Sunday, July 12, 2009

DEMOKRASIA NA UHURU WA KIUCHUMI NA KIJAMII KWA MAENEO NA WATU

AFRIKA ya leo sio ya jana. Huko nyuma wananchi katika nchi nyingi za Kiafrika waliwachukulia viongozi wao kama vile viongozi hao walikuwa BABA zao. Na viongozi hao waliona raha kuitwa baba wa taifa au baba wa hili au lile. Ingawa kwa kiasi kikubwa ni wachache sana kati yao walioweza kutimiza wajibu wao kama baba. Baba alitarajiwa kuwafanyia wananchi (wanawe hata kama wa kufikia) yale yaliyo ya baraka, heri na wema wa dhati toka ndani ya moyo wa mtu. Baba alitakiwa kuwa kielelezo cha utu na ubinadamu. Haikutarajiwa hata siku moja kuwa baba atakuja geuka kuwa mtu anayependelea kati ya wanawe; atawaibia wanawe; atawadhulumu wanawe; atawasingizia uongo wa kutupwa wanawe; atawanyanyasa na kuwatesa wanawe; hatafanza ubaguzi kati ya wanawe; atawagandamiza wanawe; atawadhulumu wanawe; atawaonea na hata kuwaua wanawe.

Kwa bahati mbaya BABA wa jana na wa leo Afrika anayafanya madhambi haya hapo juu kila siku. Na mwananchi amechanganyikiwa na anajiuliza amwamini na amtegemee nani sasa.

Tatizo kubwa la Ubaba ni lile la kutaka kusimamia NYUMBA KUBWA YENYE VYUMBA ZAIDI YA 50 AU SHAMBA LA HEKTA ELFU lakini wewe unajua na unatumia tu vyumba viwili au vitatu katika jumba hilo au moja ya nane ya hekta katika shamba hilo.

Kinachotokea kwingine huna habari nayo. Labda uletewe na mtu habari. Na mjumbe huyo mara nyingi huleta uongo au habari za kupkwa. Na wewe kwa kuwa huna muda aghalabu utakuwa unaukubali uongo kuwa ukweli. Matokeo yake mpaka funza anatoka kwenye dole huku kaacha watoto milioni mwilini mwako ndio unagutuka, ala, kumbe kidoleni kuna mama wa mafunza!

Uhuru wa Mikoa na Demokrasia

Wapigania demokrasia hawataki uhuru wa mikoa eti kwa sababu wanataka kuigawa nchi au kuvunja umoja na mshikamano katika nchi. Mungu aepushilie mbali hayo. Wanataka uhuru kwa mikoa ili tujenge umoja na mshikamano imara zaidi kutokana na kutumika kikamilifu fursa za kiuchumi na kijamii zilizoko katika kila mkoa. Mikoa kama inakosa ubunifu na ujasiriamali na utundu wa kujaribu mambo mapya na ikazalisha kidogo basi keki ya taifa inakuwa ndogo. Mikoa ikijititimua na kuzalisha zaidi na keki ya taifa nayo inakuwa kubwa kila siku.

Na uhuru wa kiuchumi na kijamii hauwezi kupatikana kupitia meza ya katibu mkuu wa wizara ya serikali za mitaa au wizara kama hiyo. Uhuru wa mkoa unapatikana kwa njia moja tu. Kila mkoa kuendesha uchaguzi wa kumchagua Gavana wake au Kiongozi wao wa mkoa, wawakilishi wao na wajumbe wao wa ngazi za chini. Gavana atachagua mionngoni mwa wabunge wa mkoa husika mawaziri wa serikali itakayosimamia masuala ya uchumi na jamii ya mkoa husika. Kwa kitendo cha siku moja safari ndefu ya kuwa na mikoa inayojiendesha kiuchumi na kijamii itakuwa imeanza. Kwa saini moja tu ya Mkuu wa nchi demokrasia itakuwa imesimika mizizi ya kweli kuanzia vijijini na miji katika kila mkoa. Kwa sheria moja tu toka bunge la taifa kila mkoa utakuwa na wawakilishi wake wanaojua ni wapi kiatu kinafinya na wanaozungumzia kila kwenye kikao matatizo na ufumbuzi wa matatizo ya wananchi wanaowawakilisha na sio porojo, umbeya, uzushi na ngonjera zisizo kwisha.

Ipo hatari pia ya kujilimbikizia mamlaka iwe yale ya kisiasa, kiuchumi, kirasilimali au kifedha.
Badala ya kutumika vyema aghalabu hutapanywa. Na hiki ndicho kinachotokea kutokana na sakata ya B.O.T., EPA, baadhi ya dini kugawana fedha za wafadhili na serikali na kashfa nyingine katika wizara, taasisi na mashirika mbalimbali ya kiuchumi na kijamii nchini.

Kwa kuwa nchi ni kubwa na watu ni wengi vibilioni mia au mia mbili au mia tatu ikivigawa vinakuwa havina uwezo wa kubadili maisha ya yeyote ila kwa yule mchotaji anayewahi kutoka na tonge kubwa kabla hicho kilichotolewa hakijaanza hata kugawiwa.

Kinachotakikana hapa sio fedha bali uhuru wa kiuchumi na kijamii kwa wananchi huko huko mikoani na majimboni walipo kukaa chini na kuweka mipango na mikakati yao ya maendeleo na kukusanya nguvu zao za mwili na za kifedha kuleta mabadiliko yanayoweza kukifanya kidogo kuwa sio tu kikubwa bali kinachojizalisha na kujiendeleza chenyewe na hivyo kuwahakikishia wakazi wa mtaa, kata, tarafa, wilaya au mkoa maendeleo endelevu. Kinyume cha hivyo kama nchi ilivyo tegemezi kwa wafadhili basi mikoa nayo itaendelea kuwa tegemezi kwa serikali na kuwa vipofu kwa fursa pekee za kiuchumi wanazoweza kuzitumia wao wenyewe na kuondokana na utegemezi huu unaotulemaza na kutudamaza takriban karibu miaka hamsini kufikia sasa.

Demokrasia ya kweli
Demokrasia ya kweli itatokana tu na kila Mkoa kuwa na Gavana au kiongozi wake wa kumchagua na sio wa kupachikwa na chama chochote cha kisiasa kiwacho au serikali iliyoko madarakani. Kazi za serikali ni kusimamia wizara kisiasa na kiutawala na sio kusimamia mikoa kiuchumi na kijamii.
Kazi ya kusimamia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya mkoa inastahili kufanywa na Gavana wa mkoa, mawaziri wa mkoa na wabunge wa mkoa. Hawa wamevaa kiatu husika na wanajua kinachofinya. Vinginevyo kazi hii ikifanywa katika ngazi za wizara, basi tutaishia kila waziri kutaka kupeleka miradi yote ya wizara yake katika mkoa wake kama sio jimbo lake la uchaguzi.

Gavana wa mkoa hatakuwa muuza siasa na sera bali mtendaji mkuu wa kiuchumi na kijamii. Mkoa utakuwa ni kampuni na yeye ni Mkurugenzi au Meneja Mkuu. Wakazi wa mkoa watategemea awe na mawaziri wa vitendo na sio wa maneno. Kama kuna waziri wa maji na umwagiliaji basi waziri huyo atahakikisha kila sehemu mkoani wanapata maji na kuna umwagiliaji maji. Kama ni waziri wa Viwanda na Biashara basi waziri huyo wa mkoa atahakikisha mkoa unapata wawekezaji ndani na nje ya nchi ili mkoa uwe na viwanda inavyovihitaji na vinavyoingiza faida na sio hasara au kugeuzwa kuwa maghofu au karakana au ghala za wafanyabiashara, wenye viwanda, taasisi zisizo za kiserikali na kadhalika.

Wabunge wa mkoa watakuwa ni wawakilishi wa maeneo ya watu kati ya 50,000 na laki mbili nao kazi yao kubwa itakuwa ni kuhakikisha sauti ya wananchi wake ndiyo inayotawala katika maamuzi na utekelezaji wowote wa masuala yanayohusu eneo lake. Jimbo lake litashindana na majimbo mengine mkoani kwa kuhakikisha wana rasilimali watu tosha, barabara nzuri, maji, umeme, mazingira bora kwa wawekezaji wa ndani na nje na vitu kama hivyo.

Kwa kufanya hivi kila jimbo, kila wilaya na kila mkoa utakuwa unapambana kuwaondoa watu wake toka kwenye umaskini unaowanyima haki yao ya kuchangia katika demokrasia na maendeleo ya kweli ya nchi na watu wake.

Katika hali tuliyonayo ambayo makosa ya serikali na yale ya wanasiasa yanaendelea kumasikinisha baadhi ya mikoa haitakuwa rahisi kujenga na kuimarisha demokrasia katika maeneo mengi katika nchi zetu za Kiafrika.

Bila umasikini wa kutupwa kuondoka itakuwa ni ndoto kutarajia kujengwa kwa demokrasia ya kweli na inayofanya kazi.

Hii ni demokrasia itakayoruhusu pamoja na mambo mengine mkulima kuuza mazao yake ndani na nje ya nchi; mvuvi kuuza samaki zake ndani na nje ya nchi; mwenye mali asili kama miti au madini kuuza alichokitafuta kwa gharama na kukipata ndani na nje ya nchi; Watanzania kuwa huru kufanya kazi au kwenda kucheza michezo nje ya nchi bila kuwekewa mikwara na mtu au taasisi yoyote.

Ni demokrasia ya kijamii na kiuchumi itakayowadhihirishia Watanzania kuwa anga ndio paa la matamanio na makusudio yao na yeyote anayewakwaza ni adui wa na adui wa taifa.

© 2009 Sammy W.I.Makilla

No comments: