Thursday, June 11, 2009

DEMOKRASIA, WANANCHI NA VYOMBO VYA HABARI

Maana ya Vyombo Huru vya Habari
Vyombo huru vya habari ni vyombo vyote vya mawasiliano ya umma na vinginevyo visivyofanya kazi kwa matashi ya mtu au kikundi fulani cha watu na vyenye kujali ukweli na uwazi katika kupasha habari na kuelimisha watu na vilevile kutoa fursa kwa watu hao kutathmini na kuona uhakika na umakini wa habari husika na kisha kufikia maamuzi kutokana na jinsi wao wenyewe walivyoamini ukweli na uwazi ni upi.

Vinatambua kwa yakini kuwa hatari kubwa zaidi ipo katika kuficha ukweli na kuwaachia baadhi ya watu kugeuza urongo kuwa ukweli.

Wanatambua kwa yakini linalohusu wananchi wote wa nchi hii ni kubwa kuliko chama au mtu yeyote. Na wanaamini wajibu wao kwanza ni kwa wananchi na sio chama au mtu fulani.
Hawakubali kurubuniwa na mtu au chama fulani, na siku zote wafanyakazi wake hujitahidi kuwa na elimu na maarifa zaidi kuliko wanasiasa au wanajamii wengine
Vyombo hivyo vinaweza kuwa redio, televisheni, magazeti au tovuti na swahiba zao. Vinaweza kumilikiwa na chama au serikali au watu binafsi. Uhuru hautokani na umilikaji wa chombo bali uhuru watendaji na waandishi wa habari walionao katika kufanya kazi zao kama taaluma zao zinavyotaka bila ya kuyumbishwa na mmilikaji.

Kwa sababu hii chombo cha habari
kinachomilikiwa na serikali au chama tawala hakiwezi kuaminiwa na kuthaminiwa kama hakiripoti ukweli na badala yake kinawasaidia walioko madarakani kuficha ukweli au kudai kuwa urongo ndio ukweli.


Kwa mantiki hii kuna vyombo vya serikali na chama vinavyoweza kuwa huru na vinavoripoti ukweli. Na wakati huo huo kunaweza kuwa na vyombo binafsi ambavyo sio huru na vinavyoficha ukweli au kuwakanganya wasomaji au wasikilizaji au watazamaji wake. Ingawa kwa kawaida hapa Afrika vyombo vingi vinavyomilikiwa na serikali (kwa kisingizio kuwa ni vya umma) au vyama vya kisiasa ni vyombo ambavyo ni vigumu kuwa huru.

Vyombo vya Habari ni uti wa mgongo wa demokrasia. Ndivyo vinavyotoa habari za kisiasa zinazowashawishi watu kuwa wapiga kura walioiva kimaamuzi. Hutufahamisha juu ya matatizo yaliyoko sehemu fulani na kupendekeza jinsi ya kuyashughulikia. Aidha ni walinzi dhidi ya maovu na mabaya yanayoweza kufanywa na wale wenye uwezo au vyeo. Hali kadhalika, vyombo vya habari vinaruhusu au kuwanyima wananchi kuendesha kwa uhuru kamili mijadala mbalimbali na kutoa fursa kwa wote kujifunza juu ya kile kinachohitajika kufanywa au kuzuiliwa kisiendelee au kisitokee. Katika enzi hizi ambazo baadhi ya vyombo vya habari vina nguvu kubwa upo pia uwezekano wa vyombo fulani kuweka ajenda wanayotaka wananchi na serikali kuizungumzia.

Ujio wa Tovuti na Blogi na sera zilizopitwa na wakati

Ujio wa Tovuti na hususan Blogi, vidaka picha kwenye kamera na ujumbe wa matini au maneno mafupi vimetoa chagamoto ya kuwepo kwa waandishi wananchi na vyombo vya habari vya wananchi ambavyo vina uwezo na uhuru mkubwa zaidi wa kuzungumzia hata yale ambayo wanasiasa na serikali wasingelipenda kuyasikia au kuona yanajulikana na watu wengine.

Kwa maneno mengine, kuwepo kwa simu za mkononi sasa hivi kunamuwezesha mwananchi kuwa na chombo binafsi cha habari na pengine anachokiamini zaidi kuliko chombo kingine chochote. Katika hali kama hii itakuwa ni kazi kweli kuwadanganya wananchi wote kwa wakati wote, ingawa, baadhi ya vyombo vitaweza kuwadanganya watu fulani kwa muda fulani. Kwa maneno mengine, kazi ya kusambaza uongo kwa vyombo vya habari na hasa vile vya chama na serikali iliyoko madarakani sasa inafikia ukomo wake.

Ni haki yetu sote kama wananchi kwa hiyo kudai kuwa lazima vyombo vya habari viwe na hulka, maadili na viwango fulani vya kufikiwa wakati wote wa utendaji kazi yao kwa kuzingatia majukumu yalyoorodheshwa hapo juu. Katika demokrasia haya ni matarajio ya msingi na halali kabisa toka kwa wananchi.

Gurevitch and Blumler (1990) wameainisha vizuri ni nini majukumu ya vyombo vya habari katika nchi ya kidemokrasia. Majukumu hayo ni pamoja na: kuangalia na kuzungumzia maendeleo ya kisiasa na kijamii; kuonesha mada moto za wakati uliopo; kuasisi majukwaa ya kuzungumzia masuala mbalimbali kutoka mitazamo na misimamo tofuati; kuwawajibisha viongozi kutokana na jinsi wanavyotumia uwezo, mali na vyeo walivyo navyo; kutoa hamasa, msisitizo, vishawishi kwa wananchi kusoma, kujifunza na kuelewa masuala mbalimbali; kuchagua; na kushiriki katika mchakato mzima wa siasa nchini; kuhimiza na kuchochea ushindani katika kila nyanja ya maisha na kuzuia kwa ukucha na jino hatua zozote zinazodhamiria kuvinyang'anya vyombo vya habari haki ya kuwa huru.

Uhuru wa Vyombo vya Habari na Demokrasia

Demokrasia katika nchi yoyote ile inakuwa pana na ya kina au finyu na ya juu kulingana na upana au kina cha uhuru wa vyombo vya habari katika nchi husika.

Kwa kujua au kutokujua viongozi wanaweza kubomoa au kujenga demokrasia kwa kutumia vizuri au vibaya vyombo vya habari. Pale vyombo vya habari vinapotumika kuwapa sauti wananchi wazungumze wao badala tu ya wao kuwasikiliza kinachosemwa na viongozi wa serikali au wa kisiasa demokrasia hujengwa. Pale vinapotumika kuwa 'laudispika' za viongozi demokrasia husinyaa na kupwaya.

Pale vyombo vya habari vinapokuwa mstari wa mbele kuwafungua watu macho na masikio juu ya udhaifu na makosa mbalimbali ya kiutawala na kiutendaji demokrasia hukua na kupanuka. Vinginevyo, huzuka jamii ya mbumbumbu wasiofikiri wala kufanya mchakato wa hoja na mawazo mbalimbali kabla ya kufanya maamuzi muhimu.

Nchi yetu haina miaka mingi toka kuanza kukubali vyombo huru vya habari. Hata hivyo dalili zilizopo hivi sasa zinaonesha tuna nafasi nzuri ya kuwa na vyombo vya habari vinavyochangia kukua na kupanuka kwa demokrasia kuliko vile vinavyohujumu demokrasia.

Hata hivyo, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali na vyama vya kisiasa au viongozi na wafanyabiashara binafsi havioneshi kuikubali ajenda ya demokrasia. Vingi kati yao vinaelekea kuwa na ajenda za kuhuisha maiti; kuita kilichooza kizima na kuita harufu mbaya harufu ya karafuu na marashi.

Hapa nchini na hata huko nje, inaelezwa kwamba, vyombo vya habari havitekelezi wajibu na majukumu yake kikamilifu. Aidha, baadhi ya vyombo vya habari ama vinatumiwa na wanasiasa au wale wenye kuvimiliki kwa malengo yao binafsi na sio kwa maslahi ya umma.

Katika hali ambayo waandishi wa habari wa vyombo vya umma na vile vya binafsi wanahofia ajira yao kama watakwenda kinyume na matakwa ya wenye vyombo hivyo kwa uhalali au kiutapeli, wao hujikuta ni mateka katika harakati binafsi au za kichama za waajiri wao.

Wachambuzi wa masuala ya vyombo vya habari wanasema kwamba vyombo vya habari ambavyo aidha vinasimamiwa na serikali au kuendeshwa kibiashara na matajiri wachache wa ndani na nje vimekuwa wakati mwingine vyombo vinavyopiga vita demokrasia kwa kujua au kutokujua.

Maudhui katika vyombo vilivyo vingi sio ya kuhabarisha na kuelimisha bali kustarehesha na kupumbaza. Umbeya, kashfa, uzushi, ngono na magomvi ndivyo vinavyopewa kipaumbele zaidi kuliko kitu kingine.

Habari nyingi za kisiasa ni za kushabikia mambo yazuykayo na yapitayo baada ya muda au za kuwahusu watu fulani kiwasifu au kutosheleza kiu yao ya kuonekana au kusikika katika jamii na sio habari zenye fikra mpya, mawazo mbadala, au utundu na ubunifu wa watu hao katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi au kuwaelekeza na kuwaongoza watu katika kutumia fursa za kiuchumi, kisiasa au kijamii zilizopo.

Nchi hazina mijadala muhimu ya kimaendeleo

Kutokana na kutokuwepo na mijadala na midahalo ya maana katika jamii panazuka matangazo ya propaganda yenye kauli mbiu na misemo isiyo na uzito wala maana yoyote katika maisha ya mwananchi. Matokeo yake wapiga kura wanachoshwa na kukatishwa tamaa na hali hii na kuwafanya waone siasa na wanasiasa kama vitu visivyo na maana katika maisha yao. Wengi huacha kabisa kupiga kura wakiwa na hakika kwamba wanajua tayari matokeo yatakuwaje.

Hali iliyofikisha Ulaya hivi leo kushuhudia chini ya asilimia 40 ya wanaostahili kupiga kura ndio tu wakijiandikisha kupiga kura na chini ya hapo kushiriki chaguzi mbalimbali ni somo zuri kwa wanasiasa wetu na waandishi wa habari kuhusu wapi wanaweza kuzifikisha nchi zao kama wakiendelea kama wanavyofanya sasa.

Vyombo vya habari huchangamkia kashfa katika maisha binafsi ya watu na kusahau kabisa kutathmini na kuhakiki sera na mapendekezo ya wanasiasa husika na yale yanayoweza kwa yakini kuleta mabadiliko katika maisha ya kiuchumi na kijamii ya wananchi.

Vyombo vya habari hukurupuka na kufanya ajali au athari ndogondogo kuwa mambo makubwa ya kututisha wakati yale yanayoweza kuwa baa au maafa makubwa yanasahaulika.

Ili kukidhi njaa yao ya fedha za kujiendesha vyombo vingi vya habari vimeamua kufumbia macho hatari za viwanda na bidhaa mbalimbali nchini japo vina hatari kubwa kwa maisha ya wanadamu. Hili ni kwa sababu tu kuwepo kwa vyombo hivyo kwa sasa kunategemea zaidi mapato kutokana na matangazo ya biashara kuliko vyanzo vingine au mauzo mengineyo.

Hata hivyo tunapozungumzia hapa demokrasia na vyombo vya habari hatuwezi kuzungumzia kila kitu.
Tutajikita zaidi katika kuona ni jinsi gani vyombo hivyo vinaweza kukuza na kupanua demokrasia au kuviza na kuifanya demokrasia kusinyaa.

Tathmini fupi ya vyombo mbalimbali

Tathmini ya haraka haraka inaonesha magazeti binafsi kwa hivi sasa yanafanya kazi nzuri zaidi katika kuelimisha watu na kukuza na kuendeleza demokrasia. Hata hivyo, redio na televisheni nyingi bado ziko nyuma katika kazi ya kuchangia kukua na kuendelea kwa demokrasia nchini. Redio na Televisheni zilizopo zinaonekana ama kuwa ubao wa matangazo wa watawala au vyombo vya kuwapumbaza wananchi wasipate muda wa kutafakari, kuchambua na kutoa changamoto za maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.

Awali watu waliamini kuwa kuwepo kwa redio na televisheni nyingi nchini kungeongeza ubora wa vipindi na maudhui ya vipindi. Kinachotokea ni kuwa sasa redio na televisheni nyingi ambazo hazijafikisha hata miaka kumi zimechoka na vipindi vyao ni rojo kuliko pale nchi ilipokuwa na televisheni na redio moja tu.

Katika miaka hii ya mtikisiko wa kiuchumi bila shaka hali itaendelea kuwa mbaya zaidi. Lawama ni kwa wamilikaji wote ambao wameamua aghalabu kuwekeza zaidi kwenye vitu badala ya kuwekeza kwenye watu.

Udhaifu uliopo

Vyombo vya habari vinakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo gharama za uendeshaji na uzalishaji, barabara mbovu, mawasiliano mabovu na ghali, umeme usioaminika, rasilimali watu duni, kodi kubwa, shikinizo za kisiasa na kadhalika.
Haya yote yanachangia katika udhaifu wa vyombo vya habari kuvifikia nchi nzima na kutumuka kikamilifu kama vyombo vya kuchochea mapinduzi ya kidemokrasia hadi vijijini.

Hili linachangia pia kwa vyombo vya habari vilivyopo kutokuwa na uhuru wa kimtaji na kifedha na hivyo kuishia kutumiwa na wachache kwenye jamii wenye ubavu wa kifedha au kisiasa. Katika hali kama hii itakuwa muhali kwa vyombo vya habari kuwa mtetezi wa umma na mpiganiaji uhuru, haki na demokrasia wa kweli kwa niaba ya wananchi.

Changamoto zilizopo

Kutokana na matatizo hayo hapo juu upo umuhimu wa kutoa changamoto la kuhamasisha magazeti ya jamii yakiwemo yale ya vijiji, miji, wilaya, mkoa na kando ili kukabili vizuizi vilivyopo hivi sasa katika vyombo vya habari na hasa magazeti kuwafikia watu kwa wakati na vile vile kuwa na habari zinazowahusu zaidi kuliko habari za maeneo na watu wengine.

Hali kadhalika, ni muhimu kwa wapenda demokrasia ndani na nje ya nchi kuvipa jamala vyombo vya habari ili viondokane na uhitaji na uwezekano wa kutumiwa kutokana na ukata wao.

Mengine ni kuangalia uwezekano wa tovuti kufika vijijini katika lugha ya kiswahili; kutangaza na kuonesha umuhimu wa elimu ya uraia na haki za kikatiba za mwananchi; kutangazia watu kuwa mfumo wa vyama vingi ni bora kuliko mfumo wa chama kimoja au demokrasia ni bora kuliko udikteta.

Hili linaenda pamoja na kuitumia teknolojia ya kisasa kufanya simu za mkononi ziendelee kuwa vyanzo nafuu vya habari za uhakika na kuaminika.

Tunayazungumzia yote haya tukitambua kuwa mawasiliano ni nishati pekee inayotoa nguvu na uwezo kwa jamii yoyote au nchi yoyote kubuni, kufikiria, kutafakari, kuamua na kutekeleza na kisha kutathmini na kuendeleza mambo mbalimbali yanayoifanya jamii au nchi kuwa siku zote katika mwendo wa kimaendeleo badala ya kukwama katika dimbwi la matatizo na kuchanganyikiwa kiuchumi na kijamii.

Hii ina maana demokrasia sio tu inachangia siasa na utawala bora bali pia nchi kuwa mstari wa mbele pia katika uchumi, sayansi, teknolojia, utamaduni, michezo na aina nyingine za maendeleo ya mwanadamu.

Kwa hiyo vyombo vya habari vikichangia maendeleo ya haki za binadamu, uhuru na demokrasia kwa watu wa sehemu fulani vinakuwa pia vinachangia maendeleo makubwa ya nchi na ulimwengu kwa ujumla.


© 2009 Sammy W.I.Makilla

No comments: