Wednesday, June 10, 2009

DEMOKRASIA NA WAGOMBEA HURU

Mgombea huru ni mtu gani ?

Mgombea huru ni raia yeyote katika nchi fulani anayegombea nafasi yoyote ile ya uongozi bila kuwa mwanachama wa chama fulani.

Katiba kwa kawaida huainisha wajibu na haki za watu kwa misingi ya matamko mbalimbali ya Haki za binadamu na nyinginezo na kisha hutoa haki kwa kila mtu katika misingi ya usawa, ikiwemo ile haki ya kupigiwa na kupiga kura. Baadhi ya nchi hapa Afrika , hata hivyo, zimeamua kuwadhulumu wananchi wao kwa kuwanyima watu wao haki ya kupigiwa kura kwa visingizio vya aina mbalimbali . Ni haki ya wananchi kudai na kuona kwamba wanakuwa na uhuru wa kupigiwa na kupiga kura. Na sio waruhusiwe tu na pengine kulazimishwa kupiga kura lakini wasiwe na haki ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi toka chin hadi juu katika nchi yao.

Uamuzi wa mtu kuwa mgombea huru husababishwa na mambo mbalimbali. Hufanya hivyo, aghalabu, kwa sababu anaamini kwamba viongozi wa vyama walipo ni bomu na hawawezi kufikisha jimbo au mkoa au nchi pale sehemu husika inapostahili. Wakati mwingine hukataa kuwa mwanachama wa chama fulani kwa sababu ya kiwango cha wizi na ufisadi anauona ndani ya chama husika. Aidha, huweza kukataa pia kuwa mgombea wa chama fulani kwa sababu anaamini kwamba vyama vilivyopo havitetei maslahi ya mwananchi bali maslahi binafsi ya viongozi wa vyama hivyo.

Vilevile, huweza kuamua hivyo kutokana na kutambua fika viongozi waliopo wamebeba na hawana uwezo wa kiakili, kifikira na kivitendo wa kuongoza watu na nchi.

Dhuluma kubwa inayofanywa na katiba iliyopo ni ile ya kumpa mtu haki ya kupiga kura [bila kujali ni mwanachama au sio mwanachama wa chama fulani] lakini wakati huo ikamnyima haki ya kupigiwa ila tu mtu anapokuwa ni mwanachama wa chama cha kisiasa kilichosajiliwa.

Ni dhambi isiyo na msamaha kwa mwananchi yoyote kushiriki katika vitendo vya uhuni, ubabe, unyang'anyi wa haki na uhuru wa mtu kupitia katika kuichezea na kuivuruga katiba kwa maslahi ya wachache au chama fulani cha kisiasa. Ndivyo ilivyo pia katika kupora haki ya mgombea huru.

Hadi wa leo hapajaruhusiwa kuwa na mgombea huru, mathalani, nchini Tanzania. Hata hivyo, mtu akiangalia kwa makini atagundua kuwa amri ya kukataa wagombea huru haiungwi mkono na vifungu mbalimbali vya katiba.

Katika sura hii tutajaribu kulionesha hilo huku tukitaraji kuwa wanasheria na wapigania haki na uhuru wa binadamu kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi wataliangalia jambo hili kwa macho mapya na kuondoa dhuluma wanayofanyiwa wale wanaotaka kufikia hatua ya juu katika msonge wa mahitaji ya binadamu kama ilivyoainishwa na Abraham Maslow.

Mitihani kwa wasiokubali vyama vilivyopo

Hali ilivyo hivi sasa ni kwamba mwananchi au mwanasiasa anayetaka kuwa mgombea huru anaiweka nchi au yeye mwenyewe anajikuta katika mitihani ifuatayo:
a) Kama ni mwanachama wa chama fulani anajikuta kifungoni pale anapokuwa kakiona chama ni kichafu na kibovu kiasi cha kutisha;
b) Anajikuta ni mnafiki kwa nafsi yake na anaowawakilisha;
c) Analazimishwa kutekeleza sera na mambo asiyokubaliana nao;
d) Ananyimwa nafasi ya kuchangia ubunifu, mawazo mapya na kutumika kwa fursa za maendeleo au kutatua matatizo ya wananchi kwa njia bora na yenye manufaa kwa wananchi zaidi kuliko inavyofanywa na chama au vyama;
e) Anajikuta hawezi kutumia haki zake nyingi alizopewa kikatiba kama raia;
f) Anajikuta kwamba ingawa yeye ni bora kuliko wengi wengine ananyimwa nafasi ya kuongoza nchi;
g) Inafikia hatua nchi inaongozwa na viongozi dhaifu, wezi na wabovu kutokana na vyama kuwazuia au kuwapiga vita watu walio bora kuliko wao;
h) Kwa kuwa viongozi hao (wanaowazuia wagombea huru) wanajua hakuna wanachokifanya na hawajiamini wanaanza kujiingiza kwenye vitendo vya kuimaliza nchi kiuchumi na kijamii kama bima yao ya baadaye endapo wataondolewa madarakani kwa njia yoyote ile. Njia hizo za kuifukarisha zaidi nchi ni pamoja na kushirikiana na watu wengine kuibia benki kuu na serikali au kuingia mikataba ya kiwizi wizi au kutumia fedha zilizopangwa kwa maendeleo ya wengi kwa maslahi binafsi kwa wachache au ya chama chao.

Kulazimisha uanachama ni kuvunja katiba

Kuwalazimisha watu kuwa wanachama wa chama cha kisiasa ni kosa. Kumnyima mtu haki ya kupigiwa kura eti kwa sababu sio mwanachama wa chama cha kisiasa nalo ni kosa. Na haya yote yanaweza kushuhudiwa na vifungu mbalimbali vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano [1998] hususan Sura ya Kwanza, Sehemu ya Kwanza hadi ya tatu, kama tutakavyoonesha hapa chini.

Kifungu namba 5.-(1) cha katiba ya JMT kiasema "Kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka
kumi na minane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi
unaofaywa Tanzania na wananchi. Na haki hii itatumiwa kwa
kufuata masharti ya ibara ndogo ya (2) pamoja na masharti
mengineyo ya Katiba hii na ya Sheria inayotumika nchini
Tanzania kuhusu mambo ya uchaguzi."

Masharti yaliyomo katika ibara hiyo ya pili hayazungumzii kabisa kwamba raia huyo lazima awe mwanachama wa chama cha kisiasa. Kutaka mgombea kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa lakini sio akiwa mpiga kura ni hitilafu ya kisheria yenye kuonesha uonevu na dhuluma dhidi ya haki ya kikatiba ya raia.

Ingawa kifungu namba 8.-(1) katika katiba hiyo hiyo Sehemu ya pIli kinabainisha kwamba " Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata
misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo -
(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali
itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa
wananchi kwa mujibu wa Katiba hii;
(b) lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;
(c) Serikali itawajibika kwa wananchi;
(d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao
kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii " msimamo wa sasa wa serikali kutokubali mgombea huru unaonesha sio wananchi walio na haki na uhuru wa kuamua bali ni serikali. Ari iliyoko kwenye kifungu hicho haionekani katika maamuzi na vitendo vya serikali inayotakiwa kuisimamia katiba hiyo. Ari hiyo ingelikuwepo kutokana na kifungu hiki tu, serikali isingethubutu kupinga kuwepo kwa mgombea huru.

Watanzania kunyimwa haki ya kugombea uchaguzi kama wagombea huru hakuungwi mkono hata kidogo na kifungu Namba
12.-(1) ambacho kinabainisha wazi kwamba: " Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa."

Na sehemu yake ya
(2) inaendelea: " Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na
kuthaminiwa utu wake."

Hali ilivyo sasa ni kuwa anayetaka kuwa mgombea huru hana haki wala usawa. Na ni pale tu serikali itakapopenda ndio atapata heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.

Pamoja na kuwanyima watu uhuru wa kuwa wagombea huru bado serikali imeendelea kukubali kifungu Namba
15.-(1) kinachotangaza kuwa: " Kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru.

Ambacho kinashadidiwa na kifungu kidogo cha
(2) kinachosema: " Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na
kuishi kwa uhuru, itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote
kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini,
kuhamishwa kwa nguvu au kunyang'anywa uhuru wake ......."

Licha ya kauli hii serikali imeendelea kuwafungia watu kuwa wagombea huru na kuwahamisha kwa nguvu [kutoka kwenye kundi la wanaotaka kuwa wagombea na kuwaweka kwenye kundi la wapiga kura tu] watu na kuwanyang'anya uhuru wao wa kuwa wagombea huru katika chaguzi mbalimbali.

Vifungu vingine kama vile kile cha 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22 na 31 vingelikuwa vinaeleweka vizuri na wanasheria na wabunge waliopo wangeligundua kosa linalofanyika kwa kuwanyima watu kuwa wagombea huru katika uchaguzi.

Mathalani katika kifungu Namba 16 kinazungumza haki ya faragha ambayo inaweza pia kutafsiriwa kama haki ya mtu kuwa peke yake kwa kuwa hataki au hapendi kushirikiana na watu wa aina fulani waliomo katika chama fulani.

Haki ya Uhuru wa mtu kwenda atokako, Uhuru wa Maoni na uhuru wa mawazo kama ilivyo katika kifungu Namba 17 na 18 havionekani kuzingatiwa pia katika msimamo wa serikali wa kuwazuria wagombea huru katika chaguzi mbalimbali.

Kifungu Namba
20.-(1) kinathibitisha kwamba: " Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria
za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani,
kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo
hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au
mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au
kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo."

Kutokana na hayo hapo juu ni dhahiri kuwa serikali inakiuka kifungu hiki kwa sababu haiyumkiniki kwa mtaka kuwa mgombea huru kuwa anaathiri visivyo sheria za nchi. Ila kama kuna amri ya uonevu, kumnyima mtu haki yake na ukandamizaji.

Aidha kifungu kinachozungumzia Uhuru wa kushiriki shughuli za umma
na hususan Haki ya Kufanya Kazi ni kifungu kilicho bayana kikibainisha kwamba kwa muktadha wa kile tunachokizungumza kuwa uamuzi wa kuzuia wagombea huru ni uamuzi wa kumnyima mtu haki ya kushiriki shughuli za umma na kufanya kazi hasa kwa wale ambao wamekwishapita ngazi nne za mwanzo za msonge wa Maslow.

Hofu juu ya wagombea huru

Kufikia hapa tumegundua kuwa kuzuia kwa wagombea huru kikatiba ni kosa.

Swali la kujiuliza ni je, ni kwanini serikali za awamu mbalimbali za CCM zimegwaya kuruhusu wagombea huru.

Ninadiriki kusema kuwa udhaifu na ubovu wa chama hicho na serikali yake ndio sababu kubwa ya kukataliwa kwa wagombea huru.

Vile vile wakati wowote ule ambao chama kinafanya maamuzi ya kiajabu ajabu na yasiyo na maslahi kwa wananchi itakuwa ni rahisi kukiacha chama na mtu kuendelea na ubunge kama mbunge asiye na chama.

Kwa chama hili ni hatari, kwa nchi hili lina faida kubwa kwa kuwa linasafisha vyama na kuwaruhusu wenye uchungu na kiu ya maendeleo ya watu wao kufanya mambo yao bila kukwaza na upofu au uziwi au au umdwebedo au ulegelege au udhaifu wa chama husika.

Wagombea huru wana hatari kubwa ya kuwa kina Slaa au Mwakyembe mara mbili ya hawa waliopo.

Isitoshe kwa wale wenye uwezo wataweza kuleta maendeleo ya haraka zaidi katika majimbo yao kiasi cha vyama vingine kutokuwa na nafasi tena ya kushinda sehemu hizo mpaka mgombea huyo aache au afe.

Wagombea huru wanaweza kuwa chachu kuu ya kufanikisha kuzima kiu ya wakazi wa mikoa mbalimbali nchini kuwa na haki na uhuru wa kusimamia na kuendesha masuala yao ya kiuchumi na kijamii katika ngazi ya mkoa jambo litakaloondosha kumaktaimu kwa mikoa kadhaa inayokwaza na urasimu na umangimeza toka makao makuu ya mptio nchini.

Wagombea huru katika kipindi hiki cha vyama vingi wataweza kutoa changamoto mbalimbali kwa vyama vya kisiasa na serikali kiasi cha kurahisisha mno watu kutofautisha kati ya chuya na mchele safi.

Nimalizie sehemu hii kwa kurudia kusema kwamba katiba kimsingi inaruhusu kuwepo kwa mgombea huru. Lakini kutokana na maslahi ya kichama, kwa bahati mbaya wabunge wa huko siku za nyuma na mahakama wameshawishiwa visivyo kuwakataa bila sababu yoyote ya msingi. Msimamo huu ni mmoja kati ya ile inayochangia kudumaza demokrasia badala ya kukuza na kuimarisha demokrasia hapa Afrika.
© 2009 Sammy W.I.Makilla

© 2009 Sammy W.I.Makilla

No comments: