekuwa vikiiba ili kuhonga wanasiasa wa vyama vya upinzani ili kuvivuruga na kukipa nafasi chama tawala kuendelea kubaki madarakani.

Wanasiasa ni wajasiriamali dhaifu

Historia ya nchi nyingi za Kiafrika zinaonesha kuwa wanasiasa wetu wanajua tu maneno au siasa lakini hawajui lolote kuhusu biashara na jinsi ya kuzalisha mali kwa kutumia akili na mtaji wako mwenyewe. Hii ni tofauti na China na Cuba ambako viongozi wa Kikomunisti sio haba wamekusuru kujua siasa wanayoikubali na vilevile kuwa werevu kuhusu biashara na kubwa zaidi kujua namna ya kuwaachia watumishi wa umma kuendesha biashara tulizoshindwa sisi kuendesha kwa kutumia mashirika ya umma kwa namna ambayo nchi hiyo leo inashindana na nchi zilizokuwa zikifuata moja kwa moja siasa za kibepari katika uchumi.

Kwa kuwa viongozi wetu wa siasa hawajui na hawawezi kufanya biashara wamekuwa wakitafuta njia za mkato kwa kufanya biashara za kijanja kwa kuwatumia watu ambao tayari ni wafanyabiashara au walanguzi wa hiki au kile.

Hata hivyo, bado kunabakia tatizo. Kweli mtu anakuwa na biashara kwa kumtumia mtu fulani. Lakini mwanasiasa huyo au mtumishi huyo wa umma anashindwa kufuatilia biashara yake kikamilifu. Matokeo yake anadanganywa na hata wakati mwingine kuzikwa na mwisho wa yote asiambulie lolote.

Rasilimali watu katika nchi nyingi za Kiafrika imeharibiwa na wanasiasa na viongozi wengine kutokana na kujifunza zaidi mabaya na sio mazuri ya wakubwa wao. Hili sio jambo la ajabu. Kama kiongozi wako ni mwizi na mwongo uwezekano wa wewe kuwa kinyume cha hivyo ni mdogo sana. Na ndivyo ilivyo sasa katika nchi nyingi za Kiafrika ambako utakuta kuna piramidi ya wezi toka chini hadi juu. Na wakati mwingine wa chini huiba zaidi kuliko wale wa juu kabisa.

Tofauti na China tumeshindwa kuamini kuwa kwa kufanya kazi ndani ya mashirika ya umma wote tunaweza kuwa na hali bora ya maisha. Na tunapozifanya hizi kama watu binafsi tunaishia kulizwa na walio wajanja zaidi yetu.

Hebu tuvute hatua moja nyuma. Je, hivi kweli inawezekana kila mtu akawa mwanasiasa na wakati huo huo mfanyabiashara?

Jibu ni ndio. Lakini wanaoweza kufanikiwa katika yote mawili ni wachache sana. Na mifano ipo tosha duniani. Wengi wetu tukijaribu hivyo tunaishia kuwa tatizo kwetu wenyewe, kwa watu wetu na nchi yetu.

Kwa hatua ya maendeleo tuliyofikia hivi sasa ninashauri kwamba yeyote anayechaguliwa kama mbunge na kisha kuteuliwa kama waziri aache kusimamia moja kwa moja shughuli zake binafsi za kiuchumi na biashara, na ili kuleta imani kubwa zaidi kwa watu na nchi yao akaacha kabisa shughuli hizo.

Kwa upande wa serikali ni lazima mawaziri wetu walipwe mishahara na mafao mazuri wakati wa kustaafu ili wasiwe na kishawishi cha kutafuta fedha kwa njia nyingine. Yeyote atakayevunja mwiko huu basi tusiwe na subira wala huruma naye.

Kwa namna hii mawaziri watakuwa wakiishi, kufanya kazi, kulala na kuamka wakifikiria tu majukumu yao ya kujenga serikali na nchi bora zaidi kupitia wizara zao na sio kitu kingine.

Siasa, wafanyabiashara na matajiri

Nchi inapokuwa na mawaziri wenye viwanda, mashamba makubwa, biashara kubwa, makampuni ya uwakili au makampuni ya ukaguzi haiwezi kuwa na watumishi safi na bora ambao hawatachanganya shughuli zao na zile za serikali. Itakuwa ni bora zaidi kwa hiyo kuwa na watu wanaompa Kaizari chake na Muumba naye akapewa chake.

Kutokana na hili upo umuhimu wa kuendelea kutenga shughuli za chama na serikali kwa namna ambayo kila mmoja kati yao atakuwa anatumia chake na sio cha mwingine.

Tathmini ya serikali na usimamizi wa fedha

Usimamizi wa masuala ya fedha katika nchi nyingi hapa Afrika hauridhishi. Hali hii haisababishwi na kukosa wahasibu na wataalamu wengine wa mambo ya fedha. La hasha. Hili hutokea kwa sababu wataalamu hao hawaruhusiwi na wemye serikali, wanasiasa na makuwadi wao kufanya kazi kwa kuzingatia utaalamu wao na kanuni na taratibu za kazi zao.
Kama wangeruhusiwa kufanya hivyo basi ni dhahiri lisingelikuwa jambo la kawaida kila serikali mpya inayoingia madarakani kukuta mfuko wa hazina ni mtupu.

Njia mojawapo kwa hiyo ya kukuza na kuimarisha demokrasia Afrika ni kuhakikisha kuwa masuala ya usimamizi wa fedha yanatengwa na kazi za serikali na chama tawala. Aidha wataalamu wa mambo ya fedha ni lazima waachiwe uhuru wa kufanya kazi zao kwa mujibu wa utaalamu na kanuni zao za utendaji kazi.

Tunaweza kuchelewa katika mengine lakini sio katika kuwa na serikali kwa teknohama kwa upande wa uhasibu na fedha. Katika dunia ya leo ni lazima mahesabu ya mapato na matumizi ya serikali yafuatiliwe kila mwisho wa siku. Iwe ni mwiko kwa watumishi wa serikali wanaohusika na mambo ya fedha kuondoka kazini bila kufunga mahesabu ya kila siku kama inavyofanyika katika benki.

Wakuu wa nchi na fedha

Baadhi ya wakuu wa nchi wamekuwa ni wavivu wa kufuatlia masuala ya fedha na kukaimu kazi hizo wakati mwingine kwa wasaidizi wao ambao si wenye uchungu na fedha na maendeleo ya watu na nchi yao na wala pia si waaminifu.

Kwa mfano nyakati zingine makuwadi au walanguzi wanaotumiwa na viongozi hao wamekuwa wakiwaamrisha wasimamizi wa masuala ya fedha na mawaziri wa hazina kufanya mambo ambayo kiongozi mwenyewe wa nchi hana habari nayo licha ya kuyaruhusu au kutoa kibali chake. Na haya mara nyingi yamekuwa yakifanyika kwa kisingizio cha kukipatia chama tawala fedha za kukirejesha tena madarakani.

Aghalabu wengi wamekuwa wakiridhika na ripoti za kupikwa. Ili mradi wao wanapata mishahara na maruputupu yao, wanajengewa nyumba nzuri kila sehemu ya nchi huku wake na watoto wao nao wakinufaika na matunda haramu ya walanguzi hao na wanakuwa hawana ari ya kufuatilia kila shilingi inayoingia na kutoka katika mfuko wa hazina. Matokeo yake meli ya nchi inaweza kuzama huku nahodha kalala na hana habari na kinachoendelea.

Rais asiwe tu Amiri Jeshi bali pia Amiri wa Hazina

Dawa yangu kwa hili sikuzote imekuwa ni kushauri kwamba kama vile Rais wa nchi anavyokuwa ni jemadari wa majeshi yetu basi Rais huyo ni lazima pia awe Jemadari wa masuala ya fedha. Hili likiimanisha kwamba hakuna lolote kuhusu matumizi makubwa ya fedha linaloweza kufanyika bila ruhusa na ridhaa ya kimaandishi ya mkuu wa nchi.

Hii ni akili ya kawaida tu. Maana kati yetu sote hapa hakuna aliyewahi kuona kampuni ambayo Meneja wake mkuu au Mkurugenzi Mkuu au mwenye Kampuni anakubali kuwaachia wasaidizi wake masuala yote yanayohusu mapato na matumizi ya kampuni. Kampuni yenye watu wa aina hiyo ni dhahiri watahitajika kupimwa akili zao.

Umefika wakati wa Waafrika kuzitaka serikali zao kuwa bayana katika kuonesha ni kina nani wanahusika na masuala ya fedha kwa namna ambayo kila hatua inafuatiliwa, kuchunguzwa na kudhibitiwa na hatua nyingine.

Haiwezekani kufuatana na kanuni za uhasibu na ukaguzi, mathalani, kwa mtu mmoja kuwa ndiye huyohuyo anayepokea fedha, anayeandika risiti, anayehifadhi fedha, anayehakikisha fedha iko sawa na anayepeleka na kutoa fedha benki.

Aidha haiwezekani kwa waziri wa fedha au gavana wa benki kutoa fedha eti kwa kuwa Rais ndiye katuma tena kwa maneno bila barua yoyote wala kuzungumza na mkuu huyo kwa simu za mkononi ambazo hata mkulima kijijini anayo leo. Hivi kweli unaweza kuendesha nchi kwa kutuma kwa maneno bila maandishi yoyote au kuandika hilo nyuma ya bahasha chafu kama una nia nzuri na watu na nchi yako ?

Siasa, Serikali na Teknohama

Katika miaka hii ya teknolojia zinarahisisha na kuongeza udhibiti mzuri wa fedha ni muhimu pia kuangalia
ni jinsi gani kwa kuwa na Serikali-T au serikali ya Teknohama kifedha inavyoweza kuanzishwa na kuendelezwa kwa ajili ya kuwa na mtandao hai kati ya Benki Kuu, Wizara, Taasisi Kubwa za Fedha na Ikulu husika.

Demokrasia halisi inakuwepo pale ambapo:
-kuna mfumo unaoruhusu mwingiliano wa watu wote wakati wote;
-viongozi na taasisi za serikali kufikiwa wakati wote;
-hulka ya kisiasa inayokubali mawazo mbadala kushindana wakati wote;
-na wakati huohuo kuruhusu ushiriki wa walio wengi hadi kufikia maamuzi ya mwisho kuhusu malengo ya kuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Demokrasia hutenga wanasiasa a mangimeza

Vilevile, demokrasia hustawi pale ambapo miingiliano ya vionogzi wa serikali na watumishi wa serikali haiwayumbishi kundi la pili kichama au kisiasa na wanakuwa huru kufanya maamuzi yao kwa mujibu wa taaluma zao. Watumishi hawa ni pamoja na wale wa Hazina na Benki Kuu ya nchi.

Miingiliano hii hufanyika katika ngazi mbalimbali kipekee wakati huohuo.
Miingiliano hii hutawaliwa na mazungumzo au mijadala isiyokwisha juu ya fani au nyanja mbalimbali za maisha.

Suala lingine muhimu katika mada hii ni ulazima wa kuwa na sheria na taratibu wazi za uwajibikaji katika michakato ya vyama kujipatia fedha za kuendesha kazi zao za kawaida na zile za kuendesha kampeni za uchaguzi kwa nyakati mbalimbali.

Kama suala hili linakuwa gizani kwa maana kwamba hatujui jinsi vyama vinavyopata fedha zao, kiasi wanachopata na watu au taasisi zinazovipa vyama fedha basi ni rahisi nchi hii kuuzwa bila wananchi wake kujua.

Demokrasia badala ya kuchangia kukua kiuchumi kwa nchi itakuwa inachangia kuingiza nchi katika madeni ya kiajabu ajabu ambayo sio tu yatazuia nchi kupata maendeleo ya kiuchumi na kijamii lakini vile yatakuwa ndio chanzo cha kuua amani, utulivu na mshikamano katika nchi.

© 2009 Sammy W.I.Makilla

Thursday, June 11, 2009

DEMOKRASIA, WANANCHI NA VYOMBO VYA HABARI

Maana ya Vyombo Huru vya Habari
Vyombo huru vya habari ni vyombo vyote vya mawasiliano ya umma na vinginevyo visivyofanya kazi kwa matashi ya mtu au kikundi fulani cha watu na vyenye kujali ukweli na uwazi katika kupasha habari na kuelimisha watu na vilevile kutoa fursa kwa watu hao kutathmini na kuona uhakika na umakini wa habari husika na kisha kufikia maamuzi kutokana na jinsi wao wenyewe walivyoamini ukweli na uwazi ni upi.

Vinatambua kwa yakini kuwa hatari kubwa zaidi ipo katika kuficha ukweli na kuwaachia baadhi ya watu kugeuza urongo kuwa ukweli.

Wanatambua kwa yakini linalohusu wananchi wote wa nchi hii ni kubwa kuliko chama au mtu yeyote. Na wanaamini wajibu wao kwanza ni kwa wananchi na sio chama au mtu fulani.
Hawakubali kurubuniwa na mtu au chama fulani, na siku zote wafanyakazi wake hujitahidi kuwa na elimu na maarifa zaidi kuliko wanasiasa au wanajamii wengine
Vyombo hivyo vinaweza kuwa redio, televisheni, magazeti au tovuti na swahiba zao. Vinaweza kumilikiwa na chama au serikali au watu binafsi. Uhuru hautokani na umilikaji wa chombo bali uhuru watendaji na waandishi wa habari walionao katika kufanya kazi zao kama taaluma zao zinavyotaka bila ya kuyumbishwa na mmilikaji.

Kwa sababu hii chombo cha habari
kinachomilikiwa na serikali au chama tawala hakiwezi kuaminiwa na kuthaminiwa kama hakiripoti ukweli na badala yake kinawasaidia walioko madarakani kuficha ukweli au kudai kuwa urongo ndio ukweli.


Kwa mantiki hii kuna vyombo vya serikali na chama vinavyoweza kuwa huru na vinavoripoti ukweli. Na wakati huo huo kunaweza kuwa na vyombo binafsi ambavyo sio huru na vinavyoficha ukweli au kuwakanganya wasomaji au wasikilizaji au watazamaji wake. Ingawa kwa kawaida hapa Afrika vyombo vingi vinavyomilikiwa na serikali (kwa kisingizio kuwa ni vya umma) au vyama vya kisiasa ni vyombo ambavyo ni vigumu kuwa huru.

Vyombo vya Habari ni uti wa mgongo wa demokrasia. Ndivyo vinavyotoa habari za kisiasa zinazowashawishi watu kuwa wapiga kura walioiva kimaamuzi. Hutufahamisha juu ya matatizo yaliyoko sehemu fulani na kupendekeza jinsi ya kuyashughulikia. Aidha ni walinzi dhidi ya maovu na mabaya yanayoweza kufanywa na wale wenye uwezo au vyeo. Hali kadhalika, vyombo vya habari vinaruhusu au kuwanyima wananchi kuendesha kwa uhuru kamili mijadala mbalimbali na kutoa fursa kwa wote kujifunza juu ya kile kinachohitajika kufanywa au kuzuiliwa kisiendelee au kisitokee. Katika enzi hizi ambazo baadhi ya vyombo vya habari vina nguvu kubwa upo pia uwezekano wa vyombo fulani kuweka ajenda wanayotaka wananchi na serikali kuizungumzia.

Ujio wa Tovuti na Blogi na sera zilizopitwa na wakati

Ujio wa Tovuti na hususan Blogi, vidaka picha kwenye kamera na ujumbe wa matini au maneno mafupi vimetoa chagamoto ya kuwepo kwa waandishi wananchi na vyombo vya habari vya wananchi ambavyo vina uwezo na uhuru mkubwa zaidi wa kuzungumzia hata yale ambayo wanasiasa na serikali wasingelipenda kuyasikia au kuona yanajulikana na watu wengine.

Kwa maneno mengine, kuwepo kwa simu za mkononi sasa hivi kunamuwezesha mwananchi kuwa na chombo binafsi cha habari na pengine anachokiamini zaidi kuliko chombo kingine chochote. Katika hali kama hii itakuwa ni kazi kweli kuwadanganya wananchi wote kwa wakati wote, ingawa, baadhi ya vyombo vitaweza kuwadanganya watu fulani kwa muda fulani. Kwa maneno mengine, kazi ya kusambaza uongo kwa vyombo vya habari na hasa vile vya chama na serikali iliyoko madarakani sasa inafikia ukomo wake.

Ni haki yetu sote kama wananchi kwa hiyo kudai kuwa lazima vyombo vya habari viwe na hulka, maadili na viwango fulani vya kufikiwa wakati wote wa utendaji kazi yao kwa kuzingatia majukumu yalyoorodheshwa hapo juu. Katika demokrasia haya ni matarajio ya msingi na halali kabisa toka kwa wananchi.

Gurevitch and Blumler (1990) wameainisha vizuri ni nini majukumu ya vyombo vya habari katika nchi ya kidemokrasia. Majukumu hayo ni pamoja na: kuangalia na kuzungumzia maendeleo ya kisiasa na kijamii; kuonesha mada moto za wakati uliopo; kuasisi majukwaa ya kuzungumzia masuala mbalimbali kutoka mitazamo na misimamo tofuati; kuwawajibisha viongozi kutokana na jinsi wanavyotumia uwezo, mali na vyeo walivyo navyo; kutoa hamasa, msisitizo, vishawishi kwa wananchi kusoma, kujifunza na kuelewa masuala mbalimbali; kuchagua; na kushiriki katika mchakato mzima wa siasa nchini; kuhimiza na kuchochea ushindani katika kila nyanja ya maisha na kuzuia kwa ukucha na jino hatua zozote zinazodhamiria kuvinyang'anya vyombo vya habari haki ya kuwa huru.

Uhuru wa Vyombo vya Habari na Demokrasia

Demokrasia katika nchi yoyote ile inakuwa pana na ya kina au finyu na ya juu kulingana na upana au kina cha uhuru wa vyombo vya habari katika nchi husika.

Kwa kujua au kutokujua viongozi wanaweza kubomoa au kujenga demokrasia kwa kutumia vizuri au vibaya vyombo vya habari. Pale vyombo vya habari vinapotumika kuwapa sauti wananchi wazungumze wao badala tu ya wao kuwasikiliza kinachosemwa na viongozi wa serikali au wa kisiasa demokrasia hujengwa. Pale vinapotumika kuwa 'laudispika' za viongozi demokrasia husinyaa na kupwaya.

Pale vyombo vya habari vinapokuwa mstari wa mbele kuwafungua watu macho na masikio juu ya udhaifu na makosa mbalimbali ya kiutawala na kiutendaji demokrasia hukua na kupanuka. Vinginevyo, huzuka jamii ya mbumbumbu wasiofikiri wala kufanya mchakato wa hoja na mawazo mbalimbali kabla ya kufanya maamuzi muhimu.

Nchi yetu haina miaka mingi toka kuanza kukubali vyombo huru vya habari. Hata hivyo dalili zilizopo hivi sasa zinaonesha tuna nafasi nzuri ya kuwa na vyombo vya habari vinavyochangia kukua na kupanuka kwa demokrasia kuliko vile vinavyohujumu demokrasia.

Hata hivyo, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali na vyama vya kisiasa au viongozi na wafanyabiashara binafsi havioneshi kuikubali ajenda ya demokrasia. Vingi kati yao vinaelekea kuwa na ajenda za kuhuisha maiti; kuita kilichooza kizima na kuita harufu mbaya harufu ya karafuu na marashi.

Hapa nchini na hata huko nje, inaelezwa kwamba, vyombo vya habari havitekelezi wajibu na majukumu yake kikamilifu. Aidha, baadhi ya vyombo vya habari ama vinatumiwa na wanasiasa au wale wenye kuvimiliki kwa malengo yao binafsi na sio kwa maslahi ya umma.

Katika hali ambayo waandishi wa habari wa vyombo vya umma na vile vya binafsi wanahofia ajira yao kama watakwenda kinyume na matakwa ya wenye vyombo hivyo kwa uhalali au kiutapeli, wao hujikuta ni mateka katika harakati binafsi au za kichama za waajiri wao.

Wachambuzi wa masuala ya vyombo vya habari wanasema kwamba vyombo vya habari ambavyo aidha vinasimamiwa na serikali au kuendeshwa kibiashara na matajiri wachache wa ndani na nje vimekuwa wakati mwingine vyombo vinavyopiga vita demokrasia kwa kujua au kutokujua.

Maudhui katika vyombo vilivyo vingi sio ya kuhabarisha na kuelimisha bali kustarehesha na kupumbaza. Umbeya, kashfa, uzushi, ngono na magomvi ndivyo vinavyopewa kipaumbele zaidi kuliko kitu kingine.

Habari nyingi za kisiasa ni za kushabikia mambo yazuykayo na yapitayo baada ya muda au za kuwahusu watu fulani kiwasifu au kutosheleza kiu yao ya kuonekana au kusikika katika jamii na sio habari zenye fikra mpya, mawazo mbadala, au utundu na ubunifu wa watu hao katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi au kuwaelekeza na kuwaongoza watu katika kutumia fursa za kiuchumi, kisiasa au kijamii zilizopo.

Nchi hazina mijadala muhimu ya kimaendeleo

Kutokana na kutokuwepo na mijadala na midahalo ya maana katika jamii panazuka matangazo ya propaganda yenye kauli mbiu na misemo isiyo na uzito wala maana yoyote katika maisha ya mwananchi. Matokeo yake wapiga kura wanachoshwa na kukatishwa tamaa na hali hii na kuwafanya waone siasa na wanasiasa kama vitu visivyo na maana katika maisha yao. Wengi huacha kabisa kupiga kura wakiwa na hakika kwamba wanajua tayari matokeo yatakuwaje.

Hali iliyofikisha Ulaya hivi leo kushuhudia chini ya asilimia 40 ya wanaostahili kupiga kura ndio tu wakijiandikisha kupiga kura na chini ya hapo kushiriki chaguzi mbalimbali ni somo zuri kwa wanasiasa wetu na waandishi wa habari kuhusu wapi wanaweza kuzifikisha nchi zao kama wakiendelea kama wanavyofanya sasa.

Vyombo vya habari huchangamkia kashfa katika maisha binafsi ya watu na kusahau kabisa kutathmini na kuhakiki sera na mapendekezo ya wanasiasa husika na yale yanayoweza kwa yakini kuleta mabadiliko katika maisha ya kiuchumi na kijamii ya wananchi.

Vyombo vya habari hukurupuka na kufanya ajali au athari ndogondogo kuwa mambo makubwa ya kututisha wakati yale yanayoweza kuwa baa au maafa makubwa yanasahaulika.

Ili kukidhi njaa yao ya fedha za kujiendesha vyombo vingi vya habari vimeamua kufumbia macho hatari za viwanda na bidhaa mbalimbali nchini japo vina hatari kubwa kwa maisha ya wanadamu. Hili ni kwa sababu tu kuwepo kwa vyombo hivyo kwa sasa kunategemea zaidi mapato kutokana na matangazo ya biashara kuliko vyanzo vingine au mauzo mengineyo.

Hata hivyo tunapozungumzia hapa demokrasia na vyombo vya habari hatuwezi kuzungumzia kila kitu.
Tutajikita zaidi katika kuona ni jinsi gani vyombo hivyo vinaweza kukuza na kupanua demokrasia au kuviza na kuifanya demokrasia kusinyaa.

Tathmini fupi ya vyombo mbalimbali

Tathmini ya haraka haraka inaonesha magazeti binafsi kwa hivi sasa yanafanya kazi nzuri zaidi katika kuelimisha watu na kukuza na kuendeleza demokrasia. Hata hivyo, redio na televisheni nyingi bado ziko nyuma katika kazi ya kuchangia kukua na kuendelea kwa demokrasia nchini. Redio na Televisheni zilizopo zinaonekana ama kuwa ubao wa matangazo wa watawala au vyombo vya kuwapumbaza wananchi wasipate muda wa kutafakari, kuchambua na kutoa changamoto za maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.

Awali watu waliamini kuwa kuwepo kwa redio na televisheni nyingi nchini kungeongeza ubora wa vipindi na maudhui ya vipindi. Kinachotokea ni kuwa sasa redio na televisheni nyingi ambazo hazijafikisha hata miaka kumi zimechoka na vipindi vyao ni rojo kuliko pale nchi ilipokuwa na televisheni na redio moja tu.

Katika miaka hii ya mtikisiko wa kiuchumi bila shaka hali itaendelea kuwa mbaya zaidi. Lawama ni kwa wamilikaji wote ambao wameamua aghalabu kuwekeza zaidi kwenye vitu badala ya kuwekeza kwenye watu.

Udhaifu uliopo

Vyombo vya habari vinakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo gharama za uendeshaji na uzalishaji, barabara mbovu, mawasiliano mabovu na ghali, umeme usioaminika, rasilimali watu duni, kodi kubwa, shikinizo za kisiasa na kadhalika.
Haya yote yanachangia katika udhaifu wa vyombo vya habari kuvifikia nchi nzima na kutumuka kikamilifu kama vyombo vya kuchochea mapinduzi ya kidemokrasia hadi vijijini.

Hili linachangia pia kwa vyombo vya habari vilivyopo kutokuwa na uhuru wa kimtaji na kifedha na hivyo kuishia kutumiwa na wachache kwenye jamii wenye ubavu wa kifedha au kisiasa. Katika hali kama hii itakuwa muhali kwa vyombo vya habari kuwa mtetezi wa umma na mpiganiaji uhuru, haki na demokrasia wa kweli kwa niaba ya wananchi.

Changamoto zilizopo

Kutokana na matatizo hayo hapo juu upo umuhimu wa kutoa changamoto la kuhamasisha magazeti ya jamii yakiwemo yale ya vijiji, miji, wilaya, mkoa na kando ili kukabili vizuizi vilivyopo hivi sasa katika vyombo vya habari na hasa magazeti kuwafikia watu kwa wakati na vile vile kuwa na habari zinazowahusu zaidi kuliko habari za maeneo na watu wengine.

Hali kadhalika, ni muhimu kwa wapenda demokrasia ndani na nje ya nchi kuvipa jamala vyombo vya habari ili viondokane na uhitaji na uwezekano wa kutumiwa kutokana na ukata wao.

Mengine ni kuangalia uwezekano wa tovuti kufika vijijini katika lugha ya kiswahili; kutangaza na kuonesha umuhimu wa elimu ya uraia na haki za kikatiba za mwananchi; kutangazia watu kuwa mfumo wa vyama vingi ni bora kuliko mfumo wa chama kimoja au demokrasia ni bora kuliko udikteta.

Hili linaenda pamoja na kuitumia teknolojia ya kisasa kufanya simu za mkononi ziendelee kuwa vyanzo nafuu vya habari za uhakika na kuaminika.

Tunayazungumzia yote haya tukitambua kuwa mawasiliano ni nishati pekee inayotoa nguvu na uwezo kwa jamii yoyote au nchi yoyote kubuni, kufikiria, kutafakari, kuamua na kutekeleza na kisha kutathmini na kuendeleza mambo mbalimbali yanayoifanya jamii au nchi kuwa siku zote katika mwendo wa kimaendeleo badala ya kukwama katika dimbwi la matatizo na kuchanganyikiwa kiuchumi na kijamii.

Hii ina maana demokrasia sio tu inachangia siasa na utawala bora bali pia nchi kuwa mstari wa mbele pia katika uchumi, sayansi, teknolojia, utamaduni, michezo na aina nyingine za maendeleo ya mwanadamu.

Kwa hiyo vyombo vya habari vikichangia maendeleo ya haki za binadamu, uhuru na demokrasia kwa watu wa sehemu fulani vinakuwa pia vinachangia maendeleo makubwa ya nchi na ulimwengu kwa ujumla.


© 2009 Sammy W.I.Makilla

Wednesday, June 10, 2009

DEMOKRASIA NA WAGOMBEA HURU

Mgombea huru ni mtu gani ?

Mgombea huru ni raia yeyote katika nchi fulani anayegombea nafasi yoyote ile ya uongozi bila kuwa mwanachama wa chama fulani.

Katiba kwa kawaida huainisha wajibu na haki za watu kwa misingi ya matamko mbalimbali ya Haki za binadamu na nyinginezo na kisha hutoa haki kwa kila mtu katika misingi ya usawa, ikiwemo ile haki ya kupigiwa na kupiga kura. Baadhi ya nchi hapa Afrika , hata hivyo, zimeamua kuwadhulumu wananchi wao kwa kuwanyima watu wao haki ya kupigiwa kura kwa visingizio vya aina mbalimbali . Ni haki ya wananchi kudai na kuona kwamba wanakuwa na uhuru wa kupigiwa na kupiga kura. Na sio waruhusiwe tu na pengine kulazimishwa kupiga kura lakini wasiwe na haki ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi toka chin hadi juu katika nchi yao.

Uamuzi wa mtu kuwa mgombea huru husababishwa na mambo mbalimbali. Hufanya hivyo, aghalabu, kwa sababu anaamini kwamba viongozi wa vyama walipo ni bomu na hawawezi kufikisha jimbo au mkoa au nchi pale sehemu husika inapostahili. Wakati mwingine hukataa kuwa mwanachama wa chama fulani kwa sababu ya kiwango cha wizi na ufisadi anauona ndani ya chama husika. Aidha, huweza kukataa pia kuwa mgombea wa chama fulani kwa sababu anaamini kwamba vyama vilivyopo havitetei maslahi ya mwananchi bali maslahi binafsi ya viongozi wa vyama hivyo.

Vilevile, huweza kuamua hivyo kutokana na kutambua fika viongozi waliopo wamebeba na hawana uwezo wa kiakili, kifikira na kivitendo wa kuongoza watu na nchi.

Dhuluma kubwa inayofanywa na katiba iliyopo ni ile ya kumpa mtu haki ya kupiga kura [bila kujali ni mwanachama au sio mwanachama wa chama fulani] lakini wakati huo ikamnyima haki ya kupigiwa ila tu mtu anapokuwa ni mwanachama wa chama cha kisiasa kilichosajiliwa.

Ni dhambi isiyo na msamaha kwa mwananchi yoyote kushiriki katika vitendo vya uhuni, ubabe, unyang'anyi wa haki na uhuru wa mtu kupitia katika kuichezea na kuivuruga katiba kwa maslahi ya wachache au chama fulani cha kisiasa. Ndivyo ilivyo pia katika kupora haki ya mgombea huru.

Hadi wa leo hapajaruhusiwa kuwa na mgombea huru, mathalani, nchini Tanzania. Hata hivyo, mtu akiangalia kwa makini atagundua kuwa amri ya kukataa wagombea huru haiungwi mkono na vifungu mbalimbali vya katiba.

Katika sura hii tutajaribu kulionesha hilo huku tukitaraji kuwa wanasheria na wapigania haki na uhuru wa binadamu kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi wataliangalia jambo hili kwa macho mapya na kuondoa dhuluma wanayofanyiwa wale wanaotaka kufikia hatua ya juu katika msonge wa mahitaji ya binadamu kama ilivyoainishwa na Abraham Maslow.

Mitihani kwa wasiokubali vyama vilivyopo

Hali ilivyo hivi sasa ni kwamba mwananchi au mwanasiasa anayetaka kuwa mgombea huru anaiweka nchi au yeye mwenyewe anajikuta katika mitihani ifuatayo:
a) Kama ni mwanachama wa chama fulani anajikuta kifungoni pale anapokuwa kakiona chama ni kichafu na kibovu kiasi cha kutisha;
b) Anajikuta ni mnafiki kwa nafsi yake na anaowawakilisha;
c) Analazimishwa kutekeleza sera na mambo asiyokubaliana nao;
d) Ananyimwa nafasi ya kuchangia ubunifu, mawazo mapya na kutumika kwa fursa za maendeleo au kutatua matatizo ya wananchi kwa njia bora na yenye manufaa kwa wananchi zaidi kuliko inavyofanywa na chama au vyama;
e) Anajikuta hawezi kutumia haki zake nyingi alizopewa kikatiba kama raia;
f) Anajikuta kwamba ingawa yeye ni bora kuliko wengi wengine ananyimwa nafasi ya kuongoza nchi;
g) Inafikia hatua nchi inaongozwa na viongozi dhaifu, wezi na wabovu kutokana na vyama kuwazuia au kuwapiga vita watu walio bora kuliko wao;
h) Kwa kuwa viongozi hao (wanaowazuia wagombea huru) wanajua hakuna wanachokifanya na hawajiamini wanaanza kujiingiza kwenye vitendo vya kuimaliza nchi kiuchumi na kijamii kama bima yao ya baadaye endapo wataondolewa madarakani kwa njia yoyote ile. Njia hizo za kuifukarisha zaidi nchi ni pamoja na kushirikiana na watu wengine kuibia benki kuu na serikali au kuingia mikataba ya kiwizi wizi au kutumia fedha zilizopangwa kwa maendeleo ya wengi kwa maslahi binafsi kwa wachache au ya chama chao.

Kulazimisha uanachama ni kuvunja katiba

Kuwalazimisha watu kuwa wanachama wa chama cha kisiasa ni kosa. Kumnyima mtu haki ya kupigiwa kura eti kwa sababu sio mwanachama wa chama cha kisiasa nalo ni kosa. Na haya yote yanaweza kushuhudiwa na vifungu mbalimbali vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano [1998] hususan Sura ya Kwanza, Sehemu ya Kwanza hadi ya tatu, kama tutakavyoonesha hapa chini.

Kifungu namba 5.-(1) cha katiba ya JMT kiasema "Kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka
kumi na minane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi
unaofaywa Tanzania na wananchi. Na haki hii itatumiwa kwa
kufuata masharti ya ibara ndogo ya (2) pamoja na masharti
mengineyo ya Katiba hii na ya Sheria inayotumika nchini
Tanzania kuhusu mambo ya uchaguzi."

Masharti yaliyomo katika ibara hiyo ya pili hayazungumzii kabisa kwamba raia huyo lazima awe mwanachama wa chama cha kisiasa. Kutaka mgombea kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa lakini sio akiwa mpiga kura ni hitilafu ya kisheria yenye kuonesha uonevu na dhuluma dhidi ya haki ya kikatiba ya raia.

Ingawa kifungu namba 8.-(1) katika katiba hiyo hiyo Sehemu ya pIli kinabainisha kwamba " Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata
misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo -
(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali
itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa
wananchi kwa mujibu wa Katiba hii;
(b) lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;
(c) Serikali itawajibika kwa wananchi;
(d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao
kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii " msimamo wa sasa wa serikali kutokubali mgombea huru unaonesha sio wananchi walio na haki na uhuru wa kuamua bali ni serikali. Ari iliyoko kwenye kifungu hicho haionekani katika maamuzi na vitendo vya serikali inayotakiwa kuisimamia katiba hiyo. Ari hiyo ingelikuwepo kutokana na kifungu hiki tu, serikali isingethubutu kupinga kuwepo kwa mgombea huru.

Watanzania kunyimwa haki ya kugombea uchaguzi kama wagombea huru hakuungwi mkono hata kidogo na kifungu Namba
12.-(1) ambacho kinabainisha wazi kwamba: " Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa."

Na sehemu yake ya
(2) inaendelea: " Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na
kuthaminiwa utu wake."

Hali ilivyo sasa ni kuwa anayetaka kuwa mgombea huru hana haki wala usawa. Na ni pale tu serikali itakapopenda ndio atapata heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.

Pamoja na kuwanyima watu uhuru wa kuwa wagombea huru bado serikali imeendelea kukubali kifungu Namba
15.-(1) kinachotangaza kuwa: " Kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru.

Ambacho kinashadidiwa na kifungu kidogo cha
(2) kinachosema: " Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na
kuishi kwa uhuru, itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote
kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini,
kuhamishwa kwa nguvu au kunyang'anywa uhuru wake ......."

Licha ya kauli hii serikali imeendelea kuwafungia watu kuwa wagombea huru na kuwahamisha kwa nguvu [kutoka kwenye kundi la wanaotaka kuwa wagombea na kuwaweka kwenye kundi la wapiga kura tu] watu na kuwanyang'anya uhuru wao wa kuwa wagombea huru katika chaguzi mbalimbali.

Vifungu vingine kama vile kile cha 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22 na 31 vingelikuwa vinaeleweka vizuri na wanasheria na wabunge waliopo wangeligundua kosa linalofanyika kwa kuwanyima watu kuwa wagombea huru katika uchaguzi.

Mathalani katika kifungu Namba 16 kinazungumza haki ya faragha ambayo inaweza pia kutafsiriwa kama haki ya mtu kuwa peke yake kwa kuwa hataki au hapendi kushirikiana na watu wa aina fulani waliomo katika chama fulani.

Haki ya Uhuru wa mtu kwenda atokako, Uhuru wa Maoni na uhuru wa mawazo kama ilivyo katika kifungu Namba 17 na 18 havionekani kuzingatiwa pia katika msimamo wa serikali wa kuwazuria wagombea huru katika chaguzi mbalimbali.

Kifungu Namba
20.-(1) kinathibitisha kwamba: " Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria
za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani,
kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo
hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au
mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au
kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo."

Kutokana na hayo hapo juu ni dhahiri kuwa serikali inakiuka kifungu hiki kwa sababu haiyumkiniki kwa mtaka kuwa mgombea huru kuwa anaathiri visivyo sheria za nchi. Ila kama kuna amri ya uonevu, kumnyima mtu haki yake na ukandamizaji.

Aidha kifungu kinachozungumzia Uhuru wa kushiriki shughuli za umma
na hususan Haki ya Kufanya Kazi ni kifungu kilicho bayana kikibainisha kwamba kwa muktadha wa kile tunachokizungumza kuwa uamuzi wa kuzuia wagombea huru ni uamuzi wa kumnyima mtu haki ya kushiriki shughuli za umma na kufanya kazi hasa kwa wale ambao wamekwishapita ngazi nne za mwanzo za msonge wa Maslow.

Hofu juu ya wagombea huru

Kufikia hapa tumegundua kuwa kuzuia kwa wagombea huru kikatiba ni kosa.

Swali la kujiuliza ni je, ni kwanini serikali za awamu mbalimbali za CCM zimegwaya kuruhusu wagombea huru.

Ninadiriki kusema kuwa udhaifu na ubovu wa chama hicho na serikali yake ndio sababu kubwa ya kukataliwa kwa wagombea huru.

Vile vile wakati wowote ule ambao chama kinafanya maamuzi ya kiajabu ajabu na yasiyo na maslahi kwa wananchi itakuwa ni rahisi kukiacha chama na mtu kuendelea na ubunge kama mbunge asiye na chama.

Kwa chama hili ni hatari, kwa nchi hili lina faida kubwa kwa kuwa linasafisha vyama na kuwaruhusu wenye uchungu na kiu ya maendeleo ya watu wao kufanya mambo yao bila kukwaza na upofu au uziwi au au umdwebedo au ulegelege au udhaifu wa chama husika.

Wagombea huru wana hatari kubwa ya kuwa kina Slaa au Mwakyembe mara mbili ya hawa waliopo.

Isitoshe kwa wale wenye uwezo wataweza kuleta maendeleo ya haraka zaidi katika majimbo yao kiasi cha vyama vingine kutokuwa na nafasi tena ya kushinda sehemu hizo mpaka mgombea huyo aache au afe.

Wagombea huru wanaweza kuwa chachu kuu ya kufanikisha kuzima kiu ya wakazi wa mikoa mbalimbali nchini kuwa na haki na uhuru wa kusimamia na kuendesha masuala yao ya kiuchumi na kijamii katika ngazi ya mkoa jambo litakaloondosha kumaktaimu kwa mikoa kadhaa inayokwaza na urasimu na umangimeza toka makao makuu ya mptio nchini.

Wagombea huru katika kipindi hiki cha vyama vingi wataweza kutoa changamoto mbalimbali kwa vyama vya kisiasa na serikali kiasi cha kurahisisha mno watu kutofautisha kati ya chuya na mchele safi.

Nimalizie sehemu hii kwa kurudia kusema kwamba katiba kimsingi inaruhusu kuwepo kwa mgombea huru. Lakini kutokana na maslahi ya kichama, kwa bahati mbaya wabunge wa huko siku za nyuma na mahakama wameshawishiwa visivyo kuwakataa bila sababu yoyote ya msingi. Msimamo huu ni mmoja kati ya ile inayochangia kudumaza demokrasia badala ya kukuza na kuimarisha demokrasia hapa Afrika.
© 2009 Sammy W.I.Makilla

© 2009 Sammy W.I.Makilla

Tuesday, June 9, 2009

DEMOKRASIA NA UTAWALA WA KISHERIA

Maana ya Utawala wa Kisheria
UTAWALA wa kisheria kwa muktadha wa sura hii unatafsiriwa kama kufuatwa kwa katiba na sheria za nchi juu ya masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

Katika nchi inayofuata utawala wa kisheria mtu hawezi akapendelewa au kuonewa kutokana na kuwa mwanachama wa chama hiki au kile.

Hii ina maana hata kwa vyama vyenyewe vya kisiasa mwajiriwa wao anaweza asiwe mwanachama ili mradi tu ni Mtanzania. Uanachama wa mtu utatokana na yeye kuamini chama hicho ndicho kinachomfaa na sio kulazimishwa kwa ahadi za kupewa hiki au kile.

Aidha, mfanyakazi wa serikali hana sababu ya kuficha uanachama wake eti kwa kuwa anaogopa atafukuzwa au kutopandishwa cheo eti kwa sababu sio mwanachama wa chama tawala.

Serikali ni umeneja sio usiasa
Kama ilivyo katika dini, kwa maana ya kwamba, serikali haina dini. Ndivyo ilivyo pia kwa serikali na siasa. Serikali haina usiasa. Kwa maana serikali ni ya vyama vyote. Kipindi fulani serikali inaweza ikawa ya Chama B. na miaka mitano baadaye ikawa ya Chama C. na kadhalika. Utawala wa kisheria hapa kwa hiyo ni ile hali inayomlinda mtumishi wa umma dhidi ya uonevu toka chama tawala au vyama vinavyotawala wakati huo.

Katiba na sheria zote za nchi zinaweka wazi maeneo mbalimbali ya mahusiano na maingiliano ya watu na jinsi kila kubaliano, amri, elekezo na ushauri unavyotakiwa kushughulikiwa.

Hata hivyo, katiba, sheria na kanuni nyingine katika nchi sio misahafu isiyobadilishwa. Kutegemeana na watu waliopo na mahitaji yao, mazingira yao, malengo yao na mustakabali wanaoutaka katiba, sheria, taratibu na kanuni mbalimbali huweza kubadilishwa ili kukidhi mahitaji ya watu .

Bila katiba mpya, utawala wa kisheria u mashakani
Nchi inapotoka kwenye mfumo mmoja wa siasa kwenda mfumo mwingine mabadiliko makubwa hutokea. Mabadiliko haya yanaweza kuwa na athari nzuri na athari mbaya. Kazi ya wanasiasa katika nyakati kama hizi ni kurudi tena kwa wananchi na kupata ridhaa ya kuwa na mkataba mpya utakaoamua mahusiano kati ya watawala na watawaliwa yanakuwa vipi.

Chama au serikali inayopuuza umuhimu wa kuwa na katiba mpya baada ya nchi kuondoka kwenye mfumo mmoja wa kiuchumi na kisiasa na kwenda kwenye mfumo mpya wa kiuchumi na kisiasa sio chama au serikali inayojua inakokwenda. Matokeo yake kwa kawaida hayawi ya manufaa kwa nchi na watu wake.

Hatima ya yote kinachotakiwa kitokee hapa ni kuwa raia au mtu yeyote katika nchi husika asiathirike visivyo pale chama kimoja kinapotoka madarakani na chama kingine kuingia madarakani. Na hili huwezekana tu pale ambapo toka mwanzo viongozi wa nchi na wale wa kisiasa wanakuwa kitu kimoja na kukubaliana kwamba utawala wa kisheria ni juu ya yote na wote.

Masharti ya kuwepo kwa utawala wa kisheria
Tunaweza kusema basi kwamba utawala wa kisheria ni taratibu na mienendo yote ya jamii huru ambayo inaruhsu watu kuendelea na maisha yao ya kawaida hata pale serikali inapotoka kwenye mikono ya chama kimoja na kuingia kwenye mikono ya chama kingine.

Ili kufanikisha hayo hapo juu ni lazima haya yatokee:
. Haki ya vyama na wanachama kukutana na kubadilishana mawazo wakati wowote wanapotaka iheshimiwe;
. Haki ya mtu kutojiunga na chama chochote lakini akawa huru kupigiwa au kupiga kura lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama na wanachama kuwasiliana kwa kutumia barua, simu, magazeti, redio, televisheni na tovuti lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama na wanachama kuandamana ili kuunga mkono au kupinga maoni au vitendo fulani lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama na wanachama kusafiri au kwenda sehemu yoyote ya nchi kufikisha ujumbe au mzigo fulani lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama au wanachama kuanzisha biashara zao na biashara hizo kulindwa na sheria kama zinavyolindwa mali za wanachama wa chama tawala lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama mbadala na wanachama wake kuwekeza wenyewe au kwa kushirikiana na wananchi na wanachama wa vyama vingine lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama na wanachama wake kujielimisha, kujifunza, kutaafiti na kujiendeleza ndani na nje ya nchi lazima iheshimiwe;
. Haki ya wanachama kuajiri na kuajiriwa bila upendeleo au ubaguzi lazima iheshimiwe;
. Haki ya wanachama kukopa toka benki ikiwemo benki kuu ni lazima iheshimiwe.

Hakuna demokrasia mfu
Pamoja na yote niliyoyazungumza hapo juu ieleweke kuwa demokrasia sio kitu kilichokufa. Ni kitu hai. Na kwa kuwa ni hai inabidi kila wakati kipate lishe, na lishe hiyo ichakatwe na mambo mapya na bora zaidi kuzaliwa mara kwa mara. Mambo mapya yanayoisaidia jamii kubadilika toka kwenye udhaifu na kwenda kwenye ubora wa hali ya juu.

Ili kukua na kupanuka kwa demokrasia kuwe ni kitu cha uhakika zaidi ni vyema kuwa na tafiti zinaoendelea katika lugha yetu ya asili Kiswahili ili wananchi walio wengi kujifunza na kuelewa masuala kama vile:
-Kwanini wakati mwingine serikali inafuata sheria na wakati mwingine haitaki kufanya i hivyo.


Je, hufanya hivyo kwa maslahi yao [serikali] na hasa pale hasara za kutokufanya hivyo [kufuata sheria] ni kubwa kuliko maslahi binafsi ya watawala.

Je, ni ipi haki ya watawala na watawaliwa. Je, watawala wana haki ya kuonekana na kuchukuliwa kuwa ni mabwana? Na je, ni haki kwa watawala kuwafanya watawaliwa watwana kwa namna moja au nyingine ?


Demokrasia ya kweli haimpi ubwana mtawala
Mfumo uliopo umejengwa kwa namna ambayo kwamba wale wanaotawala hujiona ni mabwana na watawaliwa wao ni watwana wao.

Hapa tunaangalia ushahidi uliopo kwa vitendo na sio kwa maneno na siasa.

Katika miaka hii ya kukuza na kuimarisha demokrasia katika nchi mbalimbali Afrika ni muhimu pia kutafiti na kupata majibu yatakayosaidia kutoa changamoto mpya kwa kiwango cha juu cha haki za binadamu na demokrasia kamilifu.

Ibainike kwamba siku zote kutokana na mvutano mkali kati ya kukuza na kuendeleza demokrasia kwa upande mmoja na upande mwingine kuheshimika kwa utawala wa kisheria nchini.

Mvutano huu unatokea katika hali tatu zinazojitokeza katika jamii na masuala ya kisiasa wakati wote:
1) pale wanasiasa wanapoitumia demokrasia ili kukwepa vizingiti vinavyowekwa na utawala wa kisheria na majaji;
2) pale wanasiasa wanapotumia utawala wa kisheria na uhuru wa majaji ili kuhujumu demokrasia ; na, 3) pale ambapo wanasiasa, wanapojishughulisha sio na kuhujumu demokrasia kama utawala, wanatumia uhuru wa majaji kuwakabili na kuwashinda wapinzani wao.

Haya ni mambo yanayojitokeza sio tu Afrika lakini karibu katika kila nchi yenye demokrasia changa. Kutokana na hili ni dhahiri pia kwamba kupambana na masuala haya panahitajika umoja miongoni mwa wanasiasa wa nchi mbalimbali ili kuyashughulikia kwa pamoja. Itakuwa ni kazi kubwa kwa chama kimoja katika nchi kushughulikia masuala haya. Ni lazima vyama katika nchi kuungana na vyama mbadala pia katika nchi mbalimbali kuwa na aina ya umoja unaosaidia kuondoa vikwazo kwenye barabara ya kuelekea demokrasia kamilifu.

Hakuna kusiasaishwa uhuru wa mahakama, bunge, vyombo vya habari
Ili haya yafanikiwe ni lazima kupambana na kuwashinda wale wote wanaotaka 'kusiasaishwa' (kuingiza siasa katika maamuzi juu ya vyombo visivyostahili kuingiliwa na siasa bali taaluma ) kwa
uhuru wa mahakama, vyombo vya habari, vijana, wanawake, wazee, vyuo vikuu, watumishi wa serikali na taasisi nyingine kama hizo.

Taasisi zote hizi zinatakiwa kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi au imani yao ya kisiasa.

Hii ni kutokana na ule ukweli kwamba taasisi hizi zinaposiasaishwa panakuwa na hatari ya kukiukwa kwa utawala wa kisheria.

Kusiasaishwa hatimaye huzaa makundi hasimu katika jamii. Makundi haya hasimu huweza kuja kutumiwa vibaya pale anapozuka kiongozi mbovu na ili alinde nafasi yake huanza kuwagawa watu katika makundi ya watu wangu na watu wao.

Ili tuiepushe nchi yetu na mambo kama yale yaliyozikumba nchi za Ivory Coast, Zimbabwe, Kenya, Sierra Leone, Somalia, Madagascar na nchi nyingine kama hizo ndani na nje ya Afrika.

Na njia ya kujihami na haya yote ni kuhakikisha kuwa siasa inakuwa ni kazi ya wanasiasa. Aidha, taasisi zisizostahili kujihusisha na siasa moja kwa moja zisisiasaishwe.


© 2009 Sammy W.I.Makilla

Friday, June 5, 2009

DEMOKRASIA NA TUME HURU YA UCHAGUZI

Tafsiri ya Tume Huru ya Uchaguzi

TUME Huru ya Uchaguzi ni kamati yenye nguvu za kisheria inayoundwa na wananchi walio huru na wasioshawishiwa na mahakama, bunnge, serikali au chama chochote cha kisiasa katika utendaji wa kazi zake. Katika demokrasia makini wajumbe wa Tume Huru hutokana na makundi mbalimbali katika jamii bila kujali kwamba wana elimu ya sheria au la. Wanaostahili kuwa wasomi wa sheria sio wajumbe wa Tume bali watumishi wa Tume. Watumishi hawa huwajibika kutoa ushauri wa kisheria katika maamuzi yote yanayofanwa na Tume ili kuhakikisha wakati wote Katiba ya nchi na sheria zake zinazingatiwa na kuheshimiwa.

Tume yoyote ya Uchaguzi inayoundwa na kubarikiwa na Mwenyekiti wa Chama fulani au Rais wa nchi aliyepo na inayotokana aghalabu na watu waliopewa kabla ya hapo nyadhifa za chini na kiongozi huyo huyo haiyumkiniki kuwa huru kwa sababu mbili kuu. Kwanza, watu hao huwa na mtazamo na msimamo uleule wa seriali au chama kilichowateua. Pili hujikuta wana wasiwasi na nafasi zao na ili kuzilinda inabidi wajipendekeze kwa viongozi walioko madarakani, aghalabu huwa ni tatizo kubwa wakati wa kuhesabu na kutangaza kura kwa sababu hutaka kuwasaidia wale waliowalisha fadhili ya kuwa wajumbe wa Tume ya Uchaguzi.

Kufuatia kukubalika kwa mfumo wa Vyama Vingi baadaye zilipitishwa sheria mbalimbali zilizochangia au kukwaza maendeleo ya mfumo wa vyama vingi nchini. Sheria hizo ni pamoja na zile zinazosimamia uanzishwaji, uendelezaji na uboreshaji wa siasa za mfumo wa vyama vingi.

Kwa upande mmoja kanuni za demokrasia zinazokubalika kimataifa zimechangia kuchipuka kwa maendeleo ya mfumo wa vyama vingi hapa nchini. Kwa upande mwingine, sheria zetu zenyewe zilizotungwa chini ya mfumo wa chama kimoja zimekuwa ni kikwazo hapa na pale katika uendelezwaji na uimarishwaji demokrasia nchini.

Kwa kuwa Tume Huru zilizopo zilianzishwa katika mazingira ya Chama kimoja wanaharakati wa demokrasia wanaoona kuna mapungufu kadhaa yanayochangia kudumaa kwa demokrasia nchini.

Tume huru huzaliwa na Katriba mpya sio katiba yqa viraka
Ili tume hizo kuwa na mashiko taibu na halali ya kikatiba na kisheria ilipaswa kwanza kwa serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar pengine na ya Tanganyika kuwa na katiba mpya. Hili halikufanyika.

Katiba mpya inahitajika ili kujenga mazingira ya haki na usawa kati ya vyama vyote vya siasa na wanasiasa. Haiwezekani kwa chama kimoja kuendelea kutumia fursa za upendeleo zilizopo katika katiba mapokeo bila kusababisha misuguano isiyokwisha katika mahusiano ya vyama na jamii kwa ujumla.

Chini ya chama kimoja jengo lilikuwa halina ghorofa. Baada ya kuja kwa mfumo wa vyama vingi sasa jengo linahitajika kuwa na ghorofa mbili kama sio tatu. Je, kweli tutaweza jenga maghorofa haya kwa kutumia msingi au katiba iliyopo?

Chama tawala kwa kwa kung'ang'ania katiba ya zamani ni sawa na kutaka kuwauzia wengine ghorofa lote. Lakini pale wengine wanapokataa sasa inadai itavunja sakafu ya chni na wao washikilie ghorofa zao huko juu kwa juu. Huu ni Uabunuwasi mtupu na jambo lisilokubalika.

Marekebisho katika sheria ya Tume Huru yamekuwa yakifanyika kwa mfumo wa viraka kama vile inavyofanyika kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano iliyopo leo.

Wanaodai hatuhitaji mabadiliko ya Kikatiba hawana hoja za maana zaidi ya kusema kwamba ile iliyopo bado inawafaa Watanzania.

Wanatumia zaidi hoja ya nguvu na sio nguvu ya hoja. Ili mradi chama chao kiko madarakani na katiba iliyopo inawalinda wao zaidi basi wanadhani kwamba hatuhitaji katiba mpya. Ni pale watakapojikuta upande wa pili ndipo watakapotambua tu umuhimu wa kuwepo kwa katiba mpya.

Swali la kujiuliza hapa ni je, katiba iliyotungwa wakati wa mfumo wa Chama Kimoja na katika mfumo wa siasa wa Kijamaa, kweli inaweza kukidhi mahitaji ya mfumo wa Vyama Vingi, Siasa za Ushindani na Soko Huria kwa mapana na marefu yake kikamilifu?

Kwanini Tume Huru ?
Jibu hapa linaweza kupatikana kwa kuangalia masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiteknolojia, kiutamaduni na kiutandawazi yanayolilia kila kukichwa mabadiliko ya msingi ili maeneo haya yaweze kufanya kazi zake barabara.

Ikumbukwe kwamba demokrasia kama mfumo wa siasa unaathiri na unaathiriwa na masuala mbalimbali yanayowahusu au kuwazunguka watu na nchi husika.

Mathalani, kasi ya maendeleo ya kiuchumi, kiteknolojia na kijamii huathiriwa na kuwepo au kutokuwepo demokrasia pana na ya kina. Uwezo wa watu kuchangia maendeleo ya nchi yao kwa njia hii au ile vile huathrika na kuwepo au kutokuwepo kwa demokrasia. Kwa maneno mengine, kuwepo kwa demokrasia kunaruhusu maingiliano na mahusiano mbalimbali katika jamii yanayochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwenye nchi husika. Kutokuwepo kwa demokrasia kunazuia maingiliano na mahusiano haya na hivyo kudumaza nchi kimaendeleo.

Funguo na kofuli la kupanuka au kusinyaa kwa demokrasia kwa kawaida vinashikiliwa na Tume Huru. Kama Tume kweli ni Tume Huru kazi ya kukua na kupanuka kwa demokrasia inakuwa rahisi mno. Kama Tume sio huru kukua kwa demokrasia sio tu kinakuwa kitu cha polepole sana bali pia huweza kabisa kusimama na kusinyaa.

Hali ilivyo hivi sasa ni kuwa Chama Tawala kina haki zaidi katika kuamua Mwenyekiti wa Tume awe nani na wajumbe wa Timu hizo wawe nani.

Sasa hebu fikiria pale ambapo Timu ya Simba inapokuwa na ruhusa ya kumchagua Refa wa mechi kati yao na Yanga. Na wasiishie hapo tu, bali pia Simba wapewe ruhusa ya kuchagua nani wacheze katika timu ya Yanga na marefa wasaidizi na kamishna wa mechi awe nani. Yanga itakwenda uwanjani kweli?

Swali kubwa zaidi hapa ni je, Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi wanatakiwa wamwakilishe nani? Rais aliyeko madarakani? Chama kilichoko madarakani ? Serikali iliyopo ? Wananchi ? Au wafadhili ?

Ukweli ni kuwa wajumbe wa Tume Huru wanatakiwa kutoka kwenye makundi mbalimbali ya wanajamii yasiyofungamana na upande wowote kisiasa.

Makundi haya kwa kuyagawa katika mafungu makubwa kitarafu yanajumuisha wafanyakazi wa umma, wafanyakazi sekta binafsi, wanaojiajiri, wakulima, wafanyabiashara, wafugaji, wawindaji, wavuvi, wanafunzi na wasiosoma.

Ukigawa kijinsia yana wanawake, wanaume, vijana na watoto. Ukiyagawa kiumri kuna watoto, vijana, watu wazima na wazee. Ni muhimu kuyaangalia makundi haya na kuona ni namna gani yanaweza kuchangia uwakilishi katika Tume Huru.

Wawakilishi katika Tume Huru ya Uchaguzi ndio wanaoamua kama makundi hayo yataishi kwa amani na neema au la baada ya kila uchaguzi kufanyika. Na kazi yao hiyo huweza kuharibiwa katika hatua yoyote ile ya mchakato mzima wa uchaguzi mkuu iwe ni katika maandalizi, kuandikisha wapigaji kura, upigwaji kura au kuhesabiwa kwa kura na hatimaye kutangazwa matokeo.

Hili linaonesha uzito wa dhamana waliyo nayo wajumbe na viongozi wa Tume huru. Kutokana na hili panahitajika umakini mkubwa katika kuwachagua wajumbe hao. Na hii haiwezi kuwa kazi ya serikali iliyopo madarakani au chama tawala peke yake. Maana kama kawaida tabia ya mwamba ngoma ni kuvutia ngozi upande wake.

Umuhimu wa wajumbe huru na makini
Kushirikishwa na kuwepo kwa watu makini katika Tume Huru ya Uchaguzi ndio hatua ya mwanzo na ya mwisho katika kujenga demokrasia ya kweli katika nchi.

Kwa mantiki hii ninapendekeza kwamba kabla ya kuwachagua wabunge na Rais pengine tunastahili kuwa na Uchaguzi wa Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Uchaguzi wa Wajumbe wa Tume Huru, hata hivyo, hautafanyika kila baada ya miaka mitano. Wajumbe hao wakishachaguliwa na kukubalika na wananchi wataendelea kuwepo kwenye Tume hadi kufa kwao au kuondolewa mmoja mmoja au wote pindi wananchi wanapoonesha kukosa imani na mmoja wao au Tume nzima.

Kwa mantiki hii, tutakuwa na Wajumebe wa Tume Huru ya Uchaguzi wanaochaguliwa na wananchi kwa upande mmoja na kwa upande mwingine Rais na wabunge wanaochaguliwa na wananchi. Kwa hiyo hakutakuwa na kumwogopa au kumwabudu mwenzie kama ilivyo hivi sasa. Sio lazima wajumbe hao wawe majaji au wanasheria. La muhimu hapa ni utu, uadilifu na uhuru wa mtu. Izingatiwe kuwa majaji na wanasheria wataingia kama wafanyakazi wengine katika sehemu wanaokstahili kuwepo. Nayo sio nyingine bali katika meza za kutoa ushauri wa kisheria kwa wajumbe.

Tume Huru itawajibika kwa wananchi. Wakati wowote wananchi wanapokosa imani nayo uchaguzi mwingine utaitishwa na hivyo kuwatoa wasiofaa na kuwarejesha wa zamanai au kuwaingiza wapya wanaonekana kuwa wanafaa.

Mapungugu mbalimbali kushughulikiwa
Sheria iliyounda Tume Huru ya Uchaguzi imeanisha kazi kadhaa zinazopaswa kufanywa na Tume. Hata hivyo, pana mapungufu kadhaa ambayo bado yanaweza kushughulikiwa na kurekebishwa mara kwa mara ili hatima ya yote baada ya miaka michache kuwe na sheria, kanuni na taratibu ambazo sio rahisi kukoselewa na hivyo kutoa fursa ya kuchipuka sio tu kwa Tume Huru bali kwa taasisi nyingine za kidemokrasia ambazo ni huru kivitendo na endelevu.

Ni lazima pia Tume Huru ya Uchaguzi iwe na Ruiya au Visheni. Katika nchi nyingi za Kiafrika hii itakuwa ni: ' Kuona Nchi inakuwa na demokrasia pana na ya kina hadi Vijijini.

Azma au Misheni inaweza ikawa ni kufanya yale yote yanayosaidia kujenga na kuwepo kwa demokrasia halisi nchini.

Baada ya hapo Tume inaweza ikaweka mikakati, mbinu, kanuni, mipango na taratibu mbalimbali ya kujenga na kuendeleza demokrasia nchini.

Masharti ya Awali ya Uchaguzi huru
Wakati wa Uchaguzi Tume itatakiwa kuhakisha kuwepo:

i. Haki katika upigaji na ufuatiliaji zoezi la kupiga kura
ii. Usawa katika upigaji na ufuatiliaji zoezi la kupiga kura
iii. Uwazi katika upigaji na ufuatiliaji zoezi la kupiga kura
iv. Ukweli katika upigaji na ufuatiliaji zoezi la kupiga kura,
v. Hali isiyo ya vitisho, uonevu, upendeleo au unyanyaswaji katika upigaji na ufuatiliaji zoezi la kupiga kura
vi. Umakini na uwajibikaji katika upigaji na ufuatiliaji zoezi la kupiga kura.

Haya yakiangaliwa kwa makini basi wakati wa Uchaguzi wananchi watakuwa na imani na Tume. Yasipokuwepo ni wachache sana watakaokuwa na imani na Tume na wasimamizi wake. Aghalabu kukosekana kwa hayo hapo juu ndio unaokuwa mwanzo wa kutofautiana, kuhitilafiana na kugombana. Hali ambayohatimaye hufuatiliwa na nchi kutokuwa na amani na mshikamano.

Nikamilishe sura hii kwa kukumbushwa kwamba kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi ambayo imechaguliwa na wananchi wenyewe na isiyoyumbishwa na mtu yeyote au chama chochote cha siasa au serikali au vyombo vya dola ndio mwanzo wa demokrasia kuchipuka na kukua katika nchi zetu za Kiafrika.


Copyright © 2009 S.W.I.Makilla