Saturday, July 11, 2009

DEMOKRASIA NA UWEZESHWAJI WA VYAMA VYA UPINZANI

HAIWEZEKANI kuwa na demokrasia ya kweli katika nchi nyingi za Kiafrika kutokana na nguvu kubwa iliyo nayo chama tawala ukilinganisha na udhaifu mkubwa wa vyama mbadala.

Kubwa zaidi ni kukosa uwezo wa kuwa na ofisi katika kila wilaya, mji na kijiji; pia kukosa uwezo wa kuwa na vyombo vya usafiri vinavyofaa na kutosheleza mahitaji yao; hali kadhalika, kuwa na fedha za kutosha kuwalipa baadhi ya watendaji wao ili washughulike na kazi moja tu ya kukijenga chama na uwezo wake wa kuchangia maendeleo ya nchi na watu wake.

Kwa sababu hii ninashauri watu wote ikiwemo wafadhili toka nchi za nje kwamba wakati umefika sasa wa kusaidia vyama mbadala kuwa na msingi bora na imara wa kuanza kushirikisha kikamilifu na kwa dhati katika siasa za vyama vingi nchini.

Ninapendekeza msaada huu usiwe ni sadaka bali ni mkopo wa riba nafuu na utakaolipwa baada ya miaka 20 au zaidi. Mikopo hiyo iwawezeshe wanasiasa na vyama vya siasa mbadala kujenga ofisi ambazo pia zitakuwa na vyumba au ghorofa za kukodishwa ili kuviingizia pato kila mwaka; vyombo vya usafiri na fedha za mbegu za kusimika vyema mizizi ya vyama hivyo hasa huko wilayani na vijijini.

Uhalali wa vyama mbadala kusaidiwa katika hili unatokana na ukweli huu hapa chini:

Vyama tawala vingi vilikuwa na miaka 35 au zaidi ya kujilimbikizia ukwasi na mali za kila aina wakati vyama mbadala havina zaidi ya miaka 10 toka vianze kutafuta wapi pa kuanzia. Isitoshe vyama tawala vinavibana vyama mbadala kwa kila hali ili visijenge na visiwe na uwezo kama wao wakijua fika kwamba kwa kuwaachia wapinzani kuwa na nguvu basi utakuwa ni msiba kwao. Kwa hiyo hatuwezi kutarajia serikali ya chama tawala fulani kusaidia kuimarisha chama cha upinzani waziwazi. Ingawa hili halizuii mtu mmoja mmoja katika chama tawala kusaidia chama hiki au kile mbadala kwa sababu moja au nyingine.

Aidha vyama vingi tawala kwa kupitia kisingizio cha ujamaa na utafa vilipora mali za wananchi na kuzifanya mali za chama. Hadi wa leo hakuna chama chochote tawala kilichokiri hili na kuzirudisha mali hizo ila pale ambapo chama hicho kimeondolewa madarakani na mahakama au wananchi wenyewe kudai na kunyakua kilichokuwa chao.

Vyama vingi tawala Afrika vimejenga nyufa na mianya makusudi ili kuiba fedha toka Hazina, bima, pensheni, mfuko wa usalama wa jamii, wizarani, serikali za mitaa na mashirika kama hayo kwa namna ambayo chama hakihusishwi kabisa na wizi huo ingawa kwa yakini mwizi ni chama na sio hao wanaotumiwa na wanasiasa na makuwadi wao wa fedha haramu wanazoibiwa wananchi wakiwemo wanyonge kama wazee, mayatima, wagonjwa, wanavijiji, walemavu na wengine kama hao.

Kwa kutumia mamlaka za kodi aidha vyama tawala katika nchi nyingi huwafanya wafanyabiashara na wenyeviwanda na wawekezaji ama kwa kupenda au kushawishiwa kiujanja au kulazimishwa au kwa kutoa rushwa kuvipatia fedha vyama hivyo kwa mihadi kwamba mali zao zitaongezeka pale chama kinaporudi madarakani.

Fedha nyingi ambazo vyama tawala vinapata hazitumiwi ili kuwaelewesha wananchi vijijini kwamba vyama vingi na demokrasia ni jambo zuri kwa nchi zetu bali hutumika kwa kazi kinyume cha hiyo. Aghalabu fedha hizo hutumika kuwaghilibu wananchi kwamba watakuwa maskini zaidi, wataingia katika matatizo makubwa na pengine hata watauawa wakichagua chama kingine kutawala nchi.

Ni vyama mbadala vichache sana ambavyo watumishi wake wana mishahara au uhakika wa kipato jambo ambalo ni tofauti kwa upande wa vyama tawala. Uhakika huu kwa vyama tawala unawapa watumishi wake jeuri, kiburi, tamaa na ulafi wa kupata zaidi na dharau ya kuwaburuza wananchi. Wakati unyonge huu unawapa watumishi wa vyama mbadala matende ya kuthubutu na kujaribu yale yanayoweza kuendeleza na kuimarisha upinzani nchini.

Hoja hizo hapo juu ni tosha kuonesha kwanini wazo la kuvisaidia vyama mbadala viwe na miguu yake vyenyewe ni suala muhimu na yakini ndio stata ya upinzani wa kweli katika nchi nyingi za Kiafrika.

Ili kukuza na kuimarisha demokrasia Afrika ni muhimu mambo haya yafanyike:
. Vyama mbadala viwezeshwa kuwa na majengo ya ofisi tarafani,wilayani, vijijini, kata, mitaani ili sio tu kuwa na makazi maalum yanayotambulika na kuheshimika lakini pia vyanzo vya mapato ya kila mwaka ya uhakika ili kuondokana na tamaa ya rushwa au misaada inayoua demokrasia badala ya kuijenga.
. Ni muhimu pia kwa kutambua ukubwa na upana wa nchi hii kwa vyama mbadala kupewa misaada na mikopo itakayowawezesha angalau kuwa na vyombo vya usafiri ambavyo vinaweza pia kukodishwa na kuingizia mapato chama wakati visipohitajika kwa shughuli za kichama.

. Ni muhimu watu kama Westminster Foundation for Democracy, George Soros Foundation, USIS na Umoja wa Mataifa kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo au ruzuku katika miaka ya mwanzo ili angalau sehemu nyeti ya wafanyakazi wa vyama mbadala vya kisiasa kuwa wanalipwa mishahara.

. Hili liende sambamba na wahisani kusaidia kujenga uwezo wa menejimenti na utawala ili waweze kusimamia mambo yao kisayansi na sio kisanii.

. Hili linaweza kufanyika vizuri zaidi kama kila chama kitakuwa na mpango wa kuandaa 'Strategic Planning' yake kwa shughuli za ndani za kichama na ile ya kukikuza na kukiimarisha chama kitaifa.


Pamoja na mambo mengine Mpango huo wa Kimkakati utavisadia vyama hivyo kuwa na miundo na mifumo ya vyama isiyo na matatizo na inayokwenda na wakati.

Yumkini wanasiasa wengi wa vyama mbadala wanaonekama kama watu waliochanganyikiwa, wenye matatizo yasiyokwisha, masikini na watu wenye njaa kali sio kwa sababu vyama mbadala vinataka hivyo ila kwa sababu chama tawala na serikali vinafanya makusudi ili waonekane hivyo. Hii ni tofauti kabisa na huko Ulaya na nchi nyingine zilizoendelea kidemokrasia ambako viongozi wa vyama mbadala hawachukuliwi tofauti na wale wa vyama tawala kwa kiasi hicho.

Ni dhahiri basi kwamba endapo vyama mbadala vitapata mikopo au misaada ya kufanikisha mambo hayo hapo juu hawatashindwa kuwajulisha wananchi kwamba vyama vingi ni kitu kizuri kwao na sio jambo baya kama vile vyama tawala Afrika vinavyofanya lionekane kwa hivi sasa.

Mapendekezo yangu ni kwamba pawe na:
MFUKO WA KUWAJENGEA VYAMA MBADALA AU UPINZANI MISINGI IMARA YA USHINDANI WA KISIASA KATIKA NCHI ZA KIAFRIKA KAMA INAVYOFANYIKA HUKO ULAYA KWA MSAADA WA BW. GEORGE SOROS.

Mfuko huo utoe mikopo ya riba nafuu ili angalau vyama mbadala vijenge ofisi moja kubwa katika ngazi ya mkoa na moja kila wilaya na kisha ndogo ndogo kwa kila tarafa.

Ofisi zote zipatiwe vifaa na zana muhimu za kazi.

Wakopeshwe fedha za uendeshaji kwa miaka 3 na kisha baada ya hapo baada ya kufundisha jinsi ya kukodisha baadhi ya vyumba katika majengo yao mbinu za ujasiriamali jamii ili waweze kuendelea na kazi ya kujenga na kupanua vyama vyao wao wenyewe.

© 2009 Sammy W.I.Makilla

No comments: