Sunday, July 26, 2009

DEMOKRASIA NA TAASISI ZA KIJAMII NA KIIMANI

MWAKA 1961 Tanzania ilipopata uhuru kulikuwa na vikundi huru kadhaa vikishughulika na mambo mbalimbali kuanzia maslahi ya ukoo, mtaa na kabila. Taasisi nyingi zilizokuwepo zilikuwa kwa ajili ya kutoa huduma na msaada kwa makundi fulani ya kikabila, kieneo, kidini, kibiashara,kikazi na kiuzalishaji mali.

Miaka michache baadaye chama cha TANU kikaitangaza nchi hi ni ya chama kimoja. Makundi mengi ya kijamii na kiuchumi yakanyimwa haki na uhuru wa kufanya kazi zao za kuisaidia jamii au wanasiasa wakaingizwa kwenye makundi hayo ambao badala ya kujenga walivibomoa na kuvimalizia mbali kabisa.

Mbadala ukawa ni chama cha TANU na baadaye CCM kulazimisha watu wote waliotaka maendeleo na neema kujiunga na makundi maalum yaliyoanzishwa kwa nia, sababu na maguvu ya kukifanya chama hicho kiwe na nguvu na uwezo kuliko sehemu yoyote ya jamii katika nchi hii.

Makundi hayo ni pamoja na yale ya vijana,wanawake, wazee/wazazi, wafanyakazi, wanafunzi na kadhalika. Huu ukawa mwanzo wa kile ambacho leo tunaita ubaguzi wa kichama au kisiasa ambao ni ile hali ya chama tawala kutumia mabavu ili kujinufaisha na kuwanufaisha wale wanaokiunga mkono katika masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Wengi watakumbuka kwamba ili mtu kuwa na uhakika wa kupata fursa ya kuendelea na masomo ulipaswa uwe na kadi ya TANU/CCM au vinginevyo ulikuwa huna njia nyingine ya kujiendeleza. Hili limekwisha kiuwaziwazi lakini bado liko kimafichomaficho.

Demokrasia ya kweli na inayofanya kazi haiwezi kuwepo kama kuna chama chochote cha siasa kinachotumia fursa ya kuwa chama kinachosimamia serikali kisha kuviamuru vyombo vya dola kubeza, kudharau, kupiga vita, kuvinyonya na kuvitendea isivyo haki vikundi vya kijamii visivyo na unasaba na chama tawala na jumuiya zake.

Ni muhimu kwa vijana, wanafunzi, wanawake, wazee, wafanyakazi, wanavijijini, wakulima, wafanyabiashara, watumishi wa umma na wengineo wawe na haki ya kuunda, kuanzisha na kuendeleza kikundi chochote cha kijamii na kiuchumi ambacho wanaamini kitakuwa na manufaa kwao na kwa jamaa zao na kwa jamii yao mtaani au kijijini.

Isipokuwa hivyo basi kutakuwa na mifukuto na migogoro na mioto ya chini kwa chini isiyoisha katika makundi ya kijamii ambayo badala ya kuchangia maendeleo ya watu vitakuwa ni vitu vinavyohujumu na kupoteza fursa mbalimbali za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mathalani, katiba inaruhusu haki ya kila mtu kuwa na uhuru wa kiimani na kuabudu. Kwa mapana yake na marefu ni kwamba raia yeyote wa nchi hii ana haki ya kukataa au kukubali kujiunga na kundi hili au lile katika masuala ya imani, dini na ibada. Na ni mwiko kwa serikali yoyote, iliyopo madarakani na zitakazokuja kupora na kupoka haki ya dini yoyote ile katika kukubali au kukataa taasisi fulani. Ni haki ya kidemokrasia ya mwananchi pia kuanzisha, kujenga na kuendeleza taasisi mpya endapo haridhiki au hakubaliani na zile zilizopo.

Hili linadhihirisha kwa wabunge na mawaziri wetu kwamba yale yanayofanyika leo katika kuinyima sehemu fulani ya jamii haki zao kwa upande mmoja lakini wakati huo huo kwa upande mwingine wabunge na mawaziri hao kuipa sehemu nyingine sio tu haki zao tu bali na ziada isiyodaiwa pia.

Huku hakuwezi kutafsiriwa kwa namna nyingine ila ni dhuluma na uonevu kwa yale makundi yanayonyimwa haki na maslahi yao mchana kweupe.

Aidha kitendo cha kuwa na bodi au mamlaka kuwalangua wakulima na kuwakatisha tamaa katika shughuli zao za kilimo hakutafsiriki kwa njia nyingine yoyote ile ila ni wizi wa jasho la mkulina na dhuluma na uonevu kwa waliomo katika sekta ya ukulima, uvuvi na ufugaji. Haki hapa ni kwa watu hawa kuwezeshwa kama wenye viwanda walivyowezeshwa kuzalisha na kuuza wao wenyewe kile wanachokizalsha.

Wafanyakazi wanapoamua hili au lile ili kupigania haki na maslahi yao na kisha kuingiliwa na mahakama au polisi pia hakuwezi kutafisrika kwa njia nyingine yoyote ile ila ni dhuluma na uonevu kwa wafanyakazi wa nchi hii. Mfanyakazi mmoja mmoja na kwa pamoja wana haki saa yoyote, wakati wowote na mahala popote kuonesha kutoridhika na hali ilivyo au uamuzi fulani na ni ruksa kwao kukutana, kuandamana, kupinga na kuonesha kilio na kutoridhika kwao.

Wachimbaji madini wana haki ya kidemokrasia ya kutafuta riziki yao ya kila siku. Na pale mgodi unapopewa ardhi ambayo wachimbaji wadogo ndipo walipokuwa wakipatia riziki yao wachimbaji hao wadogo wana kila haki ya kulipwa fidia ya kutosheleza riziki yao ya kila siku kwa miaka yao ya uhai iliyobakia.
Kinachofanyika sasa sio tu ni mauaji yanayobarikiwa na wakubwa, dhuluma na uonevu bali unyang'anyi wa mali ya Mtanzania unaofanywa na wageni toka nje.

Kuna wanojiuliza hivi haki ya wanawake kuwa na makundi yao ni kwa CCM tu. Huu sio ubaguzi wa kijinsia kwa wanawake wasiokuwa wanachama wa chama fulani na kilichoshika pochi la taifa ? Kwanini tulilikataa Baraza la Wanawake wa Tanzania lilikosudiwa kuwa mwamvuli wa makundi ya aina yote ya wanawake katika jamii yetu. Hivi tunaamini kuna kundi la wanawake katika nchi hii wanaostahili kuneemeka wao peke yao na neema mbalimbali zinazokuja Tanzania toka ndani na nje ya nchi ?.

Vijana kuanzia Arusha hadi Zanzibar wameachwa kwenye mataa na watawala waliopo. Maana vijana wenye maana ni wale wa chama tawala tu. Kutokana na hili wale wasiokipenda chama hicho wana wakati mgumu katika kujikwamua kiuchumi na kijamii. Je, hili ni sawa. Na kweli katiba inayovumilia jambo hili ni katiba yenye haki, usawa na uhuru kwa watu wote ?

Utengwaji huu wa vijana kutokana na ubaguzi wa kisiasa au kichama umechangia sio haba kwa Zanzibar kuwa na 'teja' kwa karibu kila familia visiwani humo.

Kutokana na kundi la Wazee lililokuwepo kuwa na mwegemeo wa kisiasa kuna wazee kadhaa waliodhulumiwa na wanaoishi maisha ya dhiki na ya umasikini mkubwa leo lakini kundi hilo la wazee la kichama sio tu haliwajulii hali bali pia halina mpango wa kuwasikiliza achilia mbali kuwasaidia katika kupigania haki zao. Tunalojifunza hapa ni umuhimu wa wazee wa kila eneo kuwa na chombo chao kwa ajili ya kupigania haki na maslahi zao wakingali hai na sio pale wanapokwishakufa. Wazee wa kisiasa wakati wa sakata la wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikaa kimya kama hilo jambo haliwahusu kabisa. Lakini ni vyema hapa wazee tukakumbushana kwamba ukimuona mwenzio ananyolewa na wewe tia kcihwa chako maji.

Wanafunzi nao wanasukwasukwa na kulazimishwa kuwa katika makundi maalum ambayo yanaishia kwa viongozi wake kushirikiana na wale wanaowakandamiza na hivyo kufanya shule na vyuo vyetu sikuzote viwanja vya migogoro na mapambano badala ya mahala vijana hao wanapoweza wakati mwingi kusaidia kufanya tafiti mbalimbali za kuiendeleza nchi hii na watu wake.

Faida za vikundi huru vya kijamii na kiimani

Kuna faida mbalimbali za kuwa na vikundi huru vya kijamii na kiuchumi katika nchi:

Kwanza, vinapanua wigo wa kutatua matatizo ya kijamii na kutumia fursa za kiuchumi na kijamii zilizopo kwa makundi mbalimbali ya watu katika jamii,

Vikundi huru vya jamii na hasa pale vinavyopewa nafasi ya uwakilishi vijijini,mjini, tarafani, wilayani , mikoani na kitaifa vinawezesha sauti ya kila mtu kusikika,

Ni njia ya uhakika na ya kuaminika zaidi ya kupanua, kuendeleza, kujenga na kuimarisha demokrasia katika ngazi ya chini ya taifa hadi ile ya juu kabisa,


Makundi huru ya jamii yanasaidia kuondoa kutawaliwa makundi na chama chochote cha siasa,

Vikundi huru vya jamii pia vinasaidia kuondoa kutumiwa kwa vikundi na wanasiasa kama ilivyofanyika kule Kenya, Zimbabwe na nchi nyingine za Kiafrika zinazobeza, kudumaza na kulemaza demokrasia,

Vikundi kama hivi vinasaidia pia kupunguza rushwa na hongo za kisiasa kwa kuwa vinajenga uwezo wa watu kujikidhi wao wenyewe mahitaji yao yote ya msingi na kinachobakia kwao sio njaa na ukata bali ni kutafuta kuendelea juu zaidi,

Vikudni vya kijamii vikijiingiza katika miradi ya ujasiriamali jamii vina uwezo mkubwa pia wa kutoa ajira kabakaba kwa vijana, wanawake na hata wazee wasiokuwa na kazi,

Vikudni vya jamii vina uwezo mkubwa wa kuchangia katika kuendeleza rasilimal watu bila hili kuwa na ila au njama ya aina yoyote ile kwa vikundi vingine katika jamii tofauti ilivyo na pale dini fulani inapotaka kupora kazi hii toka serikalini na kuifanya wao,

Vikudni vya kijamii vinavyofanya kazi na vinavyojua wajibu wao na Utaifa na Uzalendo wao vina kila sababu ya kuzuia wanasiasa na wafadhili toka nje kuwatumia viongozi wa makundi fulani,

Aidha ni vikundi hivi aghalabu vinavyovuka upofu na uoni mfupi wa viongozi wasiojua taradadi na tarajali za jamii ndivyo vinavyoweza kuzuia Taasisi za kidini kutumia ombwe linaloachwa na Serikali dhaifu ili kudhulumu dini nyingine katika masuala ya elimu, afya na huduma za jamii.

Fedha ya mlipa kodi itumike kupeleka demokrasia vijijini na sio kuiua demokrasia vijijini.

No comments: