Demokrasia ni nini ?
UTAMADUNI umejengeka wa kutafsiri demokrasia kama serikali ya watu , kwa ajili ya watu na inayosimamiwa na watu wenyewe. Hata hivyo katika miaka hii ya nchi kuwa na mamilioni ya watu sio rahisi kwa watu wote kushiriki katika serikali. Watu hushiriki kupitia kwa wawakilishi wao. Hii inaitwa demokrasia ya uwakilishwaji. Kama ni kweli hii ni demokrasia au ni kitu kingine ni suala linalohitaji mjadala mwingine.
Wasiwasi wa kama demokrasia ya uwakilishwaji ni demokrasia ya kweli unatokana na ule ukweli kwamba mara nyingi imetokea kwa wale wanaowawakilisha wenzao kujifanya wao ndio serikali na kupunguza kabisa nguvu za watu wenyewe katika maamuzi na utekelezaji wa yale ambao kama ni watu wenyewe wangelikuwa na uwezo ndio yangeamuliwa au kutekelezwa. Kwa maana nyingine katika dunia ya leo ni rahsi kwa kile kikundi cha watu kinachojiita serikali kupora mamlaka ya wananchi na kujifanya wao wenyewe ndio watu wote na maamuzi yao kuwa ni ya wote wakati sio kweli.
Tunaweza kusema basi kwamba ile demokrasia ya uwakilishwaji iwe ni demokrasia ya kweli ipo haja ya kuhakikisha kuwa yale yanayoamuliwa na wawakilishi ndio hasa yaliyokubalika na wananchi wenyewe na sio vinginevyo. Na hili haliwezi kufanyika endapo katiba ya nchi iliyopo ni ile inayoelekea kumpa kiongozi wa nchi na serikali yake fursa ya kupora mamlaka na uwezo wa wananchi bila ya wao kuulizwa au kuonekana kuwa wamefanya kosa la kikatiba na kisheria.
Ni nini maana ya Katiba ?
Katiba ni tamko la mkataba kati ya watawala na watawaliwa. Katika enzi za ufalme, usultani na uchifu katiba hazikuhitajika. Ilidaiwa watawala walikuwa wakichaguliwa na Mungu. Katika demokrasia katiba inahitajika ili kuhalalisha utawala uliopo.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyopo leo ni katiba iliyorithiwa toka chama kimoja. Pamoja na kuwekwa viraka kadhaa bado katiba hiyo inapwaya kutokana na mabadiliko makubwa yaliyotokea na yanayoendelea kutokea katika jamii yetu.
Katiba chini ya Chama Kimoja
Chini ya Mfumo wa Chama Kimoja, katiba ilikuwa ni tamko la kuhalalisha walio madarakani kufanya lolote lile kwa niaba ya wananchi. Hapakuwa na demokrasia. Kauli ya viongozi katika siasa ya Ujamaa ndiyo iliyokuwa ya mwanzo na ya mwisho.
Mahakama, vyombo vya habari na bunge vyote vilikuwa vinaendeshwa kwa namna ya kuwalinda watawala potelea mbali kama wanafanya mabaya au mazuri, wana haki au hawana haki, wanasema ukweli au wanasema uongo.
Sote tunajua mwisho wa yote siasa ya Ujamaa na udikteta wa chama kimoja vilitufikisha wapi.
Katiba mpya, mfumo mpya
Katika miaka hii ya vyama vingi na ushindani wa kisiasa na demokrasia katiba inatakiwa kutoa uhuru usio na mipaka kwa bunge, mahakama na vyombo vya habari ili kudhibiti viongozi wa serikali wasiipeleke nchi kubaya.
Aidha, serikali inatakiwa kuhakikisha vyombo vyote hivi ni huru kwa faida yake na faida ya wanachi wote kwa ujumla. Uhuru huu uwe ni ule unaoisaidia nchi kuumua ari, nguvu na uwezo wa wananchi katika kusimamisha taifa lililo makini na madhubuti kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kiteknolojia na kisiasa.
Katiba mpya ni muhimu kwa sababu kadhaa. Awali ya yote, katiba mpya ni jambo bayana kutokana na mabadiliko makubwa yaliyotokea nchini kiuchumi na kijamii.
Mabadiliko ambayo yamechangia watu kufilisi benki kuu bila viongozi wa juu kuwa na habari. Vilevile watu kuwa na vihimaya vyao ndani ya nchi bila wakubwa kujua. Kadhalika haki za binadamu kukiukwa bila ya viongozi kuwa na habari.
Nchi hii ikumbukwe kuwa ilikuwa ya chama kimoja leo ina vyama vya siasa vyenye kufurukuta angalau ya 10. Nchi hii haikuwa na televisheni. Ilikuwa na redio moja tu na vijiredio vidogo vya dini viwili vitatu. Nchi ilikuwa na magazeti mawili tu kwa nchi nzima.
Tunapozungumza hivi leo nchi ina magazeti zaidi ya 15 yanayotoka kila siku, magazeti ya wiki takriban 100 achilia mbali majarida na magazeti maalum na ya msimu. Nchi hii ina televisheni takriban 20 na redio zaidi ya 50. Je, katika hali kama hii hata kama wizara husika itakuja na sheria hii au ile tutaweza kudhibiti hali hii bila ya katiba mpya ianayoainisha vizuri zaidi mahusiano ya vyombo hivi na watu kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine ?
Udhaifu wa katiba iliyopo
Katiba iliyopo hivi leo ina udhaifu wa aina mbalimbali. Udhaifu huo ni pamoja na:
. Katiba inazungumzia nchi hii kuwa ya kijamaa wakati inaishi na kufanya shughuli zake zote kibepari;
. Katiba haizungumzii maadili na sifa nyinginezo anazostahili kuwa nazo mtu anayeitwa Mtanzania;
. Katiba ina udhaifu katika kuzungumzia jinsi makundi ya watu kwa makabila yao au shughuli zao za uchumi na maeneo ya nchi yanavyostahili kuendelezwa kutegemeana na vipaji, rasilimali na mazingira yao;
. Katiba haizingatii kwa ukamilifu wake mabadiliko makubwa ya kisiasa, kijamii, kichumi, kiteknolojia, kiutamaduni na kiutandawazi yanayotokea na yanayoendelea kutokea nchini na duniani kwa ujumla;
. Katiba ina vifungu vya sheria mbalimbali zinazowanyang'anya wananchi haki ambazo tayari wamepewa na vifungu vingine.
. Katiba inakataza ubaguzi wa rangi na kikabila lakini haikatazi ubaguzi wa kichama na ksiasa;
. Katiba haizungumzii jinsi tunavyoweza kuhusiana na majirani zetu na hivyo kujenga uchumi na jamii bora zaidi;
. Katiba inapendelea na kuwapa haki zaidi watawala kuliko watawaliwa, na kwa hiyo, watawala kupora haki za msingi za watawaliwa;
. Katiba haitilii mkazo wa kutosha kuhusu kulinda na kuendeleza mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania, ikiwemo kuhifadhi lugha zetu za asili kwa kutumia Teknohama;
. Katiba haitamki kwa uhakika nafasi ya lugha ya Kiswahili katika maendeleo yetu ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kiteknolojia na kadhalika;
. Katiba bado inampa mtawala haki ya kudhibiti mahakama na Jaji mkuu badala ya vyombo hivyo pia kuwa na uwezo sawa wa kumdhibiti mtawala;
. Katiba bado ina vipengee vinavyokwaza uhuru wa vyombo vya habari;
. Katiba sio kamilifu kuhusu suala la Muungano na hivyo kuzusha malumbano na mitafaruku ya mara kwa mara kuhusu suala la Muungano;
. Katiba na sheria nyingie bado zinamnyima mkulima kuuza mazao yake nje yeye mwenyewe kwa kisingizio hiki au kile wakati wenye viwanda wanaruhusiwa kufanya vivyo. Hili linaonekana ni upendeleo kwa wafanyabiashara na wenye viwanda na uonevu na unyonyaji kwa wakulima na watu kama wao;
. Katiba bado inainyima mikoa ambayo baadhi yake ni mikubwa kuliko Rwanda au Burundi madaraka ya kusimamia shughuli zao za kiuchumi na kijamii ili kuongeza kasi ya maendeleo yao;
. Katiba haina lolote la maana juu ya hifadhi na ustawi wa vijana, wanawake, wazee na watoto zaidi ya siasa za kawaida;
. Katiba bado inahesabu mali za wananchi kuwa ni mali za serikali [kwa mfano magazeti, redio na televisheni za wananchi vinachukuliwa na vinatumika kama vyombo vya serikali kwa ila au kwa mazuri].
. Katiba haina lolote la maana kuhusu udhibiti wa matumizi ya mali ya umma na hazina za taifa;
. Katiba haioneshi lolote kuhusu kuongeza ubora uwe wa serikali kuu yenyewe, wizara zake, mahakama, magereza, vyuo au shule za umma na maeneo kama hayo mwaka hadi mwaka;
. Katiba haioneshi waziwazi nafasi ya ushirikishwaji wananchi katika maamuzi yanayohusu maisha yao ya kila siku;
. Katiba haioneshi lini nchi nzima itakuwa na umeme, maji, huduma na mitandao mingine na kadhalika;
. Katiba haianishi namna ya kufanya mabadiliko muhimu ili serikali iweze kuwa na ufanifu na ufanisi zaidi katika shughuli zake;
. Katiba haina nafasi kwa upendeleo kwa wanasanyansi, wavumbuzi na wasomi wengine wanaoweza kuchangia kasi ya maendeleo yetu kuwa ya haraka zaidi;
. Katiba haitoi upendeleo kwa wazawa na hivyo nchi inaonekana kutothamini watu wake na badala yake inathamini wageni zaidi;
. Katiba haina ushawishi katika masuala ya kuendeleza vipaji, uwezo, akili, michezo na majaliwa mengine waliyonayo vijana wetu;
. Katiba haishughulikii ipasavyo suala la rasilimali watu, elimu na ajira au watu kujiajiri wenyewe;
. Katiba haiainishi ipasavyo haki na wajibu wa vyama mbadala, wanasiasa wasioko madarakani na wanachama wao kwa ujumla;
. Katiba bado ina mapungufu katika kutoa haki kamili za kuabudu kwa baadhi ya dini na madhehebu;
Mkutano wa Katiba
Hayo hapo juu si masuala mepesi. Ni masuala mazito. Ni masuala yanayohitaji muda kuzungumziwa na kisha kufikiwa maamuzi ya msingi katika kukubaliana au kutofautiana kimawazo. Na baada ya hapo kwa kutumia demokrasia kuamua kukubali yale ya msingi kuwa ndio mkataba mpya kati ya watawala na watawaliwa. Mkataba ambao sasa utaonekana na ile mianya inayowafanya watawala kujifanya mabwana na watawaliwa kuonekana na kujiona wao ni watwana wa wale walioko madarakani.
Ili katiba iwe kamilifu itabidi kushughulikia masuala haya moja baada ya jingine pamoja na mengineyo ambayo kwa sababu ya uharaka na nafasi sikuweza kuyataja. Ni pale tu katiba itakapokuwa haina mashimo na mabonde yanayoweza kuturudisha kwenye udikiteta wa chama kimoja na siasa za uchumi za majaribio
ndipo Watanzania watakapoweza kujihesabu kwamba sasa wamo na wanapita katika njia ya demokrasia ya kweli.
© S.W.I.Makilla 2009
Sunday, May 24, 2009
Subscribe to:
Posts (Atom)
