WAPO ambao kwa sababu wanazozijua wenyewe hawataki Watanzania wawe na katiba mpya. Wanadiriki kudai kwamba viraka vinavyowekwa kwenye katiba iliyopo vinatosha kabisa kukidhi haja na matakwa ya vijana wa Kitanzania leo kama ilivyokidhi haja ya Wazee wetu ambao wanatoweka kwenye safu za kisiasa na kimaisha siku hadi siku kwa kasi kubwa na ya kutisha.
Katika kukataa kwao kuwepo kwa katiba mpya wapinzani wa katiba mpya hawaonekani kuwa na hoja zaidi ya kwamba viraka vinatosheleza mahitaji na madai yote ya katiba mpya. Katika kuonesha dhahiri haja ya kuwepo kwa katiba mpya nchini mimi kama mwanaharakati wa demokrasia kwanza na pili mwanachama wa CCM (hai) na tatu Mtanzania mzalendo ninabainisha hoja kadhaa ambazo hata kwa wasiokwenda shule watazielewa na kuzikubali. Changamoto ni kwa wale wanaokataa katiba mpya kuja na hoja za kuwaaminisha wananchi vinginevyo.
Katiba si kitu cha watu wachache au chama kimoja cha kisiasa. Katiba ni makubaliano kati ya wanaotawala na wanaotawaliwa. Ni agano la watawala watawale vipi na wana haki gani kwa upande mmoja. Na upande wa pili wanaotawaliwa wana haki gani ya kuwawajibisha ikiwemo kuwaondoa madarakani wale wanaowatawala pindi inapoonekana watawala wamekosea au wameshindwa kutimiza wajibu wao.
Historia ni mwalimu tosha wa kuonesha fika kwamba nchi inapofanya mabadiliko makubwa kama yale ya kuutaliki ujamaa na kuukumbatia ubepari; kutoweka kwa waasisi wa uhuru katika medani za siasa na kuacha mfumo wa chama kimoja na kuukubali mfumo wa vyama vingi ni muhimu sana kuwa na mkataba mpya kati ya watawala na watawaliwa. Katika hali kama hii ndipo ulazima wa katiba mpya unapojitokeza.
Tuangalie hapa chini baadhi ya sababu zinazohalalisha kuundwa kwa katiba mpya itakayokubaliwa na walio wengi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katiba Ndio Kitu Pekee Kinachoweza Kubeba Mabadiliko Makubwa Leo na Kulihami Taifa na Wannanchi na Matukio Yajayo. Hili nitawaachia wataalamu kulizungumzia zaidi maana ni pana na zito sana katika maisha ya taifa na watu wake. Itosheleze tu kusema kwamba baadhi ya viongozi wetu leo wanaamini kwamba ni pale haja fulani inapoonekana, kwa mfano, matatizo ya muungano au nafasi yetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki au uporaji wa wawekezaji au kugundulika petroli ndio tu tunapohitaji kuibadili katiba. Sivyo ilivyo. Wingi wa viraka katika katiba unaonesha umuhimu na haja isiyokanushika ya kutengenezwa kwa katiba mpya. Katiba mpya inatakiwa ione mbali, itulinde na yaliyopo na yajayo na ituongoze na sio sisi tuiongoze. Haja hii sidhani inahitaji mjadala.
Nafasi ya Mgombea Huru katika Tanzania. Ingawa nchi hii inatoa haki kuwepo kwa mgombea huru lakini kutokana na matashi ya chama kimoja tu cha siasa haki hiyo haipo. Haiwezekani kuwa na katiba ambayo inaendeshwa kwa matakwa ya chama kimoja au wanasiasa fulani tu na sio matakwa ya wananchi walio wengi.
Demokrasia Dhidi ya Tabia za Kidikteta. Baadhi ya viongozi na taasisi nchini zinaonekana kuwa na uwezo wa kuweza kukataa hata yale wananchi wanayoyataka. Ikifikia hatua ya nanmna hii ni rahisi zaidi kujenga udikteta kuliko kujenga nguvu ya umma. Katiba mpya inahitajika kwa kiasi kikubwa kuzuia kuzuka kwa udikteta dhahiri na uliojificha katika nchi yetu -iwe ni kwa chama tawala au vyama mbadala vitakavyotawala siku zijazo.
Mahakama, Haki na Uwajibikaji wa Vyombo vya Kisheria. Mfumo uliopo hivi sasa hauwapi wananchi imani, maana kuwepo kwa viongozi wa juu wa mahakama badokwa kiasi kikubwa kunategemea matashi, mapendekezo na maamuzi ya mtu mmoja- iwe ni kwa sifa, upendeleo, udugu au ubinafsi wa aina hii au ile.
Upendeleo kwa Walioko Madarakni na Uonevu Dhidi ya Upinzani. Mapungufu na kasoro mbalimbali zilizopo katika katiba leo ndizo zinazochangia uchakachuaji demokrasia na kuifanya serikali iliyoko madarakani kuendelea kuwa na wabunge wengi bungeni kwa njia zilizo halali na zisizo halali pia.
Matumizi Mabaya ya Rasilimali na Maliasili za Nchi. Mfumo uliopo hivi leo unaruhusu baadhi ya viongozi na watumishi wa serikali kutumia maliasili na rasilimali kwa namna ambayo zinawanufaisha wao au chama fulani cha kisiasa. Mifano ni kama ile ya dhahabu waliyopewa Wachina kule Chunya au viwanja vya uwindaji walivyopewa wageni kule Loliondo na kwingineko au migodi ya madini waliyopewa wageni kwa bei sawa na bure.
Katiba lazima iweze sio tu kulinda maliasili na rasilimali zetu bali pia kuhakikisha kwa mapana na marefu yake vitu hivyo vinawanufaisha Watanzania zaidi kuliko wageni. Mathalani, katika madini Tanzania ingeliweza kukodi mitambo, wataalamu na vifaa vingine toka nchi za Ulaya Mashariki ya zamani au Afrika Kusini na kuchimba dhahabu yake wenyewe badala ya kuwapa wageni kwa kiasi cha mrabaha duni kama kilichokubalika kwa sheria zilizosababishwa na mapungufu ya kikatiba.
Katika kuongelea rasilimali za nchi ni wazi pia kwamba Benki Kuu na Hazina viko wazi kwa yeyote aliyeko madarakani kuchota chochote kilichomo humo bila ya katiba iliyopo kuwakamata na kuwawajibisha. Katiba mpya inahitajika ili kuhakikisha kilichopo Benki Kuu na Hazina bila kujali ni chama gani au kiongozi gani yuko madarakani. Vinginevyo, iko siku tutakuta Benki Kuu na Hazina kweupe na hakuna wa kuwajibishwa.
Upuuzaji na Udhalilishaji wa Rasilimali Watu Wazawa. Katiba iliyopo inazungumzia zaidi haki na usawa wa rasilimali watu. Lakini hakuna lolote la maana juu ya kuendeleza rasilimali watu na kuthamini rasilimali yetu kuliko fedha za wageni na mashine zao. Matokeo yake, Mtanzania miaka hii ya 2010 hathaminiwi na serikali yake na hathaminiwi na wageni wanaowekeza nchi hii. Angalia mishahara ya Mtanzania ukilinganisha na ya wageni au fidia Mtanzania anapopata ajali au huduma mbalimbali Mtanzania anazoahidiwa lakini hazipati kabisa au hazipati kwa ubora unaokubalika.
Kuzuka kwa Ukabila wa Kichama. Katiba iliyopo inaruhusu chama tawala kuwapa wanachama wake tu (hata wakiwa hawana uwezo) nyadhifa zote za uongozi ikiwemo uwaziri, ukuu wa mikoa, ukuu wa wilaya, ukuu wa mashirika na taasisi mbalimbali. Zanzibar inatufundisha kwamba upinzani nao unaweza ukawa na viongozi bora sawa au kuliko wale wa chama tawala. Tujifunze toka kwao. Hali ya chama kimoja tu kutoa viongozi kwa nchi nzima ni kosa. Ni hali inayojenga tunaouita UKABILA WA KICHAMA. Kama ulivyo ukabila mwingine, ukabila huu una hatari ya kubomoa zaidi ya kujenga.
Matumizi Mazuri ya Misaada Toka Nje. Tunahitaji pia katiba mpya ili tujadili pia misaada toka nje na jinsi inavyoweza kuiondoa nchi kwenye umaskini baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa takriban miaka 50 sasa. Kuna wanaoamini misaada sasa inafanana na kuwapa watu samaki badala ya kuwapa nyavu wakavue wenyewe. Na wengine wanaamini kinachopewa serikali kingi zaidi kinapotea kwenye mifuko ya wanasiasa kuliko kile kinachotumika katika kuwaondoa wananchi toka kwenye umasikini.
Kujikita Vizuri Katika Dunia ya Utandawazi. Sio tu Katiba yenu ina mapungufu makubwa ya siasa za nje, hali tunajua ni muhali kuendelea bila kutumia vyema ushirikiano wetu na nchi zinazotuzunguka na zile za mbali. Bali kubwa zaidi Tanzania kikatiba haina lolote juu ya kujilinda na kunufaika na utandawazi. Siasa za nje zilizomo mle ni zile za enzi za Vita Baridi na Nchi Zisizofungamana na upande wowote.
Kujikita Ipasavyo Katika Teknohama na Teknolojia Mpya. Ingawa Tanzania ndiyo ya kwanza kukumbatia Tekhohama hapa Afrika Mashariki leo ndio ya mwisho ila kwa simu za mkononi tu. NI dhahiri Katiba isiyo na upeo juu ya masuala kama haya (angalia wizi wa kutumia Teknohama katika mabenki) imechangia kwa kiasi kikubwa kutufanya tuwe wa mwisho na kupitwa na nchi ndogo kama Rwanda. Kwa kuzingatia Teknohama (ICT) ndio dunia ya kesho, na dunia ya kesho ni Teknohama ni muhimu tukawa na katiba inayoendana na enzi na miaka ya Teknohama na sio vinginevyo.
Teknolojia, Utengenezaji Mitambo Yetu na Maendeleo ya Viwanda. Ujenzi wa viwanda na ubunifu katika kuunda na kutengneza teknolojia na vifaa vyetu vyenyewe ni kitu adimu katika katiba iliyopo. Hatuwezi kuzungumza juu ya viwanda na teknolojia kama Waswahili kwenye kijiwe cha kahawa na kisha tukaendelea kikwelikweli. Ni lazima hili liwemo katika katiba likisaidiwa na mikakati ya kulifanikisha katika vitendo sasa na baadaye. Si vigumu kuelewa kwamba Tanzania hivi leo tunatumia kwa asilimia kubwa vitu na vifaa vilivyotengenezwa nje, japo kuna vingi tunavyoweza kuvitengeneza hapa hapa nchini na kubadili kabisa hali yetu ya kiuchumi. Sera peke yake hazitoshi. Tunahitaji Katiba Mpya kuzipa sera hizo ndimi, meno na makucha. Hatuwezi katu kuendelea kama viwanda, barabara, mifumo ya maji na umeme na kadhalika vitaendelea kutegemea mitambo na mashine toka nje badala ya sisi kuvitengeneza sisi wenyewe. Katiba mpya inahitajika kutunusuru na kuwa taifa la wachuuzi na wanunuzi wasiotengeneza chochote kile wanachokitumia wao wenyewe.
Umaskini kama karata turufu ya watawala. Yapo madai kwamba wanasiasa wa nchi yetu hawawezi kabisa kuruhusu umaskini utoweke maana kwa kufanya hivyo mtaji unaowasaidia kurudi madarakani kila baada ya miaka mitano hautakuwepo. Kwa maneno mengine, serikali na wanasiasa wanafanya mbwembwe tu kupiga makelele kuwa wanapiga umaskini vita. Ukweli ni kuwa wanapigania umaskini kuendelea kuwepo milele ili na wao watawale wajinga na wenye njaa milele.
Nafasi ya Lugha ya Kiswahili katika Maendeleo ya Nchi. Hivi sasa kuna baadhi yetu baada ya miaka 50 ya Uhuru wakingali wanaamini kwamba nchi yetu itaendelea kwa kutumia lugha za kigeni na hususan ile ya Kiingereza.
Hata hivyo, kuna waliofunguka macho ambao wanajua fika kwa kutumia Kiingereza kila tunalopangwa litapanguliwa tu hatimaye. Na kama walivyofanya ndugu zetu wa Kichina, Kikorea, Kihindi, Wajapani, Waindonesia, Wamalaysia, Kiarabu ni lazima tutumie lugha yetu wenyewe ili tukwepe kuvurugwa na Waingereza wa sasa na wa kesho.
Ipo haja pia kwa wale wote wanaotaka kuanzisha shule za chekechea, msingi, sekondari na Vyuo Vikuu vinavyotumia lugha ya Kiswahili kuruhusiwa kufanya hivyo na katiba na hivyo kuepuka mizengwe wanayofanyiwa sasa na serikali ambayo kwa kiasi kikubwa bado inaonekana kuabudu Uzungu na hususan Uingereza na kudharau lugha yetu wenyewe ya Kiswahili.
Isitoshe katika miaka na karne hii, shule na vyuo viwe huru kutumia Kiarabu au Kichina au Kijapani au Kihindi au Kiswahili (lugha za nchi zinazoendelea kwa kasi zaidi) badala ya kila shule au chuo kulazimishwa kutumia Kiingereza.
Kutekwa Nyara kwa Mjadala wa Katiba. Upo uwezekano mkubwa pia kwamba jambo hili la uundwaji wa Katiba Mpya lisipofanyika hivi sasa upo uwezekano mkubwa wa Chama Tawala kuteka mjadala na uundaji wa Katiba mpya. Hili ni dhahiri kwa kuzingatia pia kuna wafadhili ndani na nje ya nchi ambao wako tayari kufadhili kazi hii.
Na ndivyo ilivyo kwa Kilimo cha zamani, Kilimo ni Uhai, Kilimo cha Umwagiaji, Kilimo Kwanza na Kilimo "Kijacho" -bila Katiba kuwa na mashiko yenye dhamira na nia ya kweli ya kubadili hali za watu wetu, tutaendelea kuwa watu wa maneno na nyaraka nzuri lakini wafupi katika vitendo na mafanikio yetu.
Nafasi ya Mikoa Huru Kiuchumi na KIjamii. Kasoro kubwa katika muundo wa nchi yetu ni ule unaojitokeza pale ambapo watu chini ya laki nne wanapopiga kura kuchagua rais, wabunge/wawakilishi na baadaye baraza la mawaziri kwa eneo moja la Tanznia-Tanzania Visiwani. Lakini mkoa wenye wapiga kura zaidi ya milioni hauna nafasi ya kumchagua yule anaouongoza mkoa achilia mkoa huo kuwa na wajumbe na baraza lake la mawaziri, ingawa huu ndio muundo unaoonekana una nafasi kubwa zaidi ya kututoa toka kwenye umaskini kuliko ule uliopo hivi sasa. Ni dhahiri katiba mpya inahitajika ili kurekebisha hali hii.
Kutambulika na kukubalika Nafasi ya kila Mtu na Kila Chombo katika Taifa. Hivi leo nafasi ya mtu katika eneo moja la nchi inaweza ikaingiliwa na mwingine eti tu kwa sababu mtu huyo yuko Wizarani au Ikulu. Hili si sawa. Hali kadhalika, ni dhahiri kuwa vyombo vya dola kama vile polisi, jeshi na usalama wa taifa vinaweza vikaingilia kazi za taasisi zingine ama kwa ridhaa ya vyombo hivyo au kwa kulazimishwa na kiongozi fulani au chama fulani. Mwanzo wa mwisho wa demokrasia huanza pale vyombo vya dola visipotambua nafasi yao katika taifa linaloamini na kufuata demokrasia ya kweli.
Monday, December 20, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment