Maana ya Utawala wa Kisheria
UTAWALA wa kisheria kwa muktadha wa sura hii unatafsiriwa kama kufuatwa kwa katiba na sheria za nchi juu ya masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Katika nchi inayofuata utawala wa kisheria mtu hawezi akapendelewa au kuonewa kutokana na kuwa mwanachama wa chama hiki au kile.
Hii ina maana hata kwa vyama vyenyewe vya kisiasa mwajiriwa wao anaweza asiwe mwanachama ili mradi tu ni Mtanzania. Uanachama wa mtu utatokana na yeye kuamini chama hicho ndicho kinachomfaa na sio kulazimishwa kwa ahadi za kupewa hiki au kile.
Aidha, mfanyakazi wa serikali hana sababu ya kuficha uanachama wake eti kwa kuwa anaogopa atafukuzwa au kutopandishwa cheo eti kwa sababu sio mwanachama wa chama tawala.
Serikali ni umeneja sio usiasa
Kama ilivyo katika dini, kwa maana ya kwamba, serikali haina dini. Ndivyo ilivyo pia kwa serikali na siasa. Serikali haina usiasa. Kwa maana serikali ni ya vyama vyote. Kipindi fulani serikali inaweza ikawa ya Chama B. na miaka mitano baadaye ikawa ya Chama C. na kadhalika. Utawala wa kisheria hapa kwa hiyo ni ile hali inayomlinda mtumishi wa umma dhidi ya uonevu toka chama tawala au vyama vinavyotawala wakati huo.
Katiba na sheria zote za nchi zinaweka wazi maeneo mbalimbali ya mahusiano na maingiliano ya watu na jinsi kila kubaliano, amri, elekezo na ushauri unavyotakiwa kushughulikiwa.
Hata hivyo, katiba, sheria na kanuni nyingine katika nchi sio misahafu isiyobadilishwa. Kutegemeana na watu waliopo na mahitaji yao, mazingira yao, malengo yao na mustakabali wanaoutaka katiba, sheria, taratibu na kanuni mbalimbali huweza kubadilishwa ili kukidhi mahitaji ya watu .
Bila katiba mpya, utawala wa kisheria u mashakani
Nchi inapotoka kwenye mfumo mmoja wa siasa kwenda mfumo mwingine mabadiliko makubwa hutokea. Mabadiliko haya yanaweza kuwa na athari nzuri na athari mbaya. Kazi ya wanasiasa katika nyakati kama hizi ni kurudi tena kwa wananchi na kupata ridhaa ya kuwa na mkataba mpya utakaoamua mahusiano kati ya watawala na watawaliwa yanakuwa vipi.
Chama au serikali inayopuuza umuhimu wa kuwa na katiba mpya baada ya nchi kuondoka kwenye mfumo mmoja wa kiuchumi na kisiasa na kwenda kwenye mfumo mpya wa kiuchumi na kisiasa sio chama au serikali inayojua inakokwenda. Matokeo yake kwa kawaida hayawi ya manufaa kwa nchi na watu wake.
Hatima ya yote kinachotakiwa kitokee hapa ni kuwa raia au mtu yeyote katika nchi husika asiathirike visivyo pale chama kimoja kinapotoka madarakani na chama kingine kuingia madarakani. Na hili huwezekana tu pale ambapo toka mwanzo viongozi wa nchi na wale wa kisiasa wanakuwa kitu kimoja na kukubaliana kwamba utawala wa kisheria ni juu ya yote na wote.
Masharti ya kuwepo kwa utawala wa kisheria
Tunaweza kusema basi kwamba utawala wa kisheria ni taratibu na mienendo yote ya jamii huru ambayo inaruhsu watu kuendelea na maisha yao ya kawaida hata pale serikali inapotoka kwenye mikono ya chama kimoja na kuingia kwenye mikono ya chama kingine.
Ili kufanikisha hayo hapo juu ni lazima haya yatokee:
. Haki ya vyama na wanachama kukutana na kubadilishana mawazo wakati wowote wanapotaka iheshimiwe;
. Haki ya mtu kutojiunga na chama chochote lakini akawa huru kupigiwa au kupiga kura lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama na wanachama kuwasiliana kwa kutumia barua, simu, magazeti, redio, televisheni na tovuti lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama na wanachama kuandamana ili kuunga mkono au kupinga maoni au vitendo fulani lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama na wanachama kusafiri au kwenda sehemu yoyote ya nchi kufikisha ujumbe au mzigo fulani lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama au wanachama kuanzisha biashara zao na biashara hizo kulindwa na sheria kama zinavyolindwa mali za wanachama wa chama tawala lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama mbadala na wanachama wake kuwekeza wenyewe au kwa kushirikiana na wananchi na wanachama wa vyama vingine lazima iheshimiwe;
. Haki ya vyama na wanachama wake kujielimisha, kujifunza, kutaafiti na kujiendeleza ndani na nje ya nchi lazima iheshimiwe;
. Haki ya wanachama kuajiri na kuajiriwa bila upendeleo au ubaguzi lazima iheshimiwe;
. Haki ya wanachama kukopa toka benki ikiwemo benki kuu ni lazima iheshimiwe.
Hakuna demokrasia mfu
Pamoja na yote niliyoyazungumza hapo juu ieleweke kuwa demokrasia sio kitu kilichokufa. Ni kitu hai. Na kwa kuwa ni hai inabidi kila wakati kipate lishe, na lishe hiyo ichakatwe na mambo mapya na bora zaidi kuzaliwa mara kwa mara. Mambo mapya yanayoisaidia jamii kubadilika toka kwenye udhaifu na kwenda kwenye ubora wa hali ya juu.
Ili kukua na kupanuka kwa demokrasia kuwe ni kitu cha uhakika zaidi ni vyema kuwa na tafiti zinaoendelea katika lugha yetu ya asili Kiswahili ili wananchi walio wengi kujifunza na kuelewa masuala kama vile:
-Kwanini wakati mwingine serikali inafuata sheria na wakati mwingine haitaki kufanya i hivyo.
Je, hufanya hivyo kwa maslahi yao [serikali] na hasa pale hasara za kutokufanya hivyo [kufuata sheria] ni kubwa kuliko maslahi binafsi ya watawala.
Je, ni ipi haki ya watawala na watawaliwa. Je, watawala wana haki ya kuonekana na kuchukuliwa kuwa ni mabwana? Na je, ni haki kwa watawala kuwafanya watawaliwa watwana kwa namna moja au nyingine ?
Demokrasia ya kweli haimpi ubwana mtawala
Mfumo uliopo umejengwa kwa namna ambayo kwamba wale wanaotawala hujiona ni mabwana na watawaliwa wao ni watwana wao.
Hapa tunaangalia ushahidi uliopo kwa vitendo na sio kwa maneno na siasa.
Katika miaka hii ya kukuza na kuimarisha demokrasia katika nchi mbalimbali Afrika ni muhimu pia kutafiti na kupata majibu yatakayosaidia kutoa changamoto mpya kwa kiwango cha juu cha haki za binadamu na demokrasia kamilifu.
Ibainike kwamba siku zote kutokana na mvutano mkali kati ya kukuza na kuendeleza demokrasia kwa upande mmoja na upande mwingine kuheshimika kwa utawala wa kisheria nchini.
Mvutano huu unatokea katika hali tatu zinazojitokeza katika jamii na masuala ya kisiasa wakati wote:
1) pale wanasiasa wanapoitumia demokrasia ili kukwepa vizingiti vinavyowekwa na utawala wa kisheria na majaji;
2) pale wanasiasa wanapotumia utawala wa kisheria na uhuru wa majaji ili kuhujumu demokrasia ; na, 3) pale ambapo wanasiasa, wanapojishughulisha sio na kuhujumu demokrasia kama utawala, wanatumia uhuru wa majaji kuwakabili na kuwashinda wapinzani wao.
Haya ni mambo yanayojitokeza sio tu Afrika lakini karibu katika kila nchi yenye demokrasia changa. Kutokana na hili ni dhahiri pia kwamba kupambana na masuala haya panahitajika umoja miongoni mwa wanasiasa wa nchi mbalimbali ili kuyashughulikia kwa pamoja. Itakuwa ni kazi kubwa kwa chama kimoja katika nchi kushughulikia masuala haya. Ni lazima vyama katika nchi kuungana na vyama mbadala pia katika nchi mbalimbali kuwa na aina ya umoja unaosaidia kuondoa vikwazo kwenye barabara ya kuelekea demokrasia kamilifu.
Hakuna kusiasaishwa uhuru wa mahakama, bunge, vyombo vya habari
Ili haya yafanikiwe ni lazima kupambana na kuwashinda wale wote wanaotaka 'kusiasaishwa' (kuingiza siasa katika maamuzi juu ya vyombo visivyostahili kuingiliwa na siasa bali taaluma ) kwa
uhuru wa mahakama, vyombo vya habari, vijana, wanawake, wazee, vyuo vikuu, watumishi wa serikali na taasisi nyingine kama hizo.
Taasisi zote hizi zinatakiwa kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi au imani yao ya kisiasa.
Hii ni kutokana na ule ukweli kwamba taasisi hizi zinaposiasaishwa panakuwa na hatari ya kukiukwa kwa utawala wa kisheria.
Kusiasaishwa hatimaye huzaa makundi hasimu katika jamii. Makundi haya hasimu huweza kuja kutumiwa vibaya pale anapozuka kiongozi mbovu na ili alinde nafasi yake huanza kuwagawa watu katika makundi ya watu wangu na watu wao.
Ili tuiepushe nchi yetu na mambo kama yale yaliyozikumba nchi za Ivory Coast, Zimbabwe, Kenya, Sierra Leone, Somalia, Madagascar na nchi nyingine kama hizo ndani na nje ya Afrika.
Na njia ya kujihami na haya yote ni kuhakikisha kuwa siasa inakuwa ni kazi ya wanasiasa. Aidha, taasisi zisizostahili kujihusisha na siasa moja kwa moja zisisiasaishwe.
© 2009 Sammy W.I.Makilla
Tuesday, June 9, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment