Sunday, June 21, 2009

DEMOKRASIA NA VYOMBO VYA DOLA

Maana ya Vyombo vya Dola

Vyombo vya Dola ni vyombo vyote ambavyo huwepo ili kulinda amani ya wote au amani ya wachache kulingana na hali itakavyokuwa ili mradi anayetoa amri ya mwisho kwa vyombo hivyo ndiye mkuu wa nchi. Katika demokrasia halisi vyombo vya dola hutumika kuwalinda wananchi wote na havitumiki kuwalinda wachache au wakubwa fulani tu katika nchi. Katika demokrasia finyu au chipukizi au demokrasia inayoorojeshwa au kuwekwa pembeni kabisa vyombo vya dola hutumika kuwadhibiti wananchi ili watawala wasibughudhiwe katika mabaya au mazuri wanayowafanyia watu wao. Kwa maneno mengine, vyombo vya dola vinaweza kutumika kuimarisha haki, uhuru na demokrasia ya watu au kinyume cha hivyo.


Katika demokrasia ya kweli ni muhali kwa wanajeshi au askari polisi au mgambo au makundi mengine ya kiulinzi yaliyoidhinishwa na bunge kuwaelekezea mtutu wananchi.
Vyombo vya dola havitumiki kuleta fujo na madhara kwa wananchi bali kuepusha mambo hayo, hata kama inabidi, polisi au askari kuteseka au kuumia au hata kufa.

Urithi wa mkoloni uliokubalika

Urithi ambao Mwafrika kiongozi aliukubali kwa mikono miwili ni ule wa vyombo vya dola. Aidha kwa kuhofia udhaifu wao na uwezo wao wa kuwatimizia watu wao mahitaji na matakwa yao viongozi wengi wa Afrika wameendelea kuvitumia vyombo vya dola kwa kazi ileile iliyofanywa wakati wa mkoloni nayo ni ile ya kumdhibiti mwananchi ili aibiwe, anyonywe, adhalilishwe, adhulumiwe na asifurukute kwenda upande wowote anaoweza kujichomoa.

Katika Afrika hili linakuwa rahisi kwa sababu karibu polisi na walinzi wote hulipwa mshahara mdogo sana ambao unawaingiza katika vishawishi vya aina nyingi. Vishawishi hivyo ni pamoja vile vya rushw ya fedha na rushwa za kisiasa na kiuongozi.

Kwa kuwa mkuu wa nchi ndiye anayetoa fadhila kwa fulani kuwa mkuu wa polisi au majeshi na kadhalika msururu wote wa watumishi katika vyombo vya dola huelekeza utii wao sio kwa raia ila kwa rais wa nchi na watu wake maalum au vyombo vyake vingine. Katika hali kama hii walio wengi katika vyombo vya dola kama tulivyoona kule Zimbabwe, Kenya, Liberia, Misri na kadhalika ni rahisi sana kutumiwa kwa maslahai yasiyo ya wananchi.

Kila nchi huwatumia polisi ili kudhibiti uhalifu na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao. Aidha polisi hutumika ili kuhakikisha kuna ustaarabu na utaratibu unaokubalika wakati wa maingiliano ya watu katika shughuli zao mbalimbali za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

Majukumu mengine waliyonayo polisi zaidi ya kupambana na uhalifu ni pamoja na: upatanishi kati ya wagombanao, usalama barabarani na kutoa msaada wakati wa maafa.

Majukumu haya yanatekelezwa kwa viwango tofauti katika nchi mbalimbali kulingana na uchanga au ukomavu wa demokrasia ya nchi.

Polisi kama kiungo muhimu katika demokrasia
Polisi ni kiungo muhimu katika ujenzi wa demokrasia. Ili mradi kiungo hicho kinatimiza yafuatayo:
1. Kufanya kazi kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi na sio kwa kufuata amri au matakwa ya kiongozi mbabe au chama chenye kuendekeza udikteta;
2. Kuingilia kati maisha ya raia pale tu ambapo ni lazima kabisa lakini kwa umakini na uangalifu ili kutosababisha hasara ya maisha au mali; na
3. Wanawajibika kwa wananchi wote na sio kwa kikundi fulani cha watu katika nchi.

Hata hivyo sio kweli kuwa ni polisi tu wanaoweza kuepusha ghasia au fujo ili pawepo na utulivu, mshikamano na amani katika jamii. Yapo mambo kadhaa ambayo kwa pamoja na mchango wa polisi ndio yanayoweza kuihakikishia nchi umoja na amani ya kudumu. Mambo hayo ni pamoja na:
. jamii kuwa na maadili na tabia zinazokubalika katika maingiliano yake,kwa maneno mengine, hili linalazimisha watu kutambua kwa dhahiri na bayana ni nini ni uovu na nini ni wema, nini ni dhuluma na nini ni haki, nini ni ukweli na nini ni uongo;
. shauku ya kila mtu kutaka kuthaminiwa na kuheshimiwa na wanajamii wenzake,
. ushirikiano na kusaidiana kwa wanajamii, na
. haja ya ulinzi na kupambana na mazingira yanayoizunguka jamii.

Polisi ni muhimu kwa sababu wao peke yao kisheria ndio wanaoruhusiwa tu kutumia nguvu na kuwanyima watu uhuru wao.

Uwezo huu wa polisi unaweza kukubalika na watu fulani katika jamii (kwa kuwa polisi wanawalinda au kuwasaidia) lakini ndio huohuo unaoweza kutafsiriwa kwamba ni mabavu na uonevu na kundi linaloamini linanyimwa uhuru au haki zao za kimsingi.

Uwezo huo wa polisi kwa kweli pia unatoa mwanywa wa polisi kufanya kile wanachokitaka hata ikiwa ni kinyume cha sheria.

Utekelezaji wa kazi za upolisi katika jamii yoyote ya kidemokrasia huhitaji mizania linganifu wakati wote. Maana ukweli ni kuwa polisi wanaweza wakawa ama msaada mkubwa au hatari kubwa kwa demokrasia ya nchi fulani.

Uwezo wa polisi kutumia nguvu, kutoa adhabu za papo kwa hapo, kufuatilia na kuwapeleleza watu kwa siri hivi hivi au kwa kutumia teknolojia, kuwasimamisha, kuwasachi na kuwakamata watu kunaweza kutumika kusaidia udikteta ulioko madarakani kirahisi tu.

Polisi ni neno linalotokana na neno 'polity' ambalo huko Ulaya miaka 500 iliyopita lilitumiwa kuonesha aina ya serikali inayosimamiwa na chombo cha kisiasa. Chombo hicho kilihusishwa zaidi na maisha, afya na mali za watu. Nchi hazikuwa na polisi tunaowajua leo. Waliofanya kazi hizo walikuwa ni askari au watu maalum wa kuteuliwa na viongozi.
Katika karne ya 18 polisi wakawa wanajihusisha zaidi na masuala ya ndani na usalama wa watu.

Polepole, polisi ikageuka na kukengeuka baada ya dhana ya nchi huru zanye mipaka kuibuka kuwa taasisi ya kulinda mipaka ya nchi, usalama wa ndani na kudhibiti kisheria maingiliano ya watu katika maisha yao ya kila siku.

Nchi zinahitaji polisi wa kidemokrasia sio kikoloni

Hivi leo tunazungumzia jinsi ya kuwa na jeshi la polisi linaloendana na kanuni za kidemokrasia. Polisi wa kidemokrasia wana sifa zipi? Ni rahisi kwa kweli kueleza au kufafanua polisi wasio na mwelekeo wa kidemokrasia wakoje. Hii ni kwa sababu ni wale wote wanaovunja karibu kila msingi na kanuni ya demokrasia. Hata hivyo, tutajitahidi kuelezea kwa kifupi hapa ni namna gani polisi wa kidemokrasia wanatakiwa kuwa.

Polisi wa kidemokrasia kwa kawaida huwa na sifa hizi: hufanya kazi kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi na sio kwa matakwa ya mkuu wa nchi au wanasiasa. Polisi hutumiwa nguvu na uwezo wao kwa umakini, uangalifu na kwa kuwajali sana wananchi. Mahalani, Uingereza, kwa ridhaa ya wananchi, hairuhusu polisi wake kutembea na silaha. Watu hutii polisi kwa kuwaheshimu kutokana na jukumu lao kijamii na sio kwa kutishwa.

Kazi za polisi wa kidemokrasia hujulikana kutokana na jinsi wanavyofanya kazi zao na namna wanavyofikia malengo yao. Mambo kama utesaji, kuua watuhumiwa papo kwa hapo, kuteka watu nyara au kuwakamata na kuwajeruhi watoto, ndugu au jamaa wa mtuhimiwa huwa hayakubaliki na hukatazwa kisheria.

Masuala kama kutumia nguvu au kumnyima mtu uhuru wake au kuwahoji watuhumiwa hufanyika kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na kwa ruhusa kutoka kiongozi au mamlaka husika.

Kwa ufupi polisi huwa na haki tu ya kumkamata mtuhumiwa lakini hawana haki ya kuchukua sheria mkononi mwao. Jambo ambalo sasa mara kwa mara linaonekana la kawaida katika jamii yetu.

Ni wajibu wa polisi wa kidemokrasia kuhakikisha sikuzote kuwa mtawala na mtawaliwa, tajiri na masikini, mnyonge na mwenye nguvu hakuna anayekuwa juu ya katiba na sheria za nchi.

Sio lazima polisi wa demokrasia nchini mwetu wafanane na wale wa nchi nyingine. Lakini ni lazima kwa polisi kuhakikisha kuwa wanawajibika kwa walipa kodi na sio kwa watawala au wale ambao kuwepo kwao kama wao kunategemea kodi anayolpa mwananchi. Baada ya hapa mengine yanakuwa ni rahisi.


Kukua na kukomaa kwa demokrasia kunategemea sana jinsi jeshi la polisi linavyolelewa katika nchi husika.

Vyama tawala visihodhi polisi

Viongozi wa chama tawala katika nchi husika wanaweza wakalilea jeshi la polisi kama vile ni jeshi la kulinda chama tawala na viongozi wake. Au wanaweza wakalilea jeshi hilo kama lenye kuwajibika kwa wananchi wote bila kujali wanatokea chama gani.

Dhuluma, uonevu, wizi na ubabe katika siasa, aghalabu, hutokea pale ambapo jeshi la polisi linalelewa kwa namna ile ya kwanza.

Hili huzaa hali ya polisi kuona kwamba chama tawala, viongozi na wanachama wake kwamba wao sikuzote ndio wenye haki, wenye kusema ukweli na walio safi kuliko wanajamii wengine na makundi au vyama vyao vya kisiasa na visivyo vya kisiasa. Tatizo linakuja pale ambapo chama husika kinakuwa ndio mwizi au jambazi na wengine ndio wanaoibiwa au kudhulumiwa. Polisi wa nchi atasimama wapi ?

Katika hali kama hii wananchi wasiokiunga chama tawala mkono na hususan wanachma na viongozi wa vyama mbadala huonekna sikuzote ni wakorofi, wabishi na wavunja sheria.

Uhusiano wa polisi na chama tawala kwa hiyo huwa ni wawenzetu na ule wa jeshi hilo na wasio wanachama wa chama tawala huwa ni uhusiano na wahalifu au wahalifu watarajiwa.

Haya yote yanaonesha upo umuhimu wa kurejea vipengele katika katiba ya nchi (na kama tutakuwa na katiba mpya ni vyema zaidi) ili kuweka uhusiano wa polisi na viongozi kwa upnade mmoja na polisi na wananchi kwa upande mwingine bayana. Katika marejeo hayo izingatiwe kuwa ni kosa kwa polisi kutumiwa na chama chohcote cha kisiasa, kikiwemo, pia chama tawala. Na endapo hili linakiukwa basi wananchi wawe na haki ya kulishtaki jeshi hilo kwa kuvunja katiba na sheria za nchi.

Nani kumteua polisi mkuu

Jeshi la polisi, hata hvyo, haliwezi kubadilika kama wakuu wa polisi wataendelea kuchaguliwa na rais na sio bunge au Jaji mkuu kama jaji huyo ndiye anayechaguliwa na bunge. Uoga wa makamanda wengi kuwa wanaweza wakatemwa na chama tawala kama wasipokipendelea chama hicho na kuvionea vyama mbadala utatoweka mara moja kama kamanda huyo atakuwa hawezi kufukuzwa kazi na rais au waziri mkuu au kiongozi mwingine wa serikali.

Katika miaka hii ambayo tunazungumzia pia kuwa na wizara chache na wizara zilizo nyingi kugeuzwa kuwa ni wakala, kamisheni, tume au taasisi maalum ni muhimu pia kuangalia ni jinsi gani jeshi hilo linaweza kugeuzwa kuwa la kukuza na kupanua demokrasia zaidi na sio jeshi la kukwaza na kuidhofisha.

Hili litahitaji jeshi letu kutokuendelea kuwa la kupokea amri za kikoloni, kibabe na kidhulumati na kutumia mabavu badala ya busara na hekima ili kujenga udugu na mshikamano muafaka katika jamii husika. Jambo ambalo husaidia wananchi kujipolisi wao wenyewe.

Aidha, hili litasaidia kuzika tabia iliyozika ya baadhi ya vyama vya siasa Afrika kujijenga kwa kuruhusu baadhi ya wanajamii kuvunja sheria za nchi na kuwalinda.

Masharti ya matumizi bora ya polisi

Ili haya yote yafanikiwe ni muhimu mambo kadhaa kufanyika:

Kwanza, lazima pawe na jitihada zinazoonekana kufanyika na kuendelezwa wakati wote na kuzuia polisi kutumiwa na chama cha kisiasa hata kama kikiwa ni chama tawala wakati huo. Katika misingi ya utawala wa kisheria hakuna chama kinachostahili kuwa juu ya sheria katika demokrasia. Vyote lazima viwe chini ya sheria. Kazi nyeti zaidi itakuwa ni kwa jeshi hilo kujua namna ya kutenga kati ya mambo ya serikali na yale ya chama au vyama tawala vya wakati huo. Na pasiwe na raia yeyote anayeweza kuonewa au kunyanyaswa kwa kuwa amefuata sheria za nchi nukta baada ya nukta.

Polisi nao wanapaswa kuwa chini ya sheria- ikiwa ni sehemu muhimu ya uwajibikaji katika mfumo wa vyama vingi. Hili lisipofanyika ni rahisi kutoa mwanya kwa watu wezi, wauaji, wauza madawa na kama hao kujipenyeza ndani ya jeshi hilo na kuunda dola ndani ya dola au serikali ndani ya serikali. Angalia kinachofanyika sasa Algeria, Arbezeijan, Kenya, Kongo, Burundi, Ethiopia, Misri, Moldovia, Burma, Mexico, Colombia na Zimbabwe.

Kurejesha imani ya wananchi kwa jeshi la polisi kama ilivyokuwa katika siku za mwanzo za uhuru itatupasa tuyasuke upya majeshi yetu ya polisi. Polisi na wananchi laizma wawe ni pande mbili zinazotegemeana kwa faid aya jamhuri nzima. Pasiwe na upand unaougeuza upande mwingine kuwa ni buzi la kuchuna mchana kweupe!

Ili uhuru, usawa na haki viimarike katika nchi ni muhimu sana kwa jeshi la polisi kuonekana kama ni walinda haki na watu sio tu wanaokubalika bali wanaothaminiwa sana na jamii. Mfumo unaowafanya wananchi walione jeshi la polisi kama ni jeshi la watu wabaya na wasioaminika haliwezi kujenga jamii bora na nchi inayoheshimika. Na mara nyingi hali hutokea pale jeshi hilo linapogeuzwa kuwa ni jeshi la 'wanyama wakali' waliokusanywa kumlinda mmiliki wao hata kama mmiliki huyo akiwa jambazi.

Ndio kusema kwamba jeshi la polisi linastahili kurudishwa chuoni. Huko watajifunza kuwa demokrasia sio tu jambo zuri kwa nchi bali kwao pia na kwa wananchi wenzao.

Itapaswa wajue kwamba raia ni dada, kaka, baba, mama, bibi na babu zao. Na chochote wanachokifanya kiwe kizuri au kibaya hakiwezi kutoka nje ya mduara ambao wote tunacheza humo.

Wito wa polisi katika nchi inayotaka kujenga demokrasia inayofanya kazi kikwelikweli ni lazima uwe -'usalama na ulinzi kwa wote bila kubagua.'

Kukua na kuimarika demokrasia na polisi
Zipo njia mbalimbali ambazo nchi inaweza ikatumia ili kukuza na kupanua demokrasia. Njia hizo ni pamoja kwa haraka haraka na masuala kama:

. Kutenganisha kazi zao na masuala ya kisiasa.
. Kutokubali kuingizwa katika hali au mitego inayoweza kusababisha wao kuwa ndio waanzishaji fujo mahala fulani. Hii ni pamoja na kukataa kuingia kwenye maeneo ya shule na vyuo. Tabia iliyozuka siku za karibuni kuruhusu mkuu wa shule kuwaita polisi au wanajeshi kuvamia vyuo sio uamuzi wa busara wala hekima. Kila shule au chuo kinastahili kuwa na walinzi wake wanaotenda haki kwa wote bila kujali nafasi au cheo cha mtu katika taasisi husika;
. Kurahisisha na sio kuzuia kufanyika kwa mikutano na maandamano ya wananchi. Ni kosa la katiba na kisheria kuwazuia wananchi popote pale nchini kufanya mikutano au maandamano;
. Kuhakikisha kuna mwingiliano kati ya mapolisi na raia kupitia mambo mbalimbali kama vile michezo, starehe, uwekezaji na shughuli za maendeleo ya kijamii.
. Kusaidia makundi ya kijamii ikiwemo vyama vya kisiasa kuendesha mambo yao katika hali ya utulivu na usalama.
. Kutokubali kuwepo kwa wezi, makuwadi, vibaka, dhulumati, wala rushwa, walevi, wazinzi, matapeli na wababishaji katika jeshi hilo.

Ikiwa hayo hapo juu yatafnyika bila shaka kutakuwa na uhusiano mzuri kati ya polisi na jamii. Uhusiano mzuri kati ya polisi na jamii huchangia kwa kiasi kikubwa kuchanua na kustawi kwa demokrasia na shughuli zote zinazoendana na ujenzi wake.

Aidha Polisi wanastahili pia kufanya kazi kwa ushirikiano na ukaribu zaidi na mahakama, bunge na viongozi wa kijamii ili kukuza na kupanua demokrasia wakati wote.


Polisi ni watumishi sio mabwana
Aidha serikali na wakuu wa polisi wakati mwingine hujisahau na kudhani kuwa wao ni mabwana na wananchi ni watwana. Katika demokrasia inayofanya kazi sawasawa yeyote anayejisahau kwamba ni mtumishi wa wananchi anapaswa kuondolewa mara moja na nafasi yake kuchukuliwa na yule anayetambua ukweli huu kuwa watumishi wa serikali wakiwmo polisi ni watumishi wa wananchi na sio mabwana wao. Hili la polisi kuwa watumishi na sio mabwana ni jambo muhimu sana. Ni pale ambapo aghalabu polisi wamepewa vichwa na viongozi kisha wakajiona wao ndio mabwana kwa sababu wana silaha na nguvu za dola ndipo ambapo nchi zimechafuka na kutokea uvunjaji haki wa kutisha na hata mauaji ya kimbari. Tuliepuke hili kwa kuwakumbusha polisi wetu sikuzote kuwa wao ni watumishi wa watu na sio mabwana.


© 2009 Sammy W.I.Makilla

No comments: