Saturday, June 13, 2009

DEMOKRASIA, VYAMA NA HAZINA

Marx na Demokrasia.
YULE mkomunisti maarufu duniani mwenye asili ya Kijerumani, Profesa Karl Marx aliwahi kusema kwamba : " Mfumo wa Kidemokrasia sio mfumo endelevu. Huweza kudumu tu hadi pale viongozi wanapogundua kwamba wanaweza kupora Hazina na wasifanywe lolote na umma. Basi watakapopora Hazina ndio unakuwa mwisho wa demokrasia.'



Hata hivyo, demokrasia anayozungumzia Marx hapa sio ile ambayo wananchi ndio wameshika mpini. Hii ni demokrasia ambayo wananchi wameshika makali na viongozi ndio walioshika mpini.
Anayoizungumzia Marx ni demokrasia ambayo viongozi wachache na chama tawala ndivyo vyenye sauti na uwezo wa kifedha na mwingineo na watumia majaliwa yao hayo kuzuia kuwepo kwa demokrasia ya kweli inayoendeshwa kwa nguvu za wananchi.

Ni demokrasia ambayo haina mashiko ya kikatiba, nguzo zingine za kitaifa haziheshimiwi na zinaburuzwa na serikali, wanasiasa wanawatumia watumishi wa serikali kukidhi matakwa na mahitaji yao na siyo yale ya wananchi na wanaoamua kuwepo au kutokuwepo kwa mabadiliko sio wananchi bali wanasiasa wachache.

Binafsi yangu ili mradi wananchi wenye nchi wana uwezo na nguvu ya kuwawajibisha viongozi wao jambo kama hilo la kufilisiwa kwa hazina haliwezi kutokea na viongozi wasiwajibishwe. Na huu ndio uzuri na ubora wa demokrasia. Humzawadia anayeijenga na kuiimarisha na kumwadhibu anayetaka kuiharibu ikiwa kila kitu kinakwenda sawa na wananchi ndio watawala (kwa tasihili ya kufanya maamuzi ya kuwaondoa au kuwaweka watu wengine madarakani ) na sio chama au kikundi cha watu wachache katika nchi.

Katika demokrasia ya kweli inayosimamiwa na wananchi watu hawamuheshimu wala hawamwogopi mtu au chama fulani eti kwa kuwa kimeshika madaraka.

Mtu na chama chochote kile huheshimiwa na kuthaminiwa kutokana na jitihada zake za kutetea mamlaka ya wananchi dhidi ya watawala wao, uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi na kulindwa kwa maslahi ya walio wengi dhidi ya vitimbi vya watu wa chache katika nchi.

Katika demokrasia ya kweli hakuna kiongozi yeyote au mtumishi yeyote toka ngazi ya chini hadi juu ambaye analindwa anapokiuka misingi ya sheria na katiba ya nchi.

Kiongozi au chama kinachopora au kuwalaghai au kuwatapeli wananchi kwa namna yoyote ile ni adui wa demokrasia na maendeleo ya watu.

Demokrasia haiwezi kukua wala kuendelezwa katika nchi yoyote ile ambayo viongozi, vyama vya kisiasa na taasisi chache zina njia lukuki za kupata fedha kirahisi na viongozi na vyama vingine vingi vinazuiwa, vinatiliwa ngumu au mikwara, vinanyimwa, havipewi au havipati fursa kama hiyo. Wakati mwingine viongozi wengine na vyama vingine vinazuiwa hata fursa za kuendesha shughuli halali za kujiingizia mapato ili kuendesha mambo yao bila kutegemea sehemu nyingine.

Katika nchi nyingi za Kiafrika vyama tawala hutumia nafasi waliyo nayo kuchota fedha toka Hazina na mabenki; wakusanyaji kodi, makadirio hewa yaliyoko kwenye bajeti na kadhalika; kudanganya kwa kalamu katika masuala ya ununuzi wa vifaa ghali vinavyodaiwa kuhitajika kitaifa hata kama ' watu watakula manyasi' au na serikali na kisha kulipwa fedha nyingi zaidi kuliko bei halali ya chombo husika; kutangaza hali ya njaa na kisha kuuza chakula cha njaa na kuweka mfukoni pesa ipatikanayo; kuchota toka Mifuko ya Pensheni, Hifadhi za Jamii, Bima mbalimbali na mashirika mengine ya umma fedha kwa matumizi ya chama cha kisiasa kinyume na sheria za nchi.

Aghalabu panapotokea kisingizio kama kile cha Ugaidi au 'udobi wa fedha' wajanja huitumia fursa hiyo pia kama njia ya kuwapatia viongozi wezi na walafi na chama husika fedha. Hakuna anayejali kama fedha hiyo ni ya jumuiya fulani au mtu fulani na kamwe haikutumwa kwa ajili ya matumizi mabaya. Baadhi ya waumini hapa nchini bado wana majeraha na maumivu ya fedha zao kukamatwa na kishwa kuliwa kwa namna isiyofahamika huku maendeleo yao katika kila nyanja yakibaki nyuma kutokana na kitendo hicho.

Je, haya hutokea kwa sababu chama cha siasa husika kinahitaji sana fedha za matumizi ya kawaida?

Hapana haya yote, aghalabu, hayafanyiki kwa kukidhi fedha za matumizi ya kila siku bali fedha kwa ajili ya kuhonga na kuwarubuni wananchi ili wakipigie tena kura chama husika. Hii ni rushwa tunayoweza kuitwa mama wa Rushwa zote. Ni rushwa hii ndiyo inayokuwa gugu lenye sumu kali na lisiloruhusu kabisa demokrasia kukua, kuota mizizi mirefu na kupanuka kwa mapana na marefu.

Mbio za chama chochote cha siasa zinazoelekea katika kujilimbikizia fedha kutoka vyanzo vyenye mashaka ni mbio za kuzuia na kupiga vita kukua na kuimarika kwa demokrasia katika nchi yoyote ile duniani. Katika baadhi ya nchi vyama vya kisiasa vinavyotawala vimekuwa vikiiba ili kuhonga wanasiasa wa vyama vya upinzani ili kuvivuruga na kukipa nafasi chama tawala kuendelea kubaki madarakani.

Wanasiasa ni wajasiriamali dhaifu

Historia ya nchi nyingi za Kiafrika zinaonesha kuwa wanasiasa wetu wanajua tu maneno au siasa lakini hawajui lolote kuhusu biashara na jinsi ya kuzalisha mali kwa kutumia akili na mtaji wako mwenyewe. Hii ni tofauti na China na Cuba ambako viongozi wa Kikomunisti sio haba wamekusuru kujua siasa wanayoikubali na vilevile kuwa werevu kuhusu biashara na kubwa zaidi kujua namna ya kuwaachia watumishi wa umma kuendesha biashara tulizoshindwa sisi kuendesha kwa kutumia mashirika ya umma kwa namna ambayo nchi hiyo leo inashindana na nchi zilizokuwa zikifuata moja kwa moja siasa za kibepari katika uchumi.

Kwa kuwa viongozi wetu wa siasa hawajui na hawawezi kufanya biashara wamekuwa wakitafuta njia za mkato kwa kufanya biashara za kijanja kwa kuwatumia watu ambao tayari ni wafanyabiashara au walanguzi wa hiki au kile.

Hata hivyo, bado kunabakia tatizo. Kweli mtu anakuwa na biashara kwa kumtumia mtu fulani. Lakini mwanasiasa huyo au mtumishi huyo wa umma anashindwa kufuatilia biashara yake kikamilifu. Matokeo yake anadanganywa na hata wakati mwingine kuzikwa na mwisho wa yote asiambulie lolote.

Rasilimali watu katika nchi nyingi za Kiafrika imeharibiwa na wanasiasa na viongozi wengine kutokana na kujifunza zaidi mabaya na sio mazuri ya wakubwa wao. Hili sio jambo la ajabu. Kama kiongozi wako ni mwizi na mwongo uwezekano wa wewe kuwa kinyume cha hivyo ni mdogo sana. Na ndivyo ilivyo sasa katika nchi nyingi za Kiafrika ambako utakuta kuna piramidi ya wezi toka chini hadi juu. Na wakati mwingine wa chini huiba zaidi kuliko wale wa juu kabisa.

Tofauti na China tumeshindwa kuamini kuwa kwa kufanya kazi ndani ya mashirika ya umma wote tunaweza kuwa na hali bora ya maisha. Na tunapozifanya hizi kama watu binafsi tunaishia kulizwa na walio wajanja zaidi yetu.

Hebu tuvute hatua moja nyuma. Je, hivi kweli inawezekana kila mtu akawa mwanasiasa na wakati huo huo mfanyabiashara?

Jibu ni ndio. Lakini wanaoweza kufanikiwa katika yote mawili ni wachache sana. Na mifano ipo tosha duniani. Wengi wetu tukijaribu hivyo tunaishia kuwa tatizo kwetu wenyewe, kwa watu wetu na nchi yetu.

Kwa hatua ya maendeleo tuliyofikia hivi sasa ninashauri kwamba yeyote anayechaguliwa kama mbunge na kisha kuteuliwa kama waziri aache kusimamia moja kwa moja shughuli zake binafsi za kiuchumi na biashara, na ili kuleta imani kubwa zaidi kwa watu na nchi yao akaacha kabisa shughuli hizo.

Kwa upande wa serikali ni lazima mawaziri wetu walipwe mishahara na mafao mazuri wakati wa kustaafu ili wasiwe na kishawishi cha kutafuta fedha kwa njia nyingine. Yeyote atakayevunja mwiko huu basi tusiwe na subira wala huruma naye.

Kwa namna hii mawaziri watakuwa wakiishi, kufanya kazi, kulala na kuamka wakifikiria tu majukumu yao ya kujenga serikali na nchi bora zaidi kupitia wizara zao na sio kitu kingine.

Siasa, wafanyabiashara na matajiri

Nchi inapokuwa na mawaziri wenye viwanda, mashamba makubwa, biashara kubwa, makampuni ya uwakili au makampuni ya ukaguzi haiwezi kuwa na watumishi safi na bora ambao hawatachanganya shughuli zao na zile za serikali. Itakuwa ni bora zaidi kwa hiyo kuwa na watu wanaompa Kaizari chake na Muumba naye akapewa chake.

Kutokana na hili upo umuhimu wa kuendelea kutenga shughuli za chama na serikali kwa namna ambayo kila mmoja kati yao atakuwa anatumia chake na sio cha mwingine.

Tathmini ya serikali na usimamizi wa fedha

Usimamizi wa masuala ya fedha katika nchi nyingi hapa Afrika hauridhishi. Hali hii haisababishwi na kukosa wahasibu na wataalamu wengine wa mambo ya fedha. La hasha. Hili hutokea kwa sababu wataalamu hao hawaruhusiwi na wemye serikali, wanasiasa na makuwadi wao kufanya kazi kwa kuzingatia utaalamu wao na kanuni na taratibu za kazi zao.
Kama wangeruhusiwa kufanya hivyo basi ni dhahiri lisingelikuwa jambo la kawaida kila serikali mpya inayoingia madarakani kukuta mfuko wa hazina ni mtupu.

Njia mojawapo kwa hiyo ya kukuza na kuimarisha demokrasia Afrika ni kuhakikisha kuwa masuala ya usimamizi wa fedha yanatengwa na kazi za serikali na chama tawala. Aidha wataalamu wa mambo ya fedha ni lazima waachiwe uhuru wa kufanya kazi zao kwa mujibu wa utaalamu na kanuni zao za utendaji kazi.

Tunaweza kuchelewa katika mengine lakini sio katika kuwa na serikali kwa teknohama kwa upande wa uhasibu na fedha. Katika dunia ya leo ni lazima mahesabu ya mapato na matumizi ya serikali yafuatiliwe kila mwisho wa siku. Iwe ni mwiko kwa watumishi wa serikali wanaohusika na mambo ya fedha kuondoka kazini bila kufunga mahesabu ya kila siku kama inavyofanyika katika benki.

Wakuu wa nchi na fedha

Baadhi ya wakuu wa nchi wamekuwa ni wavivu wa kufuatlia masuala ya fedha na kukaimu kazi hizo wakati mwingine kwa wasaidizi wao ambao si wenye uchungu na fedha na maendeleo ya watu na nchi yao na wala pia si waaminifu.

Kwa mfano nyakati zingine makuwadi au walanguzi wanaotumiwa na viongozi hao wamekuwa wakiwaamrisha wasimamizi wa masuala ya fedha na mawaziri wa hazina kufanya mambo ambayo kiongozi mwenyewe wa nchi hana habari nayo licha ya kuyaruhusu au kutoa kibali chake. Na haya mara nyingi yamekuwa yakifanyika kwa kisingizio cha kukipatia chama tawala fedha za kukirejesha tena madarakani.

Aghalabu wengi wamekuwa wakiridhika na ripoti za kupikwa. Ili mradi wao wanapata mishahara na maruputupu yao, wanajengewa nyumba nzuri kila sehemu ya nchi huku wake na watoto wao nao wakinufaika na matunda haramu ya walanguzi hao na wanakuwa hawana ari ya kufuatilia kila shilingi inayoingia na kutoka katika mfuko wa hazina. Matokeo yake meli ya nchi inaweza kuzama huku nahodha kalala na hana habari na kinachoendelea.

Rais asiwe tu Amiri Jeshi bali pia Amiri wa Hazina

Dawa yangu kwa hili sikuzote imekuwa ni kushauri kwamba kama vile Rais wa nchi anavyokuwa ni jemadari wa majeshi yetu basi Rais huyo ni lazima pia awe Jemadari wa masuala ya fedha. Hili likiimanisha kwamba hakuna lolote kuhusu matumizi makubwa ya fedha linaloweza kufanyika bila ruhusa na ridhaa ya kimaandishi ya mkuu wa nchi.

Hii ni akili ya kawaida tu. Maana kati yetu sote hapa hakuna aliyewahi kuona kampuni ambayo Meneja wake mkuu au Mkurugenzi Mkuu au mwenye Kampuni anakubali kuwaachia wasaidizi wake masuala yote yanayohusu mapato na matumizi ya kampuni. Kampuni yenye watu wa aina hiyo ni dhahiri watahitajika kupimwa akili zao.

Umefika wakati wa Waafrika kuzitaka serikali zao kuwa bayana katika kuonesha ni kina nani wanahusika na masuala ya fedha kwa namna ambayo kila hatua inafuatiliwa, kuchunguzwa na kudhibitiwa na hatua nyingine.

Haiwezekani kufuatana na kanuni za uhasibu na ukaguzi, mathalani, kwa mtu mmoja kuwa ndiye huyohuyo anayepokea fedha, anayeandika risiti, anayehifadhi fedha, anayehakikisha fedha iko sawa na anayepeleka na kutoa fedha benki.

Aidha haiwezekani kwa waziri wa fedha au gavana wa benki kutoa fedha eti kwa kuwa Rais ndiye katuma tena kwa maneno bila barua yoyote wala kuzungumza na mkuu huyo kwa simu za mkononi ambazo hata mkulima kijijini anayo leo. Hivi kweli unaweza kuendesha nchi kwa kutuma kwa maneno bila maandishi yoyote au kuandika hilo nyuma ya bahasha chafu kama una nia nzuri na watu na nchi yako ?

Siasa, Serikali na Teknohama

Katika miaka hii ya teknolojia zinarahisisha na kuongeza udhibiti mzuri wa fedha ni muhimu pia kuangalia
ni jinsi gani kwa kuwa na Serikali-T au serikali ya Teknohama kifedha inavyoweza kuanzishwa na kuendelezwa kwa ajili ya kuwa na mtandao hai kati ya Benki Kuu, Wizara, Taasisi Kubwa za Fedha na Ikulu husika.

Demokrasia halisi inakuwepo pale ambapo:
-kuna mfumo unaoruhusu mwingiliano wa watu wote wakati wote;
-viongozi na taasisi za serikali kufikiwa wakati wote;
-hulka ya kisiasa inayokubali mawazo mbadala kushindana wakati wote;
-na wakati huohuo kuruhusu ushiriki wa walio wengi hadi kufikia maamuzi ya mwisho kuhusu malengo ya kuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Demokrasia hutenga wanasiasa a mangimeza

Vilevile, demokrasia hustawi pale ambapo miingiliano ya vionogzi wa serikali na watumishi wa serikali haiwayumbishi kundi la pili kichama au kisiasa na wanakuwa huru kufanya maamuzi yao kwa mujibu wa taaluma zao. Watumishi hawa ni pamoja na wale wa Hazina na Benki Kuu ya nchi.

Miingiliano hii hufanyika katika ngazi mbalimbali kipekee wakati huohuo.
Miingiliano hii hutawaliwa na mazungumzo au mijadala isiyokwisha juu ya fani au nyanja mbalimbali za maisha.

Suala lingine muhimu katika mada hii ni ulazima wa kuwa na sheria na taratibu wazi za uwajibikaji katika michakato ya vyama kujipatia fedha za kuendesha kazi zao za kawaida na zile za kuendesha kampeni za uchaguzi kwa nyakati mbalimbali.

Kama suala hili linakuwa gizani kwa maana kwamba hatujui jinsi vyama vinavyopata fedha zao, kiasi wanachopata na watu au taasisi zinazovipa vyama fedha basi ni rahisi nchi hii kuuzwa bila wananchi wake kujua.

Demokrasia badala ya kuchangia kukua kiuchumi kwa nchi itakuwa inachangia kuingiza nchi katika madeni ya kiajabu ajabu ambayo sio tu yatazuia nchi kupata maendeleo ya kiuchumi na kijamii lakini vile yatakuwa ndio chanzo cha kuua amani, utulivu na mshikamano katika nchi.

© 2009 Sammy W.I.Makilla

No comments: