Saturday, June 27, 2009

DEMOKRASIA, UNDUGU NA UBAGUZI MPYA

Maana ya Undugu na Ubaguzi Mpya

Maana ya Undugu kwa muktadha huu ni pale mwanasiasa anapotumia nafasi aliyo nayo [akijua wake au chake haviwezi kukataliwa na wajumbe au wabunge-maana yeye ndiye anayewahakikishia kuwepo kwao na maslahi wanayopata, na kwa nafasi hiyo yeye kashika mpini na wanachama na wananchi kwa ujumla wameshika makali. ] kuwapa nafasi za kazi katika chama au serikali ndugu, watoto, wake, jamaa au marafiki zake. Undugu unapokithiri unamloga kiongozi kiasi cha kumfanya atake pia awe na sifa za kifalme falme, ikiwemo pia kurithisha uongozi kwa mwanae au yule amtakaye yeye na siyo yule wanayemtaka wanachama au wananchi. Na akiona anayemtaka hatakiwi anaweza akafanya yote yale ya kuwazaini na kuwatisha watu wake mpaka wakubali kumkubalia matakwa yake. Ingawa imekwishatokea pale watendaji wa chini wanapogundulika na viongozi wa juu kumpandikiza asiyetakikana kwa huyo aliyepandikizwa kuombwa kumuachia yule anayekubalika.

Wakati maana ya Ubaguzi wa aina mpya katika nchi nyingi za Kiafrika, Kiarabu na Kiasia
ni kuachiwa kuzuka kwa ubaguzi kati ya wananchi walio wanachama wa chama tawala na wale wasio wanachama wake. Hawa wanaweza kuwa wanachama wa vyama vingine vya kisiasa au wananchi ambao hawaoni umuhimu wa kuwa wanachama wa chama chochote cha kisiasa kwa kuwa wao malengo yao makubwa ni ya kiuchumi na kijamii na siasa kwao ni kikwazo na sio msaada au tajamali.

Kwa kuwa chama tawala ndicho kinachoshika serikali basi kinachotokea ni kuwa wanachama wake hupewa vyeo vyote katika nchi hata kama uwezo wao katika hilo ni mdogo au hawana uwezo kabisa. Inakuwa nadra sana kwa asiye mwanachama wa chama tawala kupewa nafasi yoyote ya maana katika kuchangia maendeleo ya nchi na watu wake. Huu ndio ubaguzi mpya. Na kadri demokrasia inavyokuwa dhaifu katika nchi ndivyo ubaguzi huo unavyoshamiri katika nchi ambayo badala ya kwenda mbele kidemokrasia na kimaendeleo huwa inarudi kinyume nyume.

Afrika ilipinga vikali kuwepo kwa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini. Hii leo nchi zenye tabia za kufanya baadhi ya watu wao watumwa zinatazamwa kwa jicho la hasira. Katika nchi mbalimbali za Kiafrika ubaguzi wa kijinsia uko mashakani. Wanawake sasa sio tu wanasemwa ni huru lakini wanaonekana kuwa huru kuliko huko nyuma. Wasiojiweza na walemavu nao hawakuachwa nyuma. Wote wanajua sasa kwamba wana haki sawa na raia au watu wengine nchini mwao. Haya yote yanaonesha kuwa Waafrika kwa asili yao hawakubali na hawapendi ubaguzi.

La ajabu ni kuwa ujio wa siasa za mfumo wa vyama vingi umekuja na aina mpya ya ubaguzi au 'apartheid' ya kisiasa kama sio ki-chama.

Watu wengi bado hawajaujua kwa undani ubaguzi huu unavyokwenda. Katika makala haya tutajaribu kuonesha jinsi ubaguzi huu ulivyo na unavyoendeshwa.

Ubaguzi wa kichama au kisiasa Afrika unajionesha kwa sura au njia mbalimbali. Kubwa kati ya hizo ni ule ubaguzi unaofanyika katika masuala ya nafasi za kazi,
mikopo na masuala ya fedha,misaada, ujenzi wa miundo-mbinu, elimu. afya, uongozi na fursa nyingine za kiuchumi na kijamii.

Aidha ubaguzi huo upo pia katika kuchagua wafanyakazi kwa ajili ya nafasi za ukatibu mkuu, balozi za nchi za nje, wakuu wa mikoa na wilaya, wakuu wa mashirika, wakuu wa tume au kamisheni mbalimbali, wakuu wa polisi, wakuu wa vyuo, wakuu wa mahospitali, wakuu wa mabenki au taasisi za fedha za umma na wakuu wa serikali za mitaa.

Vilevile kuna ubaguzi pia katika nafasi za masomo ya nje na uteuzi wa wajumbe wa bodi na tume mbalimbali nchini na wakuu wa vyombo vya habari vya serikali/umma.

Kwa upande mwingine wazee, wazazi, vijana
na wanawake aghalabu wa chama tawala huonekana kupendelewa na kupewa haki, fursa na neema zaidi kuliko wale wasio wanachama.

Katika utendaji kazi za serikali aghalabu utakuta mambo yanakuwa ni rahisi na nafuu zaidi kwa wale walio wanachama wa chama tawala kuliko kwa wale wasio wanachama wa chama hicho. Na hata pale serikali inapponesha kuvumiliwa mfumo wa vyama vingi, wapinzani hulazimika kujificha kwa sababu moja au nyingine.

Sio kwamba chama husika hakijui inachokifanya. Inajua vizuri sana. Hufanya hivyo ili kuhakikisha kuwa kinaendelea kujenga mapenzi kati yake na makundi hayo ili uchaguzi unapofika iwe ni rahisi chama hicho kuchaguliwa kuliko chama kingine.


Kwa kufanya hivyo chama tawala hujenga ukuta kati ya wanachama wake na wanachama wa vyama vingine.

Hili linakuwa ni rahsi kufanyika kwa sababu katika Afrika mpaka kati ya serikali na chama tawala huonekana kwa shida sana. Kwa nchi nyingi mpaka huo ni kitu kisichokuwepo.

Kwa kuwa Gavana wa Benki anakuwa ni mtu wao inakuwa ni rahisi kumuamuru kuiba fedha hazina na kuwapa makuwadi na walanguzi wa chama ambao aghalabu huwa hawazifikishi zote. Ni asilimia ndogo tu hatimaye inayotiririkia kwenye kibakuli cha chama husika.

Kwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kodi ya Nchi fulani ni mtu wao inakuwa ni rahisi kiongozi wa chama kuamrisha mtu au kampuni fulani idaiwe kodi isipostahili au kodi kubwa kwa lengo la kumkomoa tu mtu huyo au kampuni hiyo kwa kutumia mabavu ya kisiasa.

Katika nchi nyingi kuna wazawa wengi tu wanaoweza kuwekeza katika nchi zao pengine uwekezaji wao ukashinda hata ule wa nje. Lakini kwa sababu ya vitendo vya uonevu na dhuluma wanayofanyiwa na chama tawala huamua kutofanya chochote na kuziweka tu fedha zao au kutanua kwani wanaona ni ujinga mtu kuingizwa matatani kwa sababu ya fedha zake mwenyewe.

Ubaguzi upo kila mahala, lakini kwa sababu za nafasi tuoneshe tu mifano michache ambayo yeyote yule anaweza kuipanua ikafikia kote kule anakotaka.

Katika nafasi za kazi kwa mfano kwa ajili ya mashirika ya umma, balozi za nje na mashirika ya kimaeneo na kimataifa ni dhahiri kuwa wanachama wa chama tawala ndio wanaochaguliwa zaidi sikuzote na hutokea kwa bahati mbaya tu akachaguliwa mtu ambaye sio kada wa chama tawala.

Matokeo ya hili ni kwamba mara nyingi unakuta watu wasiokuwa na uwezo wanapewa kazi au nafasi ambazo hawaziwezi na mwisho kuishia kuharibu kazi na kuziangusha taasisi wanazotakiwa kuziendesha. Hivi leo vipaji na uwezo wa Waafrika walio wengi wakiwemo Watanzania vimezikwa au vinafichwa na havitambuliki kutokana na ubaguzi wa kichama unaoendelea.

Katika nafasi za masomo ingia katika Wizara yoyote ya Elimu katika nchi mbalimbali za Afrika ufanye utafiti na utagundua watu wanaopewa nafasi nzuri za masomo ya juu ni watoto wa wanasiasa au makatibu wakuu wa wizara husika na watu kama hao na watumishi katika wizara hizo.

Katika nchi za Kiafrika vyama tawala vilitumia nafasi ile kabla ya kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi kupora majumba, viwanja vya michezo, viwanja na rasilimali zingine na kuzifanya ni zao. Apartheid ya kisiasa katika baadhi ya nchi imekuzwa sana pale chama tawala kilivyopora au kunyakua kinachostahili kuwa cha wote, baadhi ya vitu vilivyoporwa ni pamoja na:
-redio,
-magazeti,
-televisheni,
-viwanja vya michezo
-kumbi za mikutano au jamii
-maeneo ya maegesho
-vijiwe
-shule
-vyuo
-biashara
-ardhi na viwanja vilivyopimwa.

Hii ilikuwa bahati yao. Baya kwa hivi sasa ni kwa chama tawala kukataa kurudisha kile kilicho haki ya wananchi wote na kisha kuvinyima vyama mbadala nafasi ya kuwa na mali kama ilizonazo.

Wazee, wazazi, vijana na wanawake wa taifa au ?
Hili la wazazi, wazee, vijana na wanawake wa chama fulani kupata upendeleo sio tu linaleta ubaguzi wa kichama na kisiasa lakini pia linaigawa nchi katika makundi ya wazazi, wazee, vijana na wanawake wa chama tawala na wazazi, wazee, vijana na wanawake ama wasio na chama cha kuwapendelea na kuwasaidia au wale wa vyama mbadala. Huu ni mwanzo wa wanasiasa hapo baadaye kuyatumia makundi hayo kusababisha fujo, ghasia na uvunjaji amani wa aina nyingine hapa nchini.

Kwa maoni yangu, chini ya mfumo wa vyama vingi ni bora kama makundi ya wazazi, wazee, vijana na wanawake yatakuwa ni makundi huru yasiyo na mshkamano na chama chochote cha kisiasa. Au makundi hayo basi yaonekane ni ya kichama na yasipewe kiujanja ujanja sura ya kwamba ni jumuiya za kitaifa. Vinginevyo, makundi hayo yasibague kati ya wanachama wa chama tawala na wale wa vyama vingine au wasio wanachama. Na misaada inapokuja isipitishwa kijanja kusaidia jumuiya hizo kama vile ni za kitaifa kumbe ni za chama kimoja tu cha kisiasa.

Sababu kubwa za kuwepo kwa ubaguzi wa kisiasa au kichama ni ule ukweli kwamba rasilimali na hasa fedha ambazo chama tawala inaweza kuwa nazo wakati wote ni kidogo. Licha ya hivyo kama ilivyo kwa taasisi nyingine yoyote wakubwa hujipendelea kwanza wao na kisha makombo yanayobakia ndio hupewa wanachama.

Makombo hayo pia ni dhahiri hayatoshi. Na kutokana na hili hata wanachama wenyewe ndani ya chama sioi wote wanaopata na kama wanapata hawapati kwa usawa. Sikuzote kuna wanaopata zaidi ya wengine.

Ikifikia hapa ni dhahiri kuona kuwa endapo chama tawala kitafanya ujanja na kikapata fedha kwa njia halali au za kiwiziwizi bado kiasi kinachopatikana hakitoshi kuwagawiwa na wasio wanachama. Hapa ndipo ubaguzi unapoanza na kisha kuendelea siku zote chama hicho kitakavyokuwa madarakani.

Kwa hiyo hatimaye ubaguzi ulioanza kisiasa au kichama huanza kuingia kuwa ubaguzi wa kijamii (matabaka ya wanaopendelewa na wasiopendelewa) kisha ubaguzi wa kijamii huwa ubaguzi wa kiuchumi (walio nacho hupewa zaidi na wasio nacho hunyang'anywa hata kile kidogo walicho nacho) na kisha kukomalia kuwa ubaguzi wa kiraia na kimaeneo ambao huzaa makundi ya watu ambao kufa kupona hukipigia chama fulani tu kura lakini sio chama kingine.

Ubaguzi wa kichama au kisiasa kama ulivyokuwa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini sio kitu chema na hakiashirii kuendelea kwa umoja, amani na mshikamano wa kitaifa bali kinyume chake. Chama chochote ambacho huwagawa wananchi kati ya wale ambao ni wanachama wake na wale ambao sio wanachama wake wakati kikiwa serikalini sio chama kinachostahili kuwa madarakani hata siku moja.

Apartheid ya kisiasa inaanzishwa na kuendelezwa Afrika kwa malengo ya chama fulani kupata wafuasi watumainiwa na wasiokitupa chama hadi pale hao wanachama wanapotupwa. Hili linaingiza gharama isiyoonekana kiuchumi ya kuwafadhili watu wasiochangia lolote katika ukuaji wa uchumi wa nchi husika.

Kutokana na kuwa rasilimali ikiwemo fedha ni chache na adimu vyama tawala katika nchi nyingi vinaona ni rahisi kugawa wananchi kati ya wananchi wake na wananchi wasio wananchi wake. Baada ya hapo inakuwa ni rahisi kuwatumia watu hao ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. Aghalabu, wananchi wanaokubalika na chama tawala kutokana na ama kuwa wanachama au wapiganaji wake kisiasa ndio wanaopata misaada mbalimbali inayotolewa kwa watu wote. Katika baadhi ya nchi imefikia kwamba hata wakati wa maafa, watumishi wa serikali au wafuasi wa chama tawala wanaopewa majukumu ya misaada hubagua kati ya wenzetu na wengine. Hawa wenzetu ndio wanaofikiriwa na kupata kwanza, wakati wengine huachwa bila huruma wala msaada wowote. Katika tathmini ya mali iliyoharibika 'mwenzetu' sio tu analipwa zaidi lakini juu ya hivyo huweza akapewa na mkopo usiorudishwa pia.

Rushwa ya kisiaasa.

Apartheid ya kisiasa ni rushwa kama zilivyo rushwa nyingine. Wapenda demokrasia wote wanapaswa kuipiga vita kwa ukucha na jino. Ni rushwa mbaya zaidi maana inatumia umasikini na unyonge wa mwananchi kumlazimisha raia kujiunga na chama fulani au kukipigia chama fulani kura hata kama yeye moyoni hakipendi na hakitaki chama hicho.

Nimewahi kuzungumza huko nyuma kwamba rushwa mbalimbali tunazoziona katika nchi yetu asili na chanzo chake ni wanasiasa. Rushwa ikishapangisha kwenye ghorofa ya juu kabisa ya nchi kupitia chama tawala basi inakuwa ni vigumu sana kuipiga rushwa vita katika ghorofa za chini. Na hii ndiyo hali iliyopo katika nchi nyingi za Kiafrika. Rushwa imo katika chama tawala na chama tawala kinapona na kubakia madarakani kutokana na rushwa na sasa inakuwa ni kazi kuwa na uhakika kwamba kinaweza kurudi tena madarakani bila kupewa na chenyewe kutoa rushwa.

Faida za apartheid ya kisiasa

Zaidi ya manufaa ambayo viongozi na chama fulani hupata apartheid ya kisiasa haina faida kwa wananchi walio wengi na nchi husika.

Hasara za Apartheid ya kisiasa

Hasara ya kwanza ni kuwagawa wananchi kati ya wanachama na wasio wanachama. Jambo hili huongeza jeuri, kiburi na ujibari wa wanachama wa chama tawala dhidi ya wananchi wenzao.
Katika hali kama hii kuna kuwa hakuna amani, kuaminiana wala mshikamano kati ya wananchi.

PIli, apartheid ya kisiasa huwanyang'anya walio wengi kipato na kipato hicho kupewa watu wasiostahili kukipata. Matokeo yake ni kuwa na wanasiasa uchwara ambao fedha huwalewesha wakajihusisha na uchafu wa kila aina na kusahau majukumu yao kama viongozi na wasimamizi wa maendeleo ya watu na nchi yao.

Tatu, vyombo vya dola hulazimika kupendelea kabila moja (wanachama) dhidi ya makabila mengine (wasio wanachama) na hatari ya hili ni kwamba dhuluma na unyanyasaji ukizidi nchi 'inarwandishiwa'.

Nne, katika jamii yoyote asilimia ya watu walio na akili ya kuleta maendeleo ya watu wote ni chini ya asilimia nne. Hawa wamegawanyika sio kwa kufuata uzawa, kabila, makazi au jinsia bali kwa namna isiyoeleweka na isiyotambulika. Lakini katika kundi lolote la watu ukilichunguza utakuta halina zaidi ya asilimia hiyo nne, aghalabu, idadi huwa chini ya hapo. Katika Afrika asilimia hii inasemekana kushuka chini hadi 2 kama sio moja tu.

Unapojenga apartheid ya kisiasa, kwa bahati mbaya wewe ukawa na 'wajinga' zaidi kuliko wale 'wenye akili' ndio unajenga safu za uongozi usiokubali kukosolewa, ambao ukifanya madudu bado unaona umefanya sawa tu na unaoamini siku zote wao ni bora na safi zaidi kuliko watu wengine na kinachotokea ni wao kuonewa tu wivu na wale waliokosa. Kiburi na dharau hii ya kutupwa haiwezi kamwe kujenga taifa bora na imara.

Huko Afrika Mashariki kwa mfano katika kisiwa cha Zanzibar wananchi wengi waliojaliwa akili na ujasiriamali wametengwa na waliomo serikalini. Na katika kijinchi hicho inavyoelekea wenye majaliwa ni chini ya asilimia 2 na wote hawa wamewekwa nje ya serikali. Matokeo ya hili yako wazi kwa yeyote mwenye macho kwenda kusikia na kuona hao waliobeba jukumu la uongozi katika sehemu hiyo ya Afrika Mashariki. Laiti isingelikuwa kubebwa na Tanzania bara, Wazanzibari wanaofanya kazi nje, biashara za kiajabuajabu na misaada toka nje leo wanavisiwa hao wangelikuwa wakitembelea magoti.

Wengi wa wanaojifanya ni wanachama wa chama hiki au kile Afrika wanafanya hivyo kutokana na njaa au uoga.
Aghalabu kwa kuwa mara nyingi chama tawala huonekana kwamba ndio walioshika mpini, basi wananchi walioshika makali wanaogopa wasikikaidi kisha kikavuta mpini huo kwa hasara yao. Hili halina dawa nyingine bali kuhakikisha kuwa wanaoshika mpini ni wananchi na sio chama chochote kile cha kisiasa kwa kuimarisha na kukuza demokrasia inayofanya kazi Afrika.

Kama tulivyokataa apartheid na ubaguzi wa aina nyingine hapa Afrika lazima wapendwa Uafrika na Waafrika wa kweli hapa duniani wakatae kabisa ubaguzi wa kichama. Lazima tulee familia, koo, mitaa, kata, tarafa, wilaya na mikoa ambayo sisi sote bila kujali ni wanachama wa chama fulani tunachukuliana kama watoto wenye sifa na tabia tofauti ambazo ni lazima tuviumiliane kama tunataka tuishi kwa amani na upendo.

Wanaochgia kasi ya kukua kwa ukabila wa kichama ni 'washangiliaji' na wala sio watendaji na wazalishaji mali wa kutegemewa na watu na nchi zetu.

Nini kifanyike ?

Jambo la kwanza la kufanya kabla ya kuchukua hatua zinazofaa kuirejesha hali kama ilivyokuwa kabla ya leo ni pamoja na kujiuliza:

Je, kuna chama chochote mtaani, wilayani au mkoani kinachoweza kuanzisha jambo la manufaa bila kukwaza na serikali ?

Je, kuna wanachama wa chama chochote isipokuwa chama tawala wanaoweza kukutana au kufanya maandamano bila kuingiliwa na vyombo vya dola ?

Je, mfanyabiashara akikiunga mkono au kukipigia debe chama kingine isipokuwa chama tawala biashara na mali zake zitakuwa salama ?

Je, chama chochote cha siasa kinaruhusiwa kujenga viwanja vya michezo, shule, hospitali na majengo mengine bila bughudha ?

Je, vyama vya upinzani vinaruhusiwa kuwa na vyombo vyao vya habari ?

Je, nini kinatokea kama chombo fulani cha habari kinaunga mkono au kuwatangaza zaidi upinzani kuliko chama tawala ?

Je, usipokuwa mwanacha wa chama tawala ajira yako na kupanda kwako cheo na maslahi yako yanakuwa sawa na wale wa chama tawala ?

Je, watoto na wake wa wasiokuwa katika chama tawala wanapata jamala na nyenzo sawa na wale wa chama tawala ?

Majibu kwa maswali haya yatatoa njia na mbinu za kushughulikia ukabila au ubaguzi wa kichama katika nchi zetu kwa namna bora na ya uhakika zaidi.

© 2009 Sammy W.I.Makilla

No comments: